Afisa Wa Elimu Zanzibar Bw Suleiman Yahya Ame kulia, akionesha makala ya kitabu. |
Na Abou Shatry Washington DC
Jumuiya ya Wazanzibari waishio Nchini Marekani (ZADIA), imepongezwa kwa kusaidia gurudumu la maendeleo ya Elimu visiwani Zanzibar.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Elimu ya Juu Zanzibar Bw. Suleiman Yahya Ame wakati wa kupokea mchango wa vitabu vya Ufundi na Mafunzo ya Amali uliotolewa na ZADIA kwa ajili ya shule za ufundi visiwani humo.
Akizungumza kama mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika mjini Zanzibar, Bw. Ame pia aliwashukuru Wanadiaspora hao kwa kuendeleza juhudi za kujenga jamii iliyoelimika Zanzibar.
Aliendelea kusema "Tukiwa na mahitaji makubwa ya vitabu katika shule zetu, vitabu hivi vimewasili katika wakati mwafaka, na tunashukuru kwa msaada huu", na kungoeza kuwa juhudi kama hizi zitasaidia kuigeuza Zanzibar kuwa jamii inayojitosheleza kiajira.
Alizitolea wito shule zilizofaidika na vitabu hivyo kuvitumia vizuri kwa lengo la kuisaidia Zanzibar kufikia malengo yake ya kielimu.
Bwana Ame alimalizia kwa kuitolea wito ZADIA kupanua zaidi mfumo wa misaada yake ya kielimu na kujumuisha ujenzi wa madarsa na vitabu vya taaluma nyengine ambazo Zanzibar ina upungufu mkubwa, kama vile taaluma ya Fedha na nyenginezo.
Naye Mwenyekiti wa ZADIA Bwana Omar Haji Ali, alisisitiza azma ya Jumuiya yake ya kuendeleza juhudi za kusaidia maendeleo Zanzibar.
Katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na mwakilishi wa ZADIA Zanzibar Bwana Mussa Shehe kwenye hafla ya makabidhiano ya vitabu hivyo, Bw. Ali alisema "ZADIA, tangu kuanzishwa kwake imekuwa msitari wa mbele katika harakati za kusaidia maendeleo Visiwani Zanzibar katika nyanja tofauti"
Aliendelea kutamba kwa kusema kuwa, "Kwa vile ZADIA inaelewa kuwa daima maadui wakubwa wa maendeleo ya jamii wamekuwa wakivinjari kuzorotesha maendeleo hayo, basi jeshi letu siku zote liko imara kupambana na maadui hao ambao ni maradhi, ujinga na umaskini, na kuhakikisha kuwa milele hawatothubutu kujaribu kuyachokoza maendelea ya Wazanzibari.
Aidha, Bwana Ali alisisitiza kuwa msaada huo wa vitabu siyo mwisho wa juhudi za ZADIA katika kusaidia sekta ya Elimu Zanzibar, bali ni mwendeleo wa mapambano dhidi ya adui ujinga.
Alielezea matumaini yake kuwa msaada huu utakuwa ni changamoto kwa jumuiya nyengine za Wazanzibari ulimwenguni kushiriki katika kusaidia maendeleo Zanzibar.
Bwana Omar aliwashukuru WanaZaida wote walioshiriki katika kufanikisha msaada wa vitabu hivyo, pamoja na shirikika la Goodheart-Willcox la nchini Marekani kwa ukarimu wao.
Hafla hiyo ya makabidhiano ya vitabu, pia ilihudhuriwa na maofisa wa ngazi za juu kutoka Wizara ya Elimu Zanzibar, Maofisa wa Idara ya Diaspora katika Ofisi ya Rais wa Zanzibar, wawakilishi wa Vyuo vilivyokusudiwa kufaidika na msaada huo pamoja na wawalikishi wa vyombo mbalimbali vya habari vilioko Zanzibar.
No comments:
Post a Comment