Maisha : Wizara, yakemea vitendo vya ukeketaji wanawake nchini - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


6 Feb 2017

Maisha : Wizara, yakemea vitendo vya ukeketaji wanawake nchini




Kaimu Mkurugenzi wa Maendeley ya Jinsia Bwana Julius Mbilinyi pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto Bi. Margaret Mussai k akifafanua jambo mbele ya waandishi wa habari hawapo pichani kughusu siku ya kimataifa ya kuzuia ukeketaji
-------------------------------------------------------

Masuala ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ukeketaji yameendelea kuwa tatizo kwa taifa na ulimwengu mzima na ili kukabiliana na tatizo hili, kumekuwa na mwitikio mkubwa wa kimataifa na kitaifa katika kukabilana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.


Akiongea na vyombo vya Habari Jijini Dar es Salaam leo Kaimu Mkurugenzi Idara ya Watoto wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Margaret Mussai amesema Serikali inalaani na kukemea vikali ukatili kwani unadhalilisha na kunyanyasa hadhi na utu wa mwanamke na mtoto wa kike akisema jambo hili halikubaliki.


Aidha aliongeza kuwa ni lazima jitihada za makusudi zichukuliwe na wadau wote kuhakikisha kuwa tunashiriki kwa pamoja kuzuia na hatimaye kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii zetu, hususan kuzua ukeketaji.


Aidha kulingana na takwimu za Tafiti ya Idadi ya Watu na Afya (TDHS 2010) inakadiriwa kuwa ukeketaji kwa wasichana na wanawake wenye umri wa miaka 15- 49 ni asilimia 14.6, hii imepungua kidogo ukilinganisha na asilimia 17.9 mwaka 1996. Aidha, takwimu hizo kwa mwaka 2015/16 zinaonyesha kiwango cha ukeketaji kwa wanawake na watoto kimepungua kutoka asilimia 14.6 ya mwaka 2010 hadi kufukia asilimia 10.


Margaret ametaja mikoa inayoongoza kwa vitendo vya ukeketaji ni Manyara (58%), ikifuatiwa na Dodoma (47%) na Arusha (41%) akitaja kuwa kupunguwa kwa vitendo vya ukeketaji kunatokana na kampeni za uhamasishaji, uelewa na kujitambua kwa wasichana wanaofanyiwa vitendo hivyo, hofu ya kufungwa kutokana na uwepo wa sheria zinazotekelezwa, hivyo mangariba na wazee wa kimila kwa kiasi kikubwa wanaamua kuacha mila hii ya ukeketaji.


Aidha Serikali inahimiza kuendeleza mila zenye manufaa na kujenga utamaduni chanya kwa jamii. Amewaomba wadau mabalimbali wakiwemo wana habari, mashirika yasiyo ya kiserikali, Taasisi za dini, sekta binafsi na mamlaka za serikali za mitaa kuendelea kuongeza juhudi za kuelimisha jamii kuachana na mila zinazochochea ukeketaji.


Aidha Serikali imetunga sera, sheria, miongozo na kuandaa mikakati mbalimbali katika jitihada za kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia,ikiwemo ukeketaji, Sera ya Wanawake na Maendeleo ya Jinsia (2000) na Mkakati wa Maendeleo ya Jinsia (2005), Sera ya Maendeleo ya Mtoto (2008). Sheria ya Makosa ya Kujamiiana -SOSPA (1998) na Sheria ya Mtoto (2009) vyote vikiwa na lengo la kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Katika kuongeza jitihada za kutokomeza ukeketaji serikali imeandaa Mpango wa kazi wa Taifa wa miaka mitano wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (2017/18-2021/22). Mpangokazi umeanisha maeneo nane muhimu mojawapo ni la kuondoa mila na desturi zenye madhara. Kupitia mpango huu serikali imedhamiria kupunguza ukeketaji kwa wanawake kwa asilimia 50ifikapo mwaka 2022.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad