MAKALA :Uchumi wa Nyuklia: Uchambuzi wa akiba ya urani ya Mkuju na maono ya Rais Samia ya kinu cha kwanza mwaka 2029 - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Wednesday, 10 June 2026

MAKALA :Uchumi wa Nyuklia: Uchambuzi wa akiba ya urani ya Mkuju na maono ya Rais Samia ya kinu cha kwanza mwaka 2029

 



Na Beda Msimbe, TBN, aliyekuwa Urusi

Kwa miaka mingi, mazungumzo kuhusu nishati nchini Tanzania yamekuwa yakitawaliwa na vyanzo vya maji, gesi asilia, na sasa nishati jadidifu kama jua na upepo. 

Hata hivyo, kauli ya hivi karibuni ya Rais Samia Suluhu Hassan akiwa nchini Urusi imethibitisha kuwa Tanzania sasa imedhamiria kuingia kwenye Klabu ya Nyuklia ifikapo mwaka 2029. 

Hili si jambo la kubahatisha bali ni mkakati unaoendeshwa na uwepo wa akiba kubwa ya madini ya urani katika Bonde la Mto Mkuju mkoani Ruvuma, mradi unaosubiriwa kwa hamu kubwa kuwezesha fursa ya maendeleo. Mkakati huu unalenga kuipa nchi vyanzo mbadala na imara vya nishati ili kukabiliana na changamoto za kukatika kwa umeme na kukua kwa kasi kwa sekta ya viwanda.

Historia ya mradi wa urani wa Mkuju River uliopo ndani ya mfumo wa ikolojia wa Selous na Nyerere kusini mwa Tanzania inaonyesha kuwa unatajwa kuwa miongoni mwa hifadhi kubwa zaidi za urani ambazo hazijachimbwa duniani kote.

Mradi huu unamilikiwa na kampuni ya Mantra Tanzania, ambayo ni kampuni tanzu ya Uranium One inayomilikiwa na Shirika la Nishati la Atomiki la Urusi liitwalo Rosatom. 

Ugunduzi wa madini haya ulileta matumaini makubwa tangu miaka ya 2010 ambapo tafiti za kijiolojia zilionyesha kuwa eneo hilo lina hifadhi inayokadiriwa kufikia tani milioni 152 za miamba yenye madini hayo inayoweza kuzalisha mamilioni ya ratili za urani iliyosafishwa kwa kiasi fulani kwa miaka zaidi ya 12 hadi 20 ya uhai wa mgodi huo.

Hata hivyo, mradi huo ulikabiliwa na changamoto mbalimbali zilizosababisha usitishwaji wa muda ikiwemo kuanguka kwa bei ya urani duniani baada ya ajali ya nyuklia ya Fukushima nchini Japani mwaka 2011. 

Mahitaji ya urani duniani yalishuka sana na kupelekea bei kuporomoka hali iliyofanya uchimbaji wa Mkuju kutokuwa na tija ya kibiashara kwa wakati huo. 

Changamoto nyingine ilikuwa ni mazingira na udhibiti kwa kuwa eneo la mradi lilikuwa ndani ya Hifadhi ya Selous ambayo ni eneo la Urithi wa Dunia, jambo lililolazimisha serikali kufanya mabadiliko ya mipaka ili kuruhusu uchimbaji bila kuathiri ikolojia nzima ya eneo hilo.

Baada ya usingizi wa muda mrefu, mradi wa Mkuju sasa unafufuka kwa kasi kubwa kutokana na kupanda upya kwa bei ya urani duniani na msukumo wa kisiasa kutoka kwa serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kwa sasa, Mantra Tanzania na Uranium One wamekamilisha hatua za majaribio ya teknolojia ya uchenjuaji iitwayo In-Situ Recovery au majaribio ya kinu cha majaribio. 

Teknolojia hii ni ya kisasa na salama zaidi kimazingira kwani haihusishi kuchimba mashimo makubwa bali huingiza vimiminika maalum ardhini vinavyoyeyusha urani na kuivuta juu ikiwa kimiminika.

Mazingira ya sasa yanaonyesha kuwa miundombinu ya msingi ikiwemo barabara za kuingia eneo la mradi, mifumo ya ulinzi wa mionzi, na kambi za wafanyakazi zimeshaimarishwa huku serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania ikifanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha usalama wa mionzi unazingatiwa kabla ya uchimbaji kuanza kikamilifu.

Ukimya wa miaka kadhaa uliacha maswali mengi lakini sasa wananchi na wadau wa kiuchumi wanasubiri kwa shauku kubwa kuanza kwa mgodi huu kwa sababu ya fursa za ajira na uchumi wa ndani. 

Wakazi wa mikoa ya Kusini hasa Ruvuma na Lindi wanatarajia fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja pamoja na kukuza biashara za ndani kupitia usambazaji wa bidhaa mgodini. 

Mradi huu pia unatajwa kuwa chanzo kipya na kikubwa cha mrabaha na kodi kwa serikali utakaosaidia kufadhili miradi mingine ya kijamii kama afya na elimu huku kukiwa na matumaini ya uhuru wa nishati kwani kauli ya Rais Samia kuwa urani hii itatumiwa kuzalisha umeme nchini inaleta matumaini mapya kuwa Tanzania haitakuwa tu msafirishaji wa mali ghafi bali itakuwa mtumiaji wa mwisho wa teknolojia hiyo.

Uthibitisho mkubwa zaidi unaoonyesha kuwa Tanzania inaenda kuwa na kinu cha nyuklia kwa siri na umakini mkubwa ni kuwepo kwa mkataba wa faragha ambao unazuia pande mbili yaani Shirika la Umeme Tanzania na Shirika la Rosatom la Urusi kusema chochote wakati wa mazungumzo mpaka yafikie mwisho. 

Wataalamu wa sekta ya nishati na sheria nchini wameeleza kuwa mkataba huu wa kisheria wa kutosambaza taarifa ni wa kawaida lakini wa kiwango cha juu sana unapohusisha masuala nyeti ya usalama na nishati ya kimkakati kama nyuklia. 

Siri hii kubwa inalinda maslahi ya taifa na kuzuia kuingiliwa kati kwa mazungumzo hayo na mataifa mengine au washindani wa kijiografia kabla ya makubaliano kamili kukamilika. 

Hatua hii ya usiri inatafsiriwa na wachambuzi kama ishara ya wazi kwamba pande zote mbili ziko katika hatua za mwisho za kiufundi na kisheria kufanikisha ujenzi wa kinu hicho bila kuleta taharuki.

Ili kufikia maono ya mwaka 2029 ya kuwa na kinu cha nyuklia, Tanzania inakabiliwa na kibarua kizito cha kujenga udhibiti madhubuti wa kisheria na kitaalamu. 

Rais Samia akizungumza na waandishi wa habari mjini St Petersburg, Urusi wakati akihudhuria Jukwaa la Uchumi la Kimataifa la Petersburg, alibainisha kuwa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania sasa itakuwa na kazi kubwa inayohusiana na masuala ya matumizi ya nyuklia kwa amani kama inavyoelekezwa na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki. 

Ushirikiano mpya na Urusi hautalenga tu kununua mitambo bali kuhamisha teknolojia kwa kutoa mafunzo ya wahandisi wa kiasili yanayofadhiliwa kwa sasa nchini Urusi, jambo ambalo ni la msingi sana kwani usalama wa kinu cha nyuklia unategemea kwa asilimia mia moja uwezo, maarifa, na umakini wa wanadamu wanaokiongoza.

Wataalamu wa nishati kutoka serikalini wanasisitiza kuwa hatua hii ya sasa ya kimkakati itaiwezesha nchi kuwa na uhakika kamili wa nishati ya viwanda ambayo haitayumba kutokana na mabadiliko ya tabianchi kama ilivyo kwa nishati ya maji. 

Kauli za wataalamu hao zilianikizwa na Rais Samia Suluhu Hassan aliyesema jwamba ni lengo la serikali kuwa na taifa ambalo linazalisha jumla ya megawati 8000 ili kuwa na ziada ya uhakika ya kuuza nchi za nje.

Mazungumzo yanayoendelea chini ya mkataba wa faragha yanalenga kuhakikisha kuwa ujenzi wa kinu hicho unazingatia viwango vyote vya kimataifa na gharama zinazohimilika kwa uchumi wa Tanzania. 

Hii inaonyesha kuwa serikali haikurupuki bali inasonga mbele kwa hatua madhubuti zilizofanyiwa utafiti wa kina ili kulinda maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.

Safari ya kuelekea mwaka 2029 imeshaanza kwa kasi kubwa na ya kimyakimya chini ya usimamizi thabiti Rais Samia Suluhu Hassan ambapo ziara yake nchini Urusi pamoja na kuwa na mafanikio makubwa kisiasa na kiuchumi, imewezesha kuwepo kwa mikataba ya makubaliano kadha yanayogusa teknolojia ya nyukilia.

Urani ya Mkuju si hadithi tena ya madini yaliyolala ardhini bali ni mtaji wa kimkakati unaokwenda kubadilisha kabisa ramani ya nishati katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na Kati. 

Kama ahadi ya Rais Samia itatimizwa na mazungumzo ya siri yaliyopo sasa yakazaa matunda yaliyokusudiwa, ifikapo mwaka 2029 moshi na mwanga kutoka kwenye kinu cha kwanza cha nyuklia cha Tanzania utakuwa ndio ushahidi tosha wa nchi iliyoamua kuikumbatia nishati ya kesho kwa ajili ya maendeleo endelevu ya leo.

No comments:

Post a Comment