Nishati : TANESCO Yazindua Mpango wa Mikopo ya Majiko ya Umeme na Vituo vya Kuchaji Magari ya Umeme - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Friday, 12 June 2026

Nishati : TANESCO Yazindua Mpango wa Mikopo ya Majiko ya Umeme na Vituo vya Kuchaji Magari ya Umeme


Na Janeth Raphael MichuziTv 

Serikali imezindua rasmi mpango wa ukopeshaji wa majiko ya umeme kwa wateja wa TANESCO pamoja na mradi wa vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme, hatua inayolenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi, kupunguza gharama za maisha kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya utekelezaji wa mpango huo iliyofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Nishati,  Deogratius Ndejembi (Mb.), alisema miradi hiyo ni sehemu ya matokeo ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika sekta ya umeme na kwamba sasa wananchi wanaanza kunufaika moja kwa moja na maboresho hayo.

Amesema matumizi ya umeme katika kupikia na usafiri yatawezesha familia nyingi za Kitanzania kupunguza matumizi ya fedha kwa ajili ya nishati, kuongeza muda wa kufanya shughuli za maendeleo na kuboresha mazingira ya maisha kutokana na matumizi ya nishati safi.

Waziri Ndejembi ameeleza kuwa Serikali inaona matumizi ya umeme katika sekta hizo kama njia muhimu ya kuongeza matumizi yenye tija ya umeme unaozalishwa nchini, kuongeza mapato ya TANESCO, kuvutia uwekezaji mpya na kuimarisha shughuli za kiuchumi.

Aidha, alisema hatua hiyo itafungua fursa mbalimbali za kiuchumi kwa vijana, wanawake na sekta binafsi kupitia biashara za usambazaji wa vifaa vya nishati safi, huduma za teknolojia, matengenezo ya vifaa vinavyotumia umeme pamoja na uwekezaji katika miundombinu ya kuchajia vyombo vya usafiri vya umeme.

"Hii ndiyo Tanzania tunayoijenga, Tanzania inayotumia rasilimali zake kuleta maendeleo kwa wananchi wake na inayokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia duniani," alisema Waziri Ndejembi.

Katika kuhakikisha mpango huo unaleta matokeo yaliyokusudiwa, Waziri huyo aliiagiza TANESCO kuhakikisha huduma ya mikopo ya majiko ya umeme inawafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo yote ya nchi, mijini na vijijini, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza elimu kwa umma kuhusu faida za matumizi ya umeme katika kupikia na matumizi sahihi ya vifaa vinavyookoa nishati.

Pia alitaka vituo vya kuchajia vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme vijengwe kwa wakati na kutoa huduma za uhakika kwa wananchi, huku ushirikiano kati ya TANESCO na sekta binafsi ukiendelea kuimarishwa ili kuongeza uwekezaji katika teknolojia za nishati safi.

Waziri Ndejembi aliwataka wananchi kuchangamkia fursa ya mikopo ya majiko ya umeme, akieleza kuwa masharti yaliyowekwa ni nafuu na rahisi kufikiwa na wengi. Alisema anayehitaji kunufaika na mpango huo anatakiwa kuwa mteja wa TANESCO, awe mmiliki wa nyumba anayenunua umeme mara kwa mara na awe na mita yenye taarifa zinazolingana na Kitambulisho cha Taifa (NIDA).

Katika hatua nyingine, alisema TANESCO itatoa huduma ya kuchaji vyombo vya usafiri vinavyotumia umeme bila malipo kwa siku 30 za mwanzo tangu kuanza kwa huduma hiyo ili kuwapa wananchi nafasi ya kuifahamu na kuitumia teknolojia hiyo mpya. Baada ya hapo, gharama zitakazotozwa zitakuwa nafuu na zinazoweza kumuduwa na wananchi wengi.

Kwa upande wa sekta binafsi, Waziri huyo alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika teknolojia za nishati safi ili kuongeza ushiriki wa wawekezaji katika kuendeleza sekta ya nishati na kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea matumizi makubwa ya nishati safi na uchumi wa kisasa.

Uzinduzi wa miradi hiyo unaashiria hatua mpya katika juhudi za Serikali za kuhamasisha matumizi ya umeme katika maisha ya kila siku ya Watanzania, huku ukitarajiwa kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi na kuchangia maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi nchini.






No comments:

Post a Comment