Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Erasimus Rugarabamu wakati akifungua kikao
kazi cha wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii kwa niaba ya Katibu Mkuu
wa Wizara hiyo Bi.Sihaba Nkinga mjini Dodoma.
Baadhi
ya Wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii wakifuatilia mada zilizokuwa
zikiwasilishwa wakati wa Kikao kazi chao mjini Dodoma leo.
Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Erasimus Rugarabamu (katikati) akiwa na Kaimu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii wa Wizara hiyo Bw. Enterberth Nyoni
(wa pili kushoto) na Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii
vilivyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na
Watoto Bw. Paschal Joseph Mahinyila wakifuatilia michango mbalimbali ya
wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao kazi cha wakuu hao
leo mjini Dodoma.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo akichangia jambo.
Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Bw.Erasimus Rugarabamu (katikati mstari wambele)
akiwa katika picha ya pamoja na wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini
mjini Dodoma mara baada ya kufungua kikao kazi cha wakuu hao kwa niaba
ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi.Sihaba Nkinga.
Na. Aron Msigwa - Dodoma.
Serikali
imewataka Wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kufanya kazi kwa
kuzingatia weledi , kanuni, miongozo na taratibu zinazosimamia
uendeshaji wa vyuo hivyo ili kuiwezesha sekta hiyo kupiga hatua kwa
kuzalisha wataalam wenye sifa wanaokidhi matarajio ya wananchi.
Kauli
hiyo imetolewa leo mjini Dodoma na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali
watu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Bw.Erasimus Rugarabamu wakati akifungua kikao kazi cha wakuu wa vyuo vya
Maendeleo ya Jamii kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bi.Sihaba
Nkinga.
Bw.
Rugarabamu amewataka wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kuendelea
kusimamia kwa umakini mkubwa wa Rasilimali za vyuo hivyo na kubainisha
kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua za kinidhamu na kisheria kwa mkuu
wa Chuo yeyote atakayeshindwa kuzingatia weledi , sheria, kanuni na
taratibu zinazosimamia uendeshaji wa vyuo hivyo.
"
Ninyi ndio wasimamizi wa uzalishaji wa wataalam wa Maendeleo ya Jamii
nchini, mnao wajibu wa kubadilisha fikra za wananchi na kuwa chachu ya
maendeleo, hakikisheni mnasimamia vizuri suala la udahili wa wanafunzi
kwa kuwa na wanafunzi wenye sifa.
Aidha,
amewataka wakuu hao wa vyuo kuhakikisha kuwa wanapiga vita kwa vitendo
udahili wa vyeti vya kughushi ( vyeti feki) akisisitiza kuwa Serikali
haitasita kuchukua hatua za kisheria na kinidhamu kwa Mkuu wa Chuo
yeyoye atakayehusika kwa namna moja au nyingine kusaidia udahili wa
wananfunzi wasio na sifa.
Ametoa
wito kwa wakuu na Wakuu wa taaluma wa vyuo hivyo kuwa makini katika
suala la udahili wa wanafunzi wanaojiunga katika fani ya maendeleo ya
jamii ili kuendelea kujenga heshima ya taaluma ya Maendeleo ya Jamii na
kutimiza matarajio ya kuwaletea maendeleo wananchi.
"
Hakikisheni mnaepuka maslahi binafsi katika usimamizi wa taaluma, suala
la vyeti feki lisiwe na nafasi katika vyuo vyetu, fanyeni kazi kwa
kuzingatia sheria ili tuendelee kutoa wahitimu bora" Amesisitiza
Rugarabamu.
Katika
hatua nyingine amewataka wakuu hao kuwa wabunifu ili vyuo
wanavyovisimamia viweze kuhimili soko la ushindani kutoka vyuo vingine
vya elimu ya Maendeleo ya jamiii hapa nchini ili vyuo chini ya wizara,
viweze kutekeleza majukumu kwa ufanisi na kuzalisha wataalam wanaokidhi
mahitaji ya soko.
" Ili
vyuo vyetu viendelee kuonekana lazima viweze kuhimili ushindani kutoka
katika vyuo vingine vinavyotoa taaluma kama hii, jambo hili lazima
tulifanye kwa nguvu ili tuendelee kuwa wazalishaji bora wa wataalam wa
elimu ya Maendeleo ya Jamii hapa nchini" Amesisitiza Rugarabamu.
Aidha,
ametoa wito kwa wakuu hao kusimamia vizuri rasilimali za fedha na
kufafanua kuwa suala la upimaji wa Wazi wa watumishi wa Umma (OPRAS)
lazima lizingatiwe na watumishi wote wa vyuo hivyo kwa kuwa wao ni
watumishi wa umma lazima wapimwe utendaji kazi wao kwa mujibu wa vigezo
vilivyowekwa.
Aidha,
amewataka Wakuu hao kuhakikisha kuwa wanavisimamia vyuo wanavyoviongoza
kwa mujibu wa sheria na kuhakikisha kuwa wanawasilisha taarifa kuhusu
maendeleo ya vyuo vyao kwa lengo la kuiwezesha Serikali kuchukua hatua
za katika maeneo ambayo hayaendi vizuri kuviwezesha vyuo hivyo kupiga
hatua kitaaluma.
Awali
akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa
Maendeleo ya Jamii wa Wizara hiyo Bw. Enterberth Nyoni amesema kuwa
Mkutano huo ni muhimu sana kwa kuwa umewakutanisha wakuu wa Vyuo na
Makamu Wakuu wa Vyuo wanaozalisha Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini
ambao huajiliwa na Serikali katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, taasisi
na Mashirika mbalimbali.
Amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo kuna umuhimu mkubwa katika
maendeleo ya nchi kupitia mchango wa maafisa maendeleo ya jamii ambao
husimamia shughuli za maendeleo ya wananchi kuanzia ngazi ya kijiji,
kata hadi Taifa pia usimamizi na utoaji wa elimu kuhusu Haki za makundi
mbalimbali katika jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Maendeleo ya Jamii
vilivyo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na
Watoto Bw. Paschal Joseph Mahinyila amesema kuwa vyuo vya Maendeleo ya
Jamii vinaendelea kufanya kazi nzuri ya kuzalisha wataalam wa masuala ya
maendeleo ambao wamekua msaada kwa wananchi.
Amesema kuwa Serikali inaendelea kuifanyia kazi changamoto ya
uhaba na uchakavu wa majengo inayovikabili baadhi ya vyuo vya maendeleo
ya Jamii ili viweze kudahili wanafunzi wengi zaidi na kuendelea kutoa
elimu katika mazingira bora.
Aidha, amesema kuwa kupitia kikao kazi hicho changamoto ya
Miongozo ya uendeshaji itaweza kufanyiwa kazi ili vyuo vyote viweze
kuzungumza lugha moja na kutekeleza matakwa ya Baraza la Taifa la Elimu
ya Ufundi (NACTE) pamoja na kuviwezesha vyuo vya maendeleo ya jamii
vilivyo chini ya wizara hiyo kuanza kutoa wahitimu wa shahada ya kwanza
kwa kujiunga na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Arusha.
Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Rugemba, Mafinga mkoani
Iringa Bi. Santina Mbata akizungumzia mara baada ya ufunguzi wa kikao
kazi hicho amesema kuwa kukutana kwa wakuu hao wa vyuo vya Maendeleo ya
Jamii ni fursa pekee inayowapa fursa ya kujadili masuala mbalimbali ya
kisera, kisheria, taratibu na miongozo mbalimbali inayosimamia vyuo
hivyo.
Bi.Santina ameeleza kuwa licha ya chuo anachokiongoza kukabiliwa
na changamoto mbalimbali Serikali inaendelea kukijengea uwezo ili
kuhakikisha kuwa kinaendelea kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake kwa
kuendelea kuwajengea uwezo wananchi wanaopata mafunzo kukabilina na
changamoto mbalimbali za maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment