Afya :Siku ya Idadi ya Watu Duniani yaadhimishwa kwa Kulaani Ndoa za Utotoni - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Tuesday, 12 July 2016

Afya :Siku ya Idadi ya Watu Duniani yaadhimishwa kwa Kulaani Ndoa za Utotoni


Na Adili Mhina

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalim amesema kuwa serikali iko mbioni kupeleka bungeni muswada wa marekebisho ya sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ili kutotoa mwanya kwa watoto wa kike kuolewa katika umri wa chini ya miaka 18.

Mhe. Ummy ameyasema hayo katika sherehe za kuadhimisha siku ya idadi ya watu duniani ambaazo huadhimishwa tarehe 11 Julai kila mwaka.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalim (Mb) akitoa hotuba yake katika sherehe za kuadhimisha siku ya idadi ya watu zilizofanyika Julai 11 katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Kwa hapa nchini, sherehe hizo zimefanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na kuhudhuriwa na wawakilishi mbalimbali kutoka serikalini, mashirika ya umoja wa mataifa pamoja na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.

Katika hotuba yake kwenye sherehe hizo zilizotawaliwa na kauli mbiu ‘wezesha msichana afikie ndoto zake’, Waziri Mwalim alisema serikali imejipanga vizuri kuhakikisha haki za watoto wa kike zinalindwa hivyo ni lazima kila mwanachi aelewe umuhimu wa kumlinda mtoto wa kike na kuachana na mila potofu.
Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani.

“Hata hivyo pamoja na sheria hizi nzuri tatizo la mimba za utotoni halitokwisha kama jamii haitabadilika kuhusu mtizamo hasi walio nao baadhi ya watu kuhusu wasichana. Watoto wakike wanatakiwa kuwa shuleni na kupata taarifa sahihi za msingi kuhusu afya zao na kuondoa unyanyapaa, “ alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy alieleza kuwa kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, Tanzania inakadiriwa kuwa na wasichana wadogo milioni 3.4 (wenye umri kati ya miaka 13 hadi 19) sawa na asilimia 7.6 ya watanzania wote na hivyo idadi hii haiwezi kupuuzwa katika mipango mbalimbali ya Taifa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto mhe. Ummy Mwalim akipata maelezo kutoka kwa moja ya washiriki wa maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani.

Waziri Ummy pia alitoa pongezi kwa Tume ya Mipango hususani kwa Kaim katibu Mtendaji Bibi Florence Mwanri kwa jitihada zake za kuhakikisha masuala ya watoto yanaendelea kutambuliwa zaidi na yanafungamanishwa na maendeleo ya uchumi wa nchi.

“Katika kipindi cha miaka sita niliyokaa bungeni nilikuwa sijawahi kuona waziri wa Fedha anawekea msisitizo masuala ya kukabiliana na ndoa za utotoni na kuyafungamanisha na maendeleo ya uchumi. Naamini hizi ni jitihada ulizofanya kuhakikisha masuala haya yanatambulika kwa upana zaidi, hongera sana Kaim Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango kwa kazi yako nzuri”,. Alisema Waziri Ummy.

Kaim Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri amesema kuwa katika kutekeleza mpango wa maendeleo wa miaka mitano wa sasa (2016/17-2020/21) unaohimiza uchumi wa viwanda ni lazima kuwekeza vizuri kwa watoto wa kike kwa kuwa ndio nguvu kazi ya kesho inayotarajiwa kuendesha uchumi wa viwanda.

Bibi Mwanri alisisitiza kuwa watoto wa kike wakilindwa na kupatiwa elim bora, taifa litakuwa na faida kubwa kwani hapo baadae wataweza kujitegemea na kuendesha maisha yao wenyewe, vile vile wataweza kusaidia jamaa na familia zao na pia watakuwa na mchango mkubwa katika pato la taifa.

Kwa sasa wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Tume ya Mipango pamoja na Ofisi ya Taifa ya Takwimu wanaandaa utaratibu wa kutoa elim nchi nzima juu ya masuala ya watoto wa kike hususan mimba za utotoni ili kuondokana na tatizo hilo.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalim (Mb) akisaini daftari la wageni katika banda la Ofisi ya Taifa ya Takwimu wakati wa sherehe za maadhimisho ya siku ya Idadi ya Watu Duniani ambapo , sherehe hizo zilifanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Waziri Ummy Mwalim akiangalia picha na maelezo mbalimbali katika banda la Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA).
Mhe. Ummy Mwalim akisoma jarida katika moja ya mabanda ya wadau waliohudhuria sherehe za siku ya idadi ya watu duniani katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar e s Salaam.
Kaimu Katibu Mtendaji Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri akimwonesha jambo Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar bw. Juma Reli wakati wa sherehe zakuadhimisha siku ya idadi ya watu duniani.



Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Ummy Mwalim (watatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa serikali, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa pamoja wawakilishi wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wakati wa maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani.
Waziri Ummy Mwalim (wa tatu kutoka kushoto kwa waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi waliohudhuri maadhimisho ya siku ya idadi ya watu duniani. Wa kwaza kutoka kusho ni Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa, wa pili (kutoka kushoto) ni Kaim Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Bibi Florence Mwanri, wa kwanza (kutoka kulia) ni Katibu Mtendaji Tume ya Mipango Zanzibar bw. Juma Reli na wapili kutoka kulia ni Mwakilishi mkazi wa UNFPA Tanzania Dkt. Natalia Kanem.

No comments:

Post a Comment