Maafisa
wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
wakifuatilia maadhimisho kulia ni Bi. Mindi Kasiga na Bw. Arnold
Mchemwa.
==================================================
WAZIRI WA MAMBO YA NJE ASHIRIKI KUMBUKUMBU YA MAUAJI YA KIMBARI DHIDI YA WATUTSI
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Augustine Mahiga (Mb) ameshiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya mauaji ya
kimbari nchini Rwanda dhidi ya Watutsi, yaliyoandaliwa na kuratibiwa na
Ubalozi wa Rwanda nchini chini ya Mhe. Balozi Eugene Kayihura
yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City Jijini Dar es
Salaam.
Mhe.
Waziri akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya kumbukumbu hiyo
alieleza namna mauaji hayo ya Kimbari yaliyotokea mwaka 1994 yalivyoleta
simanzi na majonzi kwa wananchi wa Rwanda, nchi majirani wa Rwanda
ambao sehemu yao ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Afrika
nzima na Duniani kwa ujumla kwakuwa mauaji hayo yalipoteza maisha ya
Wanyarwanda wasio na hatia zaidi ya laki nane (800,000) ndani ya siku
mia moja (100).
"Nilishuhudia
madhara ya mauaji hayo mwezi Agosti 1994, wakati huo nikiwa Mwakilishi
wa Umoja wa Mataifa nikisimamia masuala ya Wakimbizi nchini Rwanda, hali
niliyoikuta siku chache baada ya mauaji hayo ilikuwa ya kusikitisha na
inayotisha kwakua ardhi ilikuwa imejaa miili ya watu waliouawa wa rika
zote sambamba na mito iliyokuwa imefurika miili hiyo" alisema Waziri
Mahiga.
Pia
alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa ni wakati sasa mataifa ya Afrika
yakaangalia namna ya kuendesha masuala ya kisiasa na ulinzi katika hali
ya amani pasipo kuharibu utulivu wa Taifa husika ili kuepuka kuharibu
maisha ya watu wasio na hatia pamoja na nguvu kazi kubwa ambayo ndio
tegemeo la kuleta maendeleo sambamba na kukuza uchumi.
Aidha
Mhe. Mahiga alieleza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi
wa Rais wa awamu ya tano Mhe. John Pombe Magufuli itaendelea
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Rwanda katika jitihada za
kupigania na kukemea mauaji kama hayo na kuhakikisha hayajirudii tena
nchini Rwanda wala kutokea tena katika Taifa lolote barani Afrika na
Duniani kwa ujumla. Alisema katika mahusiano ya kidiplomasia,
yanapotokea machafuko yanayo hatarisha amani yanaharibu shughuli za
kidiplomasia zinazoendelea baina ya mataifa husika.
Balozi
wa Rwanda nchini Tanzania Mhe. Eugene Kayihura naye alitoa pole kwa
wahanga wote walionusurika na mauaji hayo na pia akatoa wito kwa
Wanyarwanda wote popote walipo kuzidi kuwafariji na kuwa karibu na
wahanga hao ili waweze kujisikia wapo na ndugu zao na kuwa na matumaini
na maisha ya sasa na ya baadae ili waweze kuendelea kushiriki katika
shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa Rwanda.
"Jumuiya
zote za Kinyarwanda popote zilipo zihakikishe zinakuwa ndugu kwa
wahanga walionusurika na mauaji hayo na kuzidi kuwapa matumaini ya
maisha ya baadae ili kuondoa kisasi dhidi ya jamii iliyosababisha mauaji
ya ndugu zao" Balozi Kayihura alisema.
Vilevile
Mhe. Kayihura alitumia fursa hiyo kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kwa kufanya ziara nchini
Rwanda na kushiriki maadhimisho ya kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari
pamoja na kutembelea maeneo ya kihistoria ya mauaji hayo akiwa na
mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Paul Kagame mapema mwezi
April mwaka huu.
Maadhimisho
ya kumbukumbu hiyo hapa nchini yalihudhuriwa na mabalozi wanaowakilisha
nchi zao hapa Tanzania, Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, Jumuiya ya
Kinyarwanda iliyopo nchini na Watanzania wengine walioalikwa kushiriki
maadhimisho hayo wakiwemo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
wa Sekondari ya Wasichana ya Jangwani.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 10 Juni 2016.
|
No comments:
Post a Comment