Na. Mwandishi Maalum
Wananchi
wa Wilayani Same katika kata ya Hedaru, Makanya na Vunta wameishukuru
serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya uratibu maafa, kwa
kuwajengea uwezo wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana na maafa
yanayotokana na ukame ambao umekuwa ukizisumbua kata hizo Kutokana na
mabadiliko ya Tabia Nchi.
Idara
ya uratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Mradi wa kujengea jamii
uwezo wa kukabili maafa ya ukame imefanikiwa kujenga uwezo huo kupitia
vikundi vya maendeleo vya wilayani humo, ikiwa vikundi kumi (10) kutoka
kata tatu za wilaya hiyo vimepatiwa Mbuzi 40, kuku 50, mbegu za mihogo,
viazi, mtama, mboga mboga pamoja na kutoa miche ya miti kwa shule moja
kila kata na vifaa vya kutunza bustani.
Akiongea
wakati Idara hiyo ilipokuwa ikifuatilia utekelezaji wa mradi huo hivi
karibuni, wilayani humo katika kata ya Makanya, kijijini Mgwasi,
Mwenyekiti wa kikundi cha Kavangere, Stephano Hamisi, alieleza kuwa
wananchi wa kata hiyo kupitia ufadhili wa mradi huo wameweza kulima na
kufuga hali inayowajengea uwezo wa kupunguza na kukabiliana na maafa
yanayotokana na ukame.
“Tunaishukuru
serikali kwa mradi huu, kwani tunao uwezo wa kuzuia, kupunguza na
kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame kwa kuwa tulipewa mbegu za
mazao yanayo himili ukame na yanayo stawi haraka kwa kipindi kifupi cha
mvua, kwa mantiki hiyo tunao uhakika wa chakula lakini pia uhakika wa
kipato kwa kilimo cha bustani, ufugaji wa mbuzi na kuku ambazo
tumewezeshwa na mradi huu ” alisema Hamisi.
Aliongeza
kuwa katika vikundi ambavyo vimewezeshwa na mradi huo wanao utaratibu
wa kila mwana kikundi kupata mbuzi (5) na wengine ambao hawapati mbuzi
hupewa kuku (5) ambapo wanakikundi hubadilishana mifugo hiyo kwa kadri
wanavyo endelea kuzaliana lengo likiwa ni kila mwanakikundi kufuga mbuzi
pamoja na kuku.
Mratibu
maafa wilayani Same, Ally mngwaya anaeleza kuwa mradi huo umeweza pia
kuzijengea jamii uwezo wa kuzuia maafa ya ukame kwa kuhamasisha upandaji
miti, ambapo shule za wilayani humo zimeshirikishwa ili kujenga kizazi
chenye uwezo wa kukabiliana na kupunguza vihatarishi vinavyoweza
kusababisha maafa ya ukame katika kata zao.
“ Kwa
kata tatu zinazofadhiliwa na mradi huu tumechagua shule moja kila kata
na tayari viriba vya miche 2500 vimegawiwa katika shule za wilaya hii
ikiwa lengo ni kufikia miche 5000. Tukipanda miti ya kutosha katika kata
hizi na tukaachana na shughuli za kibinadamu zinazochangia sana
kutokea kwa ukame kama ukataji na uchomaji wa miti ovyo na uharibifu wa
vyanzo vya maji, ninaamini tutakuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia, kukabili
na kupunguza athari zitokanazo na ukame” alisisitiza Mngwaya.
Awali
akiongea katika kata hizo, Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Mradi
huo, Harrison Chinyuka alifafanua kuwa mradi huo umefanikiwa kuwajengea
uwezo wananchi wilayani Same kwa kuwa umewatumia wataalam waliopo
katika ngazi ya Kata za wilaya hiyo katika kuijengea uwezo jamii hiyo
wa kuzuia, kupunguza na kukabiliana na maafa yanayotokana na ukame.
“katika
kutekeleza mradi huu tumewatumia wataalam wa Sekta ya Kilimo, Mifugo,
Afya, Elimu na Utawala wa kata za wilaya hii kwani wataalamu hawa wapo
karibu na jamii inayopata athari za ukame, kupitia wataalamu hawa jamii
hii imeweza kuelewa vihatarishi vinavyoweza kusababisha maafa ya ukame
na matumizi ya mbegu na pembejeo za kilimo, mifugo na misitu pamoja na
upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu na mifugo”
alisema Chinyuka.
Mradi
Wa Kuijengea Jamii Uwezo Wa Kupunguza Athari Za Maafa Kwa Mikoa
Iliyoathirika Zaidi Na Ukame umefadhiliwa na Benki ya Dunia na
kusimamiwa na UNICEF chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya
Uratibu Maafa, na Halmashauri husika wakiwa Watendaji Wakuu wa Mradi
huo. Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 uliozinduliwa
Wilayani Same, mkoani Kilimanjaro tarehe 11 Desemba 2013.
No comments:
Post a Comment