Matukio : Waziri Mkuu Amwakilisha Rais Dkt. Samia Kuaga Mwili wa Marehemu Tendwa - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Friday, 20 December 2024

Matukio : Waziri Mkuu Amwakilisha Rais Dkt. Samia Kuaga Mwili wa Marehemu Tendwa






WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa leo Desemba 19, 2024 amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kuaga mwili wa marehemu John Billy Tendwa ambaye aliwahi kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Akitoa Salama pole kwa waombolezaji wakati wa tukio la kuaga lililofanyika katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa wanafamilia, ndugu na waombolezaji kuyaenzi mema yote aliyoyafanya marehemu Tendwa katika kipindi cha uhai wake.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Marehemu Tendwa alikuwa mtumishi wa umma ambaye mara zote alitekeleza majukumu yake kwa weledi, ujasiri na uadilifu mkubwa katika kipindi ambacho vyama vya siasa vilikuwa vinajijenga. “Tunaungana na wanafamilia katika kuomboleza msiba huu, sote tuna jukumu la kuombea na kuenzi kwa kuyaendeleza mazuri yote aliyoyafanya katika nchi hii”

Naye, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Marehemu Tendwa alikuwa na sifa ya ukweli kwa vyama vyote vya siasa, ujasiri na kutokuwa na upendeleo. “Kwa Kiasi kikubwa amesaidia kujenga demokrasia ya vyama vingi nchini na huwezi kuzungumza kuhusu ustawi wa vyama vya siasa nchini bila kumtaja Marehemu Tendwa”

Kwa Upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi amesema kuwa kifo cha Marehemu Tendwa si pigo kwa familia tu bali kwa wale wote wanaotambua thamani ya mchango wake katika siasa ya demokrasia ya vyama vingi nchini.

Amesema kuwa Marehemu Tendwa alikuwa ni kiongozi mwenye maono na uadilifu wa hali ya juu, aliyediriki kujitolea kwa dhati kuhakikisha misingi ya demokrasia ya vyama vingi inajengwa kwa haki na uwazi “Uongozi wake uliweka alama kubwa katika historia ya demokrasia ya siasa ya vyama vingi hapa nchini”

Kadhalika, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Mheshimiwa Juma Ally Khatibu amesema kuwa marehemu John Billy Tendwa alikuwa nguzo ya mazungumzo ya kitaifa na mshikamano wa kisiasa kwani aliongoza kwa hekima na kujenga mazingira ya siasa yenye heshima, usawa, na mshikamano baina ya vyama vya siasa.

“Katika nafasi yake kama Msajili wa Vyama vya Siasa, marehemu alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha misingi ya demokrasia ya vyama vingi. Alisimamia taratibu za vyama kwa haki na bila upendeleo, akijenga imani kati ya wadau wa siasa na wananchi”

Marehemu Mzee Tendwa alihudumu katika nafasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kipindi cha miaka 12 kutoka Mwezi Mei 2001 hadi Agosti 2013. Marehemu Mzee Tendwa alifariki Desemba 17, 2024 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.

Baadhi ya viongozi walioshiki kuaga mwili wa Marehemu Mzee Tendwa ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderianaga, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonaz.




No comments:

Post a Comment