Lugha Yetu :Nchi 19 zashiriki Tamasha la Kimataifa la Lugha na Utamaduni nchini - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


24 Mar 2015

Lugha Yetu :Nchi 19 zashiriki Tamasha la Kimataifa la Lugha na Utamaduni nchini


Rais wa Kilimanjaro Dialogue Institute Bw. Ali Akkiz akizungumza na washiriki wa Tamasha la Kimataifa la Lugha na Utamaduni jana katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara akipokea zawadi kutoka kwa Rais wa Kilimanjaro Dialogue Institute Bw. Ali Akkiz wakati wa Tamasha la Kimataifa la Lugha na Utamaduni jana katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel kushoto akifurahia maonyesho mbalimbali yaliyokua yakionyeshwa na vijana wakati wa Tamasha la Kimatafa la Lugha na Utamaduni jana jijini Dar es Salaam. Kulia ni Rais wa Kilimanjaro Dialogue Institute Bw. Ali Akkiz na wapili kulia ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara.
Washiriki kutoka nchi 19 wakifuatilia kwa makini matukio yaliyokua yakiendelea katika Tamasha la Kimatafa la Lugha na Utamaduni lililoandaliwa na Kilimanjaro Dialogue Institute na kufanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jana jijini Dar es Salaam.
Wanafunzi kutoka shule za Feza wakiburudisha wakati wa Tamasha la Kimatafa la Lugha na Utamaduni lililoandaliwa na Kilimanjaro Dialogue Institute na kufanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Nyerere jana jijini Dar es Salaam na kuhusisha washiriki kutoka nchi 19 wakiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya lugha ya kiswahili.Picha na: Genofeva Matemu - Maelezo

Na Lorietha Laurence na May-Zuhura Simba -Maelezo

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mhe. Dkt. Fenella Mukangara ameeleza kuwa lugha ina mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii ikiwa itakuzwa sambamba na maendelao ya teknolojia.

Kauli hiyo ameitoa jana jijini Dar es Salaam wakati wa Tamasha la Kimataifa la Lugha na Utamaduni na kufafanua kuwa tamasha hilo limeonyesha kukua kwa lugha ya Kiswahili ambao ni utambulisho wa nchi yetu tangu kupatikana kwa uhuru.

“Mkusanyiko wa leo umeanzisha safari ndefu ya kukuza lugha yetu ya Taifa toka ngazi za chini hadi za kimataifa, hivyo Tanzania imefarijika kuwa mwenyeji wa shughuli hii muhimu “alisema Mhe. Dkt. Mukangara.

Aliongeza kuwa kwa upande wa serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali ya kukiendeleza Kiswahili kwa kukifanya kuwa lugha ya kufundishia kuanzi shule ya Msingi hadi Elimu ya Juu.

Dkt. Mukangara ametoa wito kwa vijana kujifunza Kiswahili na kuitumia lugha hiyo kuweza kujipatia ajira kwa kutangaza utumiaji wa bidhaa za lugha na utamaduni ambazo zina thamani kubwa kiuchumi.

“Lugha ni sawa na kiwanda ikitumiwa vizuri italeta ajira kwa jamii husika na kutumika kama lugha ya kufundisha wageni mbalimbali wanaokuja nchini na hata nchi za nje kwa kuipa hadhi ya kuzungumzwa sehemu mbalimbali” alisema Mhe. Dkt. Mukangara

Kwa Upande wa muandaaji wa tamasha hilo ambaye ni Rais wa Asasi za Kilimanjaro Dialogue Institute, Bw. Ali Akkiz amesema kuwa kupitia tamasha hilo wameweza kutangaza vivutio mbalimbali vya kiutamaduni vya jijini Dar es salaam na Zanzibar.
“Kwa kweli watoto wamefurahi kushiriki katika tamasha hili kwa kuweza kutembelea sehemu zenye vivutio vya utamaduni pamoja na historia najua wataondoka na taswira nzuri ya kutokuisahau nchi ya Tanzania” alisema Bw. Akkiz

Tamasha la Kimataifa la Lugha na Utamaduni ni la kumi 13 kufanyika ambalo limeshirikisha vijana wenye umri kati ya miaka 12 hadi 18 kutoka katika nchi 19 na nchi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa tukio hili kwa mara ya kwanza.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad