WAANDISHI wa habari sita wamenusurika kufa baada ya
gari walilikuwa wakilitumia kwenye msafara wa wabunge wa Umoja wa Kamati za
Mabunge za Hesabu za Serikali kutoka nchi Wanachama wa SADC (SADCOPAC),
kuanguka wakiwa njiani kuelekea Hifadhi ya Ngorongoro.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 3:30 asubuhi nje
kidogo ya mji wa Karatu ambapo waandishi waliokuwemo na vyombo vyao kwenye
mabano ni Veronica Mheta (Habari Leo), Asraji Mvungi (ITV), Edwin Mjwahuzi
(Mwanachi), Peter Nyanje (Citizen), Deogratius Kasamia (Cluods Tv) na Afisa
Habari wa Bunge, Owen Mwandumbya.
Gari hilo lenye namba za usajili T731 ARL lilikuwa
likiendeshwa na dereva wa kampuni ya uwakala wa utalii Shidolya Tours &
safari aliyejulikana kwa jina moja la Riziki ambaye alipoteza fahamu.
Kwa mujibu wa waandishi hao, mara baada ya tukio
hilo walipatiwa usafiri wa kuwapeleka mpaka Hospitali ya Wilaya ya Karatu kwa
matibabu ambapo baada ya uchunguzi wengine walionekana wako sawa, hivyo
kuendelea na safari Majeruhi wengine, Kasamia, Oweni, dereva, Riziki na ofisa
usalama ambaye jina lake halikupatikana walipelekwa jijini Arusha kwa matibabu
zaidi baada ya kuonekana wana majeraha.
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas,
alisema kuwa alisikia tukio hilo ingawa bado anasubiri taarifa kamili toka kwa
mkuu wa polisi wa wilaya hiyo ili aweze kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Wakielezea tukio hilo, waandishi hao walisema kuwa
gari lao likiwa katika msafara wa magari zaidi ya 50 yaliyobeba wabunge, askari
na wanausalama lilijaribu kulipita gari lililokuwa mbele ndipo ghafla gari
jingine lililokuwa kwenye msafara nalo lilitoka kwa mwendo kasi likiyapita
magari mengine.
Mheta alisema kuwa hali hiyo ilimfanya dereva wa
gari lao kupoteza muelekeo ambapo alijaribu kuwakwepa waenda kwa miguu
waliokuwa pembeni ya barabara lakini alishindwa kulimudu na hivyo likapinduka.
Chanzo: Tanzania Daima
Picha zote na Owen David
No comments:
Post a Comment