Jeshi : Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Awaaga Rasmi Watumishi wa Wizara - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


30 Jun 2022

Jeshi : Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini Awaaga Rasmi Watumishi wa Wizara

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amewasili Wizara ya Ulinzi na JKT makao Makuu Mtumba, kwa lengo la kuaga rasmi kabla ya kustaafu kwa Umri wa Utumishi Jeshini. Ziara hiyo ni mwendelezo wa utaratibu wa kupita maeneo mbalimbali kuaga.

Akizungumza wakati wa kikao cha Mheshimiwa Waziri na Menejimenti ya Wizara amesema kuwa mara hii amekuja hapa Wizarani kivingine, maana amekuja kuaga baada ya kulitumikia Jeshi kwa muda mrefu katika nafasi na sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa mafanikio makubwa.

“Leo nimekuja hapa Wizarani kivingine kuja kuaga baada ya kulitumikia Jeshi kwa muda mrefu. Utumishi wa zaidi ya miaka 40 kuanzia mwaka 1979, ni umri wa mtu mzima anayekaribia kustaafu”, alisema

Amemshukuru Mheshimiwa Waziri, Menejimenti pamoja na watumishi wote wa Wizara kwa ushirikiano waliompatia wakati analitumikia Jeshi kwa nafasi ya Mkuu wa Majeshi baada ya kuteuliwa na Rais na Amiri Jeshi Mkuu mwaka 2016.

Jenerali Mabeyo amemwomba Mheshimiwa Waziri, Menejimenti na watumishi wote kumpa kila aina ya ushirikiano anaostahili atakayeteuliwa kuchukua nafasi yake ya Mkuu wa Majeshi.

Kwa upande wake, Mheshimiwa Waziri akiongea Machache kuhusu Jenerali Mabeyo, Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) amesema kuwa kuagana si jambo jema sana, lakini inapendeza zaidi pale unapostaafu kwa heshima, kama anavyostaafu Jenerali Mabeyo.

Aidha, Mheshimiwa Waziri amesema “nakushukuru kwa mchango wako uliotukuka kwa Taifa na kwa Jeshi. Mbali na kulifundisha Jeshi, Jenerali Mabeyo pia, umeliimarisha na kuliheshimisha Jeshi na pia, ulituwakilisha vyema nje ya nchi”, alisema.

“Yapo mambo mengi umeyafanya amabyo yataendelea kubaki. Maana Bila Jeshi Wizara haipo. Na bila Jeshi hatuwezi kufanya chochote”, aliongeza.

Mheshimiwa Dkt. Stergomena alimkabidhi Barua ya Shukrani kwa kutambua mchango wake kwa Wizara na Taifa, pamoja na ushirikiano aliompa kwa kipindi chote alipokuwa Katibu Mtendaji wa SADC na hata alipoteuliwa kuiongoza Wizara hii mwezi Septemba, 2021. Kwa maana hiyo, akamhakikishaia kuwa aondoke akiwa kifua mbele huku akiamini kuwa umeliheshisha Jeshi kwa kufanya mambo mengi mazuri yaliyosaidia kulijenga msingi mzuri Jeshi letu.

Jenerali Mabeyo anastaafu rasmi utumishi wake Jeshini ifikapo tarehe 30 Juni, 2022 baada ya kulitumikia Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa miaka 43. Huku nafasi ya Ukuu wa Majeshi atakuwa ameitumikia kwa kipindi cha miaka sita, miezi mine, na siku 28.

Wakuu wa Majeshi waliomtangulia ni pamoja na Jenerali Mirisho Sam Hagai Sarakikya (1964 - 1974), Jenerali Abdallah Twalipo (1974 -1980), Jenerali David BUgozi Musuguri (1980 -1988), Jenerali Ernest Mwita Kyaro (1988 - 1991), Jenerali Philemon Robert Mboma (1991 - 2001), Jenerali George Mwita Waitara (2001 - 2007) na Jenerali Davis Adolf Mwamunyange (2007 - 2016).

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Ulinzi leo jijini Dodoma.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo akizungumza wakati wa kikao cha Mheshimiwa Waziri na Menejimenti ya Wizara ya Ulinzi na JKT leo jijini Dodoma.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo akikabidhiana baadhi ya nyaraka za wizara na Waziri wa Ulinzi Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb). jijini Dodoma leo.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Ulinzi Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) na Menejimenti ya Wizara hiyo leo jijini Dodoma.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Venance Salvatory Mabeyo akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Ulinzi Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb).

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad