Msaanii wa Bongo Muvi,Elizabeth Michael maarufu kama Lulu akiwa na wazazi waki wakiteta jambo na Wakili Peter Kibatala kabla ya shahidi amaye ni Daktari wa Hospitali ya Muhimbili kutoa ushahidiwake mbele ya mahakama kuu Kanda ya Dar es Salaam .
Na Karama Kenyunko, Globu ya Jamii.
MSANII maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, ameileza Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam kuwa hakusababisha kifo cha marehemu Kanumba bali yeye ndiye aliyeshambuliwa.
Ameeleza kuwa kama siyo Kanumba kudondoka na panga kumtoka mkononi, basi yeye ndie angekuwa marehemu sasa hivi. Kwani kwa mwili wake mkubwa sikuweza kumfanya kitu chochote.
Lulu amedai hayo mbele ya Jaji Sam Rumanyika wakati akitoa utetezi wake katika kesi inayomkabili ya mauaji ya bila kukisudia dhidi ya msanii mwenzake, Marehemu Steven Kanumba, yanayodaiwa kutokea April 6, mwaka 2012 huko Sinza Vatkan.
Akiongozwa na wakili wa utetezi Peter Kibatala, Lulu amedai, mbali ya kuwa wanafanya kazi pamoja kama wasanii, pia alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Kanumba kwa takribani miezi minne kabla ya tukio kitokea.
Msaanii wa Bongo Muvi,Elizabeth Michael maarufu kama Lulu akipitia maelezo aliyochukuliwa na Polisi kipindi alipokamatwa ambayo aliyatoa kwaajili ya ushahidi kwa kuhusishwa na kifo cha Msanii Mwenzake Steven Kanumba. Maelezo hayo ameyapitia katika mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Dar es Salaam.
Akisimulia jinsi tukio zima lilivyotokea amedai, April 6 2012, saa mbili usiku alienda nyumbani kwa rafiki zake mikocheni, akiwa huko Kanumba alikuwa akimpigia simu mara kwa mara kumuuliza mahali alipo. " sikimwambia nipo mikocheni maana mara nyingi alikuwa hapendi niwe mtu wa kutoka toka hasa kwenda sehemu za starehe bila yeye kiwepo". Amedai lulu.
Amedai baada ya kuona Kanumba anazidi kumpigia simu kumuuliza yuko wapi, aliamua kumwambia kuwa anataka kutoka ndipo akamwambia aende Sinza kumuaga.
Akadai alipita kumuaga na alipokaribia alimpigia simu kumwambia kuwa amekaribia kufika ndipo Kanumba alimwambia kuwa akifika aingie ndani moja kwa moja hadi ndani amemuachia mlango wazi.
"Niliingia ndani, nilimkuta anapaka Mafuta nywele zake akiwa kwenye dressing table na kwa kuwa chumbani hakukuwa na kiti nilipofika nilikaa kitandani tukasalimiana ambapo muda mfupi simu yake ikaita, alipokea na kuongea, " namalizia nakuja", nikajua anaongea na Chazi baba ndipo nami nikamwambia nataka kutoka"amedai lulu.
Ameendelea kudai, alipofika pale aligindua Kanumba ameishakunywa, akaniambia kama anatoka waende wote sehemu moja, akaongeza mara nyingi walipokuwa wakitoka wote sehemu moja kunatokea ugomvi, kwani ilipokuwa mtu akimsalimia akimkumbatia alikuwa akimpiga na pia walikuwa wanakwepa kwenda sehemu pamoja kwa ajili ya kukwepa vyombo vya habari.
Nilimwambia kuwa nataka nitoke na rafiki zangu twende Disco mimi sipendi muziki wa Dansi kwani ni kama wakizee, lakini yeye alikuwa hataki badala yake anataka twende wote kwenye dansi,".
Lulu amedai, wakati akiendelea kuongea na Kanumba, simu yake iliita ambapo aliogopa kupokea mbele ya Kanumba kwa sababu alihisi rafiki zake wanampigia na alishamwambia Kanumba kuwa hatoki tena hivyo endapo wangemuuliza kuhusu suala la kutoka basi Kanumba angesikia.
Akadai kuwa, baada ya kuona hivyo, alimwambia Kanumba kwamba anaenda jikoni kuchukua maji, alipokea ile simu na kuwaambia rafiki zake kuwa naenda baada ya muda mfupi
"Nikiwa naelekea kuchukua Maji nilipokea simu, ambapo nikaanza kuongea na rafiki zangu kwamba wasubiri nitatoka, lakini wakati nakata simu Kanumba alikuwa ananifatilia kwa nyuma na kuanza kuniuliza naongea na nani,
" Nilikuwa naongea na rafiki yangu, akaanza kunifuata taratibu, nikaanza kumtania kwa kumwambia unanifata hadi jikoni kujua naongea na nani,"
Akiendelea na ushahidi wake, Lulu amesema kuwa Kanumba mara nyingi alikuwa akimpiga akiwa amelewa, akimuuliza anaongea na nani huku akimfata, na akiwa katika hali ya kukasirika ambapo yeye akawa anarudi nyuma.
"Wakati wote huo alikuwa katika hali ya kulewa, hivyo wakati ananifata nikahisi anataka kunipiga na mimi nikawa nazidi kurudi nyuma nikafungua mlango na kutoka hadi nje,".
Amedai kuwa aliamua kutoka nje akiamini kwamba Kanumba asingeweza kumfata kwa sababu alivaa taulo na alikuwa kifua wazi, hivyo angeona aibu na angeshindwa kumfata kulingana na umaarufu wake lakini sivyo alivyotarajia, "aliendelea kunifata, ambapo alinikimbiza hadi getini na akatoka hadi nje ya geti akiwa peku peku,".
Lulu ameendelea kudai kuwa baada ya kuona anamfuata, aliamua kukimbia hadi lilipo gofu la baa ya Vatican ambayo ilikuwa haifanyi kazi kwa wakati huo.
" Muda wote huo umeme ulikuwa umekatika, niliingia hadi kwenye ghofu hilo na kujificha, lakini Kanumba alinifata hadi nilipojificha na kuanza kunipiga makofi ya uso,".
Amesema kuwa baada ya kumpiga alimshika mikono na kuanzia kumburuza kutoka nje hadi kumuingiza ndani, ambapo alimuingiza chumbani kwake kisha kufunga mlango na funguo na kumrushia kitandani.
"Baada ya kunitupa kitandani, aliinama chini na kuchukua Panga ambapo akaanza kunipiga nalo kwenye ubapa hasa maeneo ya mapajani na kuniambia leo nakuua nikiogopa sana nikajua atanikata, nilikuwa natapatapa ambapo nilijiziba uso ili asiweze kunikata huku nikipiga kelele za kuomba msaada,
Wakati akinipiga alikuwa akilalamika kwamba kwanini naongea na simu na mwanaume mwingine mbele yake,".
Lulu amebainisha kuwa wakati Kanumba akimpiga alikuwa akipumua kwa kasi sana na baada ya muda kidogo alishangaa panga linatupwa chini na akawa kama mtu anayekabwa.
" Akaanguka, akajigonga kwenye ukuta halafu akarudia tena akawa kama mtu anayetaka kuinuka, akatak kuinuka akajigonga tena kwa mara ya pili, alipokuwa chini alikuwa kama anatapatapa,
Lulu amedai, alijaribu kujiokoa, aliinuka na kukimbilia chooni kwa ajili ya kujificha, huku akiwa anapiga kelele za kuomba msaada lakini hakuna aliyetokea.
"Baadaye nilisikia kishindo cha ama mtu kuanguka au mlango uliobamizwa na kusikia ukimya, sikuwaza kama ameanguka nilihisi hasira zake atakuwa ametoka nje, niilipofungua mlango wa bafuni nilimkuta amelala chini wakati huo kulikuwa na mwanga wa mshumaa kwani umeme ulikatika," alidai.
Lulu alidai kwa akili zake aliwaza kuwa Kanumba amejifanyisha kuzimia ili isiwe tatizo kwake endapo mtu angetokea kutokana na kelele alizokuwa anapiga ambapo alianza kumwambia kuwa hata mtu akija atamwambia kila kitu kilichotokea lakini akawa hajibiwi.
Amedai alichukua maji chooni na kumgusisha machoni kuona kama ataamka na lakini alikuwa kimya, akadai baadaye alifungua mlango na kumuita Seth na kumueleza kuwa Kanumba ameanguka ambaye naye alijaribu kumuacha lakini hakuamka na kumpigia simu daktari wake.
Lulu anasimulia kuwa alimwambia Seth hawezi kubaki nyumbani hapo badala yake akitoa naye atatoka kwani akiamka atamuua hivyo aliondoka na gari hadi Coco beach.
Aliendelea kudai kuwa alimpigia simu daktari wa familia Paplas ambaye alikuwa anajua mahusiano yao na wakati akiumwa alikuwa anamtibu na kwamba alimueleza kuwa rafiki yake amempiga sana na iwe mara ya mwisho kumtafuta kwa sababu alimshikia panga na siku nyingine atamuua.
Alieleza kuwa alikuwa haruhusiwi kutoka nyumbani kwao usiku hivyo alikuwa anabeba nguo za ziada na anaporudi nyumbani asubuhi hudanganya kama alitoka kuosha vyombo wakati anatokea klabu.
Amesema akiwa Cocobeach alianza kupokea sms zikimwambia kuwa Kanumba amekufa na zingine zikimuuliza kama ni kweli, Kanumba amekufa.
"Nilimpigia simu Seth ambapo alikuwa hapokei nilimpigia Dk Paplas (Kidume) akamuuliza kuhusu hali ya Kanumba kwani anaona sms watu wanasema amekufa, akamwambia kuwa hajafa ila wapo hospitali na kukata simu. Baadaye Dk Paplas alinipigia kuniuliza niko wapi tukutane," alidai
"Kwa sababu nilijua Kanumba na huyu daktari ni marafiki, nilijua anamtumia rafiki yake niweze kukutana nae, mara ya kwanza nilimkatalia na nikamuuliza kama amezidiwa yupo hospitali gani niende akasema hajazidiwa anaendela vizuri, Nilitaka anihakikishie alipo na asije na Kanumba na wala hakunambia kama ameshakufa," alieleza Lulu.
Alidai walikutana Bamaga na Dk Paplas na ndipo askari walimkamata bila ya kumwambia sababu na walipofika Kituo cha Polisi, Oysterbay Polisi akakutana na watu wengi ikiwemo msanii Vincent Kigosi 'Ray' na kuhisi kwamba Kanumba amekamatwa.
Alidai alichukuliwa maelezo na kuonesha sehemu alizojeruhiwa kwa kipigo na askari wa kike ndiye aliyethibitisha na kwamba alichukuliwa maelezo mara nne ambapo alipata taarifa za kifo cha Kanumba akiwa selo.
Siku inayofuata, Lulu alidai alimueleza Afande Elnatus kwamba anaumwa hivyo alipelekwa hospitali ya Mwananyamala akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi na kuandikiwa dawa.
"Sijasababisha kifo chake yeye ndiyo alikuwa ananishambulia kwa silaha pengine asingeanguka mimi ndio ningekuwa marehemu kwa sababu sikuwa na njia yoyote ya kujitetea kwa sababu ya umbile langu dogo," alidai Lulu.
Hata hivyo, Jaji Rumanyika alimtaka Lulu kueleza kama wakati huo anaendesha gari alikuwa na leseni ambapo alidai kuwa hakuwa nayo mpaka baada ya matatizo hayo ndio aliomba leseni.
Keshi hiyo imeahirishwa mpaka ,ambapo upande wa utetezi utakuwa na shahidi mmoja Josephine Mushumbus ambaye wanadai kuwa yupo nje ya nchi.
Msaanii wa Bongo Muvi,Elizabeth Michael maarufu kama Lulu akitoka katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam mara baada ya kusikiliza Shahidi aliyeufanyia uchungunguzi Mwili wa Steven Kanumba.
Picha na Avila Kakingo,Globu ya Jamii.
No comments:
Post a Comment