Kilimo Kwanza : Simiyu kufanya Mapinduzi ya Kilimo kupitia Umwagiliaji - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 24 August 2017

Kilimo Kwanza : Simiyu kufanya Mapinduzi ya Kilimo kupitia Umwagiliaji





Na Stella Kalinga, Simiyu.


Mkoa wa Simiyu umejipanga kufanya mapinduzi ya Kilimo kupitia skimu kubwa ya Umwagiliaji inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni, kwa lengo la kuwainua wananchi Kiuchumi na kukabiliana na upungufu wa chakula.


Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa huo, Mhe.Anthony Mtaka katika kikao kilichofanyika kati ya Viongozi na Wataalam ngazi ya Mkoa,Wilaya na wananchi wa vijiji vya Kata ya Mwamanyili Wilayani Busega kujadili juu ya mipango ya utekelezaji wa skimu hiyo.


Amesema katika Skimu hiyo Halmashauri ya Wilaya ya Busega itaingia mkataba na kukopa fedha kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo(TADB) ambayo tayari imekubali kutoa mkopo huo, ili kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya maji kutoka Ziwa Victoria kwenda kwenye mashamba, kuwawezesha wananchi kununua mbegu bora, mbolea, na zana bora za kilimo.


Aidha, ameeleza kuwa wananchi katika skimu hiyo watazalisha mpunga kwa misimu miwili kwa mwaka na kupanda mazao mengine mbadala hususani ya jamii ya mikunde mara baada ya kuvuna mpunga, kwa ajili ya kurutubisha Ardhi.


Mtaka amefafanua kuwa Uongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na wananchi wenye mashamba katika Skimu ya Umwagiliaji ya Mwamanyili watakaa kupanga namna bora ya urejeshaji wa mkopo huo, ambapo amewataka wananchi kuwa waaminifu kutekeleza utaratibu watakaokubaliana.


Ameongeza kuwa kutokana na uwepo wa Maji ya Uhakika ya Ziwa Victoria mkoa umekusudia kufanya mapinduzi katika Sekta ya Kilimo na kujenga jamii ya watu wanaoishi kijasiriamali ili waweze kulima kisasa na kibiashara na kuongeza tija katika uzalishaji.


“Tungehitaji tufanye mapinduzi ya Kilimo ili hata siku Mhe.Rais atakapofanya ziara ya kikazi, anakuja kuliona shamba la ekari 2050 za wale walioitwa maskini; tunataka Wilaya ya Busega iwe ya mfano hapa Tanzania ambayo wananchi wake wanalima bila kutegemea mvua” amesema Mtaka.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Mwamanyili Mhe.Charles Luhenze ametoa wito kwa wananchi wa kata hiyo kuchangamkia fursa hiyo na kuwataka kutoa ushirikiano kwa watalaam wanaoendelea na kazi mbalimbali za kitaalam katika eneo la Skimu hiyo kila watakapohitajika.


Naye Malibe Misalaba Sitta mkazi Kijiji cha Nasa Ginnery kata ya Mwamanyili amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka kwa juhudi alizozionesha katika kuhakikisha wananchi wa wilaya ya Busega wanafanya Kilimo cha Umwagiliaji, hivyo akaomba mipango iliyobaki ikamilike haraka ili Skimu hiyo ianze kutekelezwa mara moja
Paulo Buchenja mkazi wa Kijiji cha Mwanangi kata ya Mwamanyili amesema vijana wengi wamehamasika kulima kilimo cha Umwagiliaji wakiamini kuwa kupitia skimu hiyo watalima kisasa ambapo wataongeza uzalishaji hali itakayopelekea kujikomboa kiuchumi.


Skimu ya Umwagiliaji Mwamanyili Busega itatekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa ekari 2050, wananchi watalima kisasa(kitaalam) na kibiashara ambapo mavuno yanatarajiwa kuanzia magunia 30 hadi 40 kwa ekari.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwamanyili, juu ya Skimu ya Umwagiliaji unaotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika kata hiyo Wilayani Busega.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Mhe.Tano Mwera akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwamanyili, juu ya Skimu ya Umwagiliaji inaotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika kata hiyo Wilayani Busega.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (kulia) na Mkuu wa Wilaya ya Busega Tano Mwera wakifurahia jambo kabla ya kuanza kikao na wananchi wa Kata ya Mwamanyili kujadiliana juu ya Skimu ya Umwagiliaji inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika kata hiyo Wilayani Busega.

Diwani wa Kata ya Mwamanyili Mhe. Charles Luhenze akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwamanyili, juu ya Skimu ya Umwagiliaji inaotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika kata hiyo Wilayani Busega.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwamanyili wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka (hayupo pichani) katika kikao cha kujadiliana juu ya Skimu ya Umwagiliaji inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika kata hiyo Wilayani Busega.

Ndg.Shadrack Yohana Mkazi wa Kijiji cha Nasa Ginnery Kata ya Mwamanyili,akichangia jambo katika kikao cha Viongozi wa Mkoa, Wilaya ya Busega na wananchi kilichofanyika katika Kijiji cha Mwamanyili, kwa lengo la kujadili juu ya Skimu ya Umwagiliaji inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika kata hiyo Wilayani Busega.


Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mwamanyili wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(hayupo pichani) katika kikao cha kujadiliana juu ya Skimu ya Umwagiliaji inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika kata hiyo Wilayani Busega.


Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka akizungumza na wananchi wa Kata ya Mwamanyili, juu ya maandalizi ya Skimu ya Umwagiliaji inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni katika kata hiyo Wilayani Busega.

No comments:

Post a Comment