
Wakulima wadogo nchini Tanzania hivi karibuni wataweza kupata taarifa mbalimbali za kijiditali kuhusu masuala ya pembejeo, ukiwemo ushauri utakaosaidia kutatua matatizo yanayowakabili kama vile upatikanaji wa fedha, pembejeo na mafunzo. Mradi huo umezinduliwa na taasisi tatu za Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA), Positive International Limited (PIL), na Grameen Foundation katika sherehe zilizohudhuriwa na maofisa wa serikali, wawakilishi wa vyama vya wakulima, taasisi za fedha, kampuni za mbegu, wafanyabiashara wa nyenzo za kilimo na wale wanaojishughulisha na biashara za mazao ya sekta ya kilimo. Kifaa hicho cha dijitali kitawawezesha wakulima kulipia mapema pembejeo wanazohitaji kupitia simu za mkononi kwa bei nafuu. Pia kifaa hicho kitawapa wakulima pembejeo kulingana na mazao na malengo yao ya uzalishaji na pia kupata taarifa za ushauri kuhusu matumizi bora ya pembejeo hizo. “Moja ya changamoto kubwa zinazowakabili wakulima ni kwamba hukosa fedha mwanzoni mwa msimu wa upandaji mazao, jambo ambalo huwalazimisha kutafuta fedha hizo kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo na hivyo kuwaongezea mzigo,” alisema Hedwig Siewertsen, kiongozi anayeshughulikia masuala ya fedha wa shirika la Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA). “Kifaa hicho cha dijitali kwa ajili kusaidia upatikanaji pembejeo za kilimo ni ufumbuzi wa kipekee. Kitawaimarisha na kuwasaidia wakulima kutenga fedha kwenye akaunti zao za simu ili waweze kununua pembejeo bora kwa muda muafaka na kwa bei nafuu ya asilimia 30.” Wakulima wadogo nchini Tanzania huzalisha asimia 70 ya chakula ingawa karibu nusu yao hawazalishi chakula cha kutosha kwa ajili ya mauzo. Wanakabiliwa na ukosefu wa teknolojia ya kilimo cha kisasa, hawana uwezo wa kujipatia pembejeo bora na wanakosa huduma za kiufundi za ughani zinazoweza kuwasidia kukuza kilimo pamoja na ukosefu wa mafunzo.
Badala yake wakulima hawa wanategemea zaidi kilimo cha mvua, zana duni za kilimo na mbegu hafifu ambazo ubora wake hupungua kila msimu wa kilimo. Isitoshe, wakulima wanaotaka kuwekeza katika kilimo cha kisasa wanashindwa kupata mikopo kwenye taasisi za fedha kwa vile ni asilimia 6 tu ya mikopo ya benki ndio imetengwa kusaidia sekta ya kilimo. Wakulima wanatumia fedha zao chache kununua pembejeo za kilimo kutoka kwa walanguzi; pembejeo ambazo mara nyingi hazina uthibitisho wa ubora. Wakati huo huo, wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo wa sekta binafsi wamegundua kwamba usambazaji wa huduma bora maeneo ya vijijini una faida ndogo kutokana na gharama kubwa za kufanya biashara hiyo, uwezo mdogo wa kifedha kwa upande wa wakulima na umaskini uliokithiri miongoni mwa wananchi wengi vijijini. Matokeo yake ni kwamba wastani wa uzalishaji wa mazao mengi kwa hekta unakadiriwa kuwa ni tani 1.7 na kwamba mavuno ya mazao muhimu ya chakula kama vile mahindi yamekuwa yakipungua kwa sababu ya uharibifu wa ardhi na hali mbaya ya hewa. Jinsi ya kupeleka kifaa cha dijitali kwa wakulima Kifaa cha dijitali kitakuwa na mpango mahsusi wa mazao utakaowawezesha wakulima kupata pembejeo kwa kuzingatia malengo yao ya uzalishaji. Pia, kupitia simu za mkononi, kitawezesha upatikanaji wa huduma za ughani kwa njia ya ujumbe (SMS) kuwaelimisha wakulima matumizi ya pembejeo. AGRA, shirika linaloongozwa na Waafrika wenye weledi wa kuwasaidia wakulima wadogo barani Afrika, ndilo linalogharimia ukuzaji wa kifaa hicho cha dijitali kupitia ufadhili wa MasterCard Foundation. Taasisi ya Grameen Foundation, ambayo ni taasisi inayojitegemea inayotumia teknolojia ya dijitali kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya umaskini, ndio inasisimia ukuzaji wa chombo hicho cha dijitali. Kifaa hicho pamoja na huduma zake kitatolewa na kampuni ya pembejeo za kilimo ya Positive International Limited, ambayo nembo yake ya kibiashara ya Snow Brand imesaidia sana kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wakulima nchini Tanzania. Mfumo huo wa ununuzi wa pembejeo utazingatia uwepo wa huduma za fedha za simu za mkononi zinazokua kwa kasi nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment