Matukio: Waziri Mkuu, Majaliwa Aagiza Maafisa Wanne Wakamatwe - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Monday, 9 January 2017

Matukio: Waziri Mkuu, Majaliwa Aagiza Maafisa Wanne Wakamatwe





*Ni kwa tuhuma za uzembe na upotevu korosho zaidi ya tani 2,000
* Wapelekwa Masasi chini ya ulinzi wakajibu tuhuma zinazowakabili


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Zuberi Mwombeji awakamate maafisa wanne na kuhakikisha wanapelekwa Masasi chini ya ulinzi ili wajibu tuhuma za upotevu wa tani 2, 138 za korosho.


Maafisa hao ni Kaimu Meneja Mkuu Chama Kikuu cha Ushirika cha Masasi (MAMCU), Bw. Kelvin Rajab na Meneja Tawi wa MAMCU, Bw. Lawrence Njozi. Wengine ni wakurugenzi wa kampuni ya YURAP ya Masasi inayohusika na uhifadhi wa mazao kwenye maghala, Bw. Yusuph Namkukula na Bw. Ramadhani Namakweto.


Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo kwenye kikao alichokiitisha Songea mjini jana jioni (Jumamosi, Januari 7, 2017) baina ya watendaji kutoka Bodi ya Korosho Tanzania, MAMCU, wamiliki wa ghala la BUCO – Masasi na kikundi cha wakulima sita waliowawakilisha wenzao kutoka vyama vya msingi (AMCOS) za wilaya za Mtwara na Masasi.


Katika kikao hicho, Waziri Mkuu alitaka apatiwe maelezo ya kina ni wapi zilipo hizo tani 2,138 za korosho wakati taarifa waliyompatia viongozi hao jana inaonyesha kuwa waliuza korosho zote na hakuna hata kilo moja ambayo haijanunuliwa katika mnada wa tano uliofanyika Novemba 10, mwaka jana.


Kaimu Meneja Mkuu wa MAMCU, Bw. Kelvin Rajab alikiri mbele ya Waziri Mkuu kwamba korosho zote ziliuzwa na zilishalipwa an wanunuzi wa mnda wa tano lakini akadai hakupewa taarifa ya kukosekana kwa kiasi hicho cha korosho. Naye mmiliki wa ghala la BUCO, Bw. Ramadhan Namakweto alikiri kupokelewa kwa korosho hizo ghalani kwake lakini akashindwa kutoa maelezo ni kwa nini hazionekani zilipo.


“Tangu mnada wa tano, mmekwishafanya minada mingine mitano hadi kufikia mnada wa 10. Kama kweli hizo korosho zipo ghalani, ni kwa nini korosho za hawa wakulima hazijatolewa ghalani na kuuzwa katika minada iliyofuata huku taarifa yenu ya fedha kuwa mlishazipokea na kuziuza?” alihoji Waziri Mkuu bila kupata majibu ya kueleweka.


Tuhuma zinazowakabili maafisa hao wanne ni kuwalipa kilo pungufu ya zile zilizowasilishwa ghalani, wakulima wa korosho katika wilaya ya Masasi na kutowapa maelezo yoyote juu ya upungufu huo. Mfano ni kufanya makato ya unyaufu kwa wakulima wa chama cha msingi CHAMALI kinyume na maagizo ya Serikali.


Nyingine ni kutowalipa fedha kwa wakati wakulima waliouza korosho kwenye mnada wa tano wa tarehe 10 Novemba 2016 na kutokutoa maelezo yoyote licha ya kuwa MAMCU ilishauza korosho hizo kwenye minada iliyofuatia na kupokea malipo.Nyingine ni kutopelekwa mnadani kwa makusudi kwa tani 2,138 za korosho zilizokuwa katika maghala ya Mtandi na BUCO tangu Novemba 11, mwka jana; kutokutolewa taarifa ya kuwepo korosho hizo kwa mamlaka husika na kuwasababishia hasara wananchi.


Tuhuma nyingine ni kushindwa kufuatilia malipo ya korosho ya tani 1,156,262 ambazo ziliuzwa kwenye mnada wa 10 uliofanyika Desemba 21, 2016. Korosho hizo zilinunuliwa na Maviga East Africa (tani 503,297); Machinga Transport (tani 104,200); Tastey (319,576) na Saweya Impex (tani (229,189).


Kutokana na mapungufu hayo, Waziri Mkuu aliagiza watu hao wapelekwe Masasi chini ya ulinzi ili uchunguzi ufanyike na pia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa hesabu za MAMCU na kujiridhisha kiasi cha korosho kilichonunuliwa; fedha zilizolipwa na kuingia akaunti za MAMCU; kiasi cha fedha zilizolipwa kwa vyama vya msingi na wananchi kwa ulinganifu na bei ya korosho kwa kila mnada husika.


Mapema, wakisoma risala yao kwa Waziri Mkuu, wakulima hao walisema wana kero nyingi sana kama vile kutolipwa fedha zao kwa wakati; kutoeleweka mahali zilipo korosho ambazo walishaziuza kwa MAMCU, kukatwa makato ya unyaufu ambayo Serikali ilikwishapiga marufuku na kutosikilizwa malalamiko yao na viongozi wa MAMCU pamoja na viongozi wa mkoa na wilaya.


“Makubaliano yalikuwa ni kwamba mkulima atapewa fedha yake siku sita baada ya mnada kufanyika lakini hivi sasa baadhi yetu tumeuza korosho tangu Oktoba, mwaka jana lakini hadi imefika Januari hii bado hatujalipwa. Pia kuna makato yaliyoondolewa kwenye mfumo, kwa mfano unyaufu lakini wao wameyaacha na unapoenda kuuza wanahesabu na kukukata kuwa utalipia gharama za unyaufu,” alisema msoma risala Bw. Sylvester Mtimbe ambaye pia ni mkulima kutoka AMCOS ya Chiungutwa.


Wakulima hao wa korosho kutoka Masasi mkoani Mtwara walikutana Januari 3, 2017 katika kijiji cha Chiungutwa na kuazimia kuwa wangeandamana hadi Dar es Salaam ili wawasilishe kilio chao kwa Waziri Mkuu au kwa Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli.


Kwa kutambua umbali uliopo kutoka Masasi hadi Dar es Salaam na kwamba yeye hakuwepo katika siku waliyopanga kwenda huko, Waziri Mkuu aliamua kuwaita wakulima hao wamfuate Songea ambako alikuwa na ziara ya kikazi ya siku nne.


IMETOLEWA NA
OFISI YA WAZIRI MKUU
JUMAPILI, JANUARI 8, 2017.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimuhoji Kaimu Meneja mkuu wa chama kikuu cha ushirika Masasi Mtwara (MAMCU) Bwana Kelvin Rajabu kuhusiana na upotevu wa koroshozaidi ya tani 2000 Waziri mkuu alifanya kikao na Bodi ya korosho pamoja na baadhi ya wanaushirika Mamcu kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano Ikulu ndogo Mkoani Ruvuma

Kamanda wa polisi mkoani Ruvuma Zuberi Mwombeji akiwatarifu Maofisa wa Mamcu na Yurap wako chini ya ulinzi wa polisi kuhusiana na upotevu wa korosho tani 2000 kulia mwenye kaunda suti Kaimu meneja mamcu Bwana Kelvin Rajabu anayefuatia Mkurugenzi wa YURAP inayojishughulisha nauhifadhi korosho katika Ghala la BUCO Masasi Bwana Yusuf Namkula anayefuatia Mkurugenzi mwenzake Bwana Ramadhan Nama na Meneja tawi la Mamcu Bwana Lawrence Njozi

Watuhumiwa wakipelekwa kupanda gari la polisi kwa ajili yakuwapeleka rumande

Kaimu Meneja wa Mamcu bwana Kelvin Rajabu akipanda gari la polisi tayari kwakwenda rumande.Picha na Chris Mfinanga

No comments:

Post a Comment