Elimu : Shule ya Enyorata yatenga Sh milioni 50 kusaidia watoto wenye mahitaji - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

Friday, 25 September 2026

Elimu : Shule ya Enyorata yatenga Sh milioni 50 kusaidia watoto wenye mahitaji





Na Mwandishi wetu Arusha


Shule ya Awali na Msingi ya Enyorata iliyopo Maji ya Chai, imeeleza kuwa imetenga zaidi ya Sh milioni 50 kwa ajili ya kusaidia watoto wenye mahitaji mbalimbali ya elimu, huku zaidi ya watoto yatima 100 wakinufaika na mpango huo.


Mkurugenzi wa shule hiyo, Bw. Vincent John Kinga, aliyasema hayo wakati akizungumza na wanafunzi, walimu pamoja na walezi katika sherehe za mahafali ya wanafunzi wa Darasa la Saba katika Shule ya Msingi Enyorata.


Kinga alisema shule hiyo yenye zaidi ya wanafunzi 600 imekuwa ikitoa elimu inayokwenda sambamba na malezi, ikiwemo kuwafundisha wanafunzi kuhusu maadili na namna ya kuishi kwa kuzingatia misingi mizuri katika jamii.


Alisema kupitia mpango huo wa kusaidia watoto wenye mahitaji, zaidi ya watoto yatima 100 tayari wameweza kunufaika, hatua ambayo amesema inalenga kuhakikisha watoto hao wanapata fursa ya kupata elimu na malezi bila kujisikia kutengwa.


Akizungumzia mipango ya maendeleo ya shule hiyo, Kinga alisema wana mpango wa kuendelea kuwawezesha watoto katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kuibua na kuendeleza vipaji walivyonavyo.


Alisema suala la vipaji ni muhimu kwa watoto kwa kuwa linaweza kuwasaidia kujenga uwezo wao na kutumia vipaji hivyo katika maisha yao ya baadaye.


Kinga pia aliwataka wazazi na walezi kushirikiana na shule katika kuhakikisha watoto wanalelewa katika misingi mizuri ya maadili, akisisitiza kuwa malezi ya mtoto yanaanzia katika familia.


Alisema wazazi wanapaswa kuwa mfano mzuri kwa watoto wao kwa sababu tabia na mwenendo wa wazazi vinaweza kuwa na mchango mkubwa katika kujenga tabia za watoto.


“Wazazi mnapaswa kuhakikisha mnakuwa na maadili mazuri, kwa sababu watoto wanajifunza mambo mengi kutoka kwa wazazi wao. Kama mzazi ana maadili mabaya, kuna uwezekano mtoto naye akajifunza tabia hizo,” alisema Kinga.


Aidha, aliwataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao kielimu na kitabia, ili kuhakikisha wanakua katika mazingira salama na yenye malezi bora.

No comments:

Post a Comment