Na Mwandishi wetu Arusha
Mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, Dkt Johannes Lukumayi, ameahidi kugharamia mafunzo kwa maafisa usafirishaji wa bodaboda katika Kata ya Nduruma, Wilaya ya Arumeru, kwa lengo la kuwaongezea uelewa wa sheria na usalama barabarani.
Dkt Lukumayi alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nduruma katika moja ya ziara zake za mara kwa mara, ambazo amesema lengo lake ni kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ya jimbo hilo.
Alisema fedha atakazotumia
kugharamia mafunzo hayo ni fedha zake binafsi, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuwapa vijana hao fursa ya kujifunza na kuona fursa mbalimbali za maendeleo kupitia shughuli zao za usafirishaji.
Dkt Lukumayi alisema mafunzo hayo yatawasaidia waendesha bodaboda kufahamu na kuzingatia sheria za usalama barabarani, hivyo kupunguza uwezekano wa kujikuta wakikiuka sheria za usafirishaji.
“Natamani kuona bodaboda wa Kata ya Nduruma wakiwa walinda amani wa nchi yetu,” alisema Dkt Lukumayi, akisisitiza umuhimu wa vijana hao kuwa mfano katika kuzingatia sheria na kudumisha amani katika jamii.
Akizungumzia changamoto zinazowakabili wananchi wa kata hiyo, Dkt Lukumayi alisema suala la upatikanaji wa maji lilikuwa miongoni mwa changamoto kubwa, lakini kwa sasa hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa kukabiliana na tatizo hilo.
Alisema pamoja na hatua zilizochukuliwa, ataendelea kulifikisha suala hilo katika maeneo husika ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa uhakika.
Katika sekta ya afya,
Dkt Lukumayi alisema kuna umuhimu wa kuongeza ufanisi katika huduma zinazotolewa katika Hospitali ya Nduruma ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya kwa wakati.
Alisema pia kituo cha afya Nduruma kinahitaji kuimarishwa zaidi, ikiwemo kuboreshwa kwa huduma na miundombinu, ili kiweze kukidhi mahitaji ya wananchi wanaokitegemea.

No comments:
Post a Comment