Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akikagua moja ya shamba la mahindi lililoharibiwa na tembo katika kijiji cha Kunzugu, wilaya ya Bunda Mkoani Mara jana wakati wa ziara yake ya kuangalia changamoto za uhifadhi mkoani humo. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kunzugu, wilaya ya Bunda, mkoani Mara jana alipotembelea moja ya shamba la mahindi lilioharibiwa na tembo wakati wa ziara yake ya kuangalia changamoto za uhifadhi mkoani humo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili.
NA HAMZA TEMBA - WMU
.......................................................
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema italipa madeni yote ya miaka ya nyuma ya vifuta jasho na vifuta machozi ambayo inadaiwa na wananchi waliokubwa na vitendo vya uharibifu wa wanyamapori nchini kabla ya bunge lijalo la bajeti, madeni hayo ni yale ambayo yameshaifikia wizara hiyo na kuhakikiwa.
Akizungumza jana na uongozi wa wilaya ya Bunda wakati wa kuhitimisha ziara yake ya siku moja ya kufuatilia changamoto za uhifadhi wilayani humo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhandisi Ramo Makani amesema uamuzi huo wa Serikali utaondoa kilio cha muda mrefu cha wananchi ambao wamepata madhara mbalimbali ya wanyamapori ikiwemo vifo, majeruhi, kuliwa mazao na kuharibiwa mashamba yao.
"Serikali ya awamu ya tano imeshakamilisha takwimu za madai, yale yote tunayodaiwa huko nyuma, yaliyoifikia Wizara yakafanyiwa uhakiki na nimesema kwenye uhakiki huo ndani ya kipindi cha miaka kumi, kwa wilaya zaidi kidogo ya 80 ambazo ndizo zina changamoto hizi kwa kiwango kikuu, deni jumla ni shilingi 2,081,532,700 (bil. 2.9)", amesema.
Amesema wilaya ambazo zimeathirika zaidi na vitendo hivyo na ambazo madai yao ni makubwa zaidi ya Wilaya zingine ni Serengeti na Bunda ambazo ziko mkoani Mara na zinapakana na Hifadhi ya taifa ya Serengeti, Ziwa Victoria, Pori la Akiba Grumeti na Ikorongo. "Serengeti ndiyo inayoongooza kwa madai hayo, shilingi milioni 408,547,600 alafu Bunda shilingi milioni 265,969,750",.
Pamoja na Serikali kujiwekea utaratibu huo na wananchi wa kulipa vifuta jasho na vifuta machozi kwa waathirika, amesema ipo haja ya kutafuta njia endelevu ya kukabiliana na changamoto hizo na fedha ambayo ingetumika kulipia fidia hizo ikatumika kuwezesha mpango huo endelevu. Amesema mpango huo utawezekana kwa kuwashirikisha wananchi.
"Mpango endelevu wa kukabiliana na changamoto hiyo ni ule wa ushiriki wa pamoja wa Serikali na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya uharibifu dhidi ya wanyamapori", amesema.
Ili kufanikisha mpango huo ameuagiza uongozi wa wilaya ya Bunda na Serengeti kuratibu ushiriki wa wananchi wao katika zoezi hilo kwa kuunda vikundi shirikishi katika kila kijiji, kubaini mahitaji yake ikiwemo vifaa na kuwasilisha taarifa hiyo wizarani kabla ya tarehe 15 januari mwaka huu, kwa ajili ya hatua zaidi za kufanikisha mpango huo.
Amesema ushirikiano huo pekee hautoshi kukabiliana na changamoto hizo kama wananchi nao hawataipunguzia mzigo serikali wa kupambana na vitendo vyao viovu dhidi ya uhifadhi, ili nguvu hiyo itumike katika kushirikiana nao kwenye ulinzi dhidi ya wanyama waharibifu. "Wananchi waache vitendo viovu dhidi ya uhifadhi, ujangili, kuua wanyamapori",.
Ameeleza kuwa miongoni mwa sababu za kuongezeka kwa changamoto hizo ni matokeo ya tabia za wananchi kusogelea maeneo ya hifadhi kwa ajili ya shughuli za kibinadamu, jambo ambalo lina athari kubwa katika uhifadhi na usalama wa wananchi wenyewe, hivyo ni lazima liepukwe.
"Njia ambayo tembo alikua akipita miaka 20, 30, 40 ndo anapita kila siku, sisi tumeenda kujenga, tumeenda kulima mashamba, sasa tembo wao na wenyewe wana ownership (umiliki), ile njia wao wanaona ni ya kwao tu, kwahiyo akikutana na wewe anafanya hayo anayoyafanya, hata kwenda kukaa kufanya shughuli za kibinaadamu ikiwemo kujenga na kulima jirani kabisa na kwenye mpaka ya hifadhi na yenyewe ni tatizo".
Naibu Waziri Makani amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Mara jana ambapo alitembelea vijiji kadhaa wilayani Bunda na Serengeti na kushudia athari mbalimbali za uharibifu wa wanyamapori pamoja na kupokea malalamiko mbalimbali ya uharibifu huo kutoka kwa wananchi. Alishuhudia mashamba kadhaa ya mahindi yaliyokuwa karibu na maeneo ya hifadhi yakiwa yameharibiwa na tembo.
No comments:
Post a Comment