Matukio : Mfuko wa Mawasiliano Ukamilishe Mawasiliano Vijijini - Prof. Mbarawa - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


18 Jan 2017

Matukio : Mfuko wa Mawasiliano Ukamilishe Mawasiliano Vijijini - Prof. Mbarawa



Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa(Kulia), akitoa maelekezo kwa Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote UCSAF Bw. Godfrey Simbeye, wakati alipokagua shughuli zinazofanywa na mfuko huo jijini Dar es salaam.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa(Kulia), akipata taarifa ya utendaji kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote UCSAF Eng. Peter Ulanga, alipokagua shughuli zinazofanywa na mfuko huo jijini Dar es salaam.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akikagua kumbukumbu za wateja wanaohudumiwa na kampuni ya simu TTCL kanda ya Kaskazini eneo la Kijitonyama jijini Dar es salaam.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (Katikati), akisisitiza jambo kwa maofisa wa kampuni ya Simu TTCL kanda ya Kaskazini alipokagua huduma zinazotolewa na kampuni hiyo.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa mmoja wa ofisa wa kampuni ya Simu TTCL namna ya kufanya kazi kwa ubunifu ili kuongeza wateja katika kampuni hiyo. Picha na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa ameitaka Menejimenti ya Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF), kuhakikisha vijiji vyote nchini ambavyo havijaunganishwa na huduma ya mawasiliano vinaunganishwa kabla ya mwisho wa mwaka huu.


Aidha, Profesa Mbarawa amesisitiza mfuko huo kutoa kipaumbele kwa vijiji vyote vilivyomo sehemu za mipakani ili kuimarisha ulinzi na uharaka wa mawasiliano katika maeneo hayo.


Amewaagiza UCSAF kukutana na mitandao ya simu ili kukamilisha kazi kwa mujibu wa mkataba kwa kata 121 ambazo hazijapata huduma ya mawasiliano hapa nchini.


“Nia ya Serikali ni kuhakikisha vijiji vyote nchini vinapata huduma ya mawasiliano ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba ili kuwezesha mikakati mingine ya kuboresha Mifumo ya Tehama katika shule na Hospitali kuendelea na hivyo kuhuisha huduma za Tehama katika Sekta za afya na elimu”, amesema Profesa Mbarawa.


Profesa Mbarawa ameonya kampuni za simu zitakazoshindwa kupeleka mawasiliano katika maeneo waliyopangiwa kwa wakati zitapokonywa masafa katika maeneo husika ili kuzipa kampuni zilizo tayari.


Naye Mjumbe wa Bodi ya UCSAF Bw. Godfrey Simbeye, amemhakikishia Waziri Mbarawa kuwa Bodi yake imejipanga kuhakikisha inaratibu huduma zote za Tehama zinazotolewa na taasisi mbalimbali nchini ili kuweka uwiano wa huduma hizo nchini kote.


Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa UCSAF Eng Peter Ulanga, amesema kuwa mfuko huo umejipanga kupeleka mawasiliano katika maeneo yasiyo na mvuto kibiashara ili kutoa haki kwa wakazi wa maeneo hayo kunufaika na fursa za mawasiliano na kuchochea maendeleo.


Takribani asilimia 94 ya Wakazi wa Tanzania wanapata huduma ya mawasiliano lengo likiwa ni kufikia asilimia 100 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.



Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad