Na Josephat Lukaza
Mbwa ni mnyama kama wanyama wengine ambao huweza kupata magonjwa mbalimbali ambayo hupelekea kufa au kuwapa vilema vya maisha. Mbwa ni kama binadamu yoyote tu ambaye akishambuliwa na magonjwa basi anaweza kuwa dhaifu na kupelekea kupoteza maisha au kupona lakini pia ni wanyama kama binadamu tu wengine ambao hata wakipatwa na baadhi ya magonjwa basi wanaweza kustahimili na kupona kabisa.
Basi leo tutaangalia baadhi ya magonjwa yanayowapata viumbe hivi vinavyopendwa sana na rafiki mkubwa wa binadamu. Kama ilivyo kwa wanyama wengine na binadamu ugonjwa uanza kuonekana kutokana na dalili flani ambapo ndio zinakupa taarifa za kuhisi kuwa mnyama huyu ni mgonjwa. Lakini kuna baadhi ya magonjwa ukiona dalili zake basi unajua kabisa kuwa ishatafuna sehemu kubwa na kupona ni majaaliwa na hali ipo hivyo hivyo kwa wanyama kama Mbwa.
Tuanze na Huu leo
1:Parvovirus Infection (Kwa kifupi uitwa Parvo)
Ugonjwa huu ni ugonjwa unaosababishwa na Virusi ambapo mara nyingi hushambulia mbwa wadogo wenye umri wa kuanzia wiki sita mpaka miezi sita. Ugonjwa huu ni moja ya ugonjwa mbaya sana kwa mbwa kwasababu unapomuingia tu basi matumaini ya kupona kwa mbwa huyo ni madogo sana kwasababu ni ugonjwa ambao ukimpata mbwa ndani ya masaa 24 unaweza kupelekea kifo kwa mbwa huyo.
Ugonjwa huu husambulia sana mapigo ya moyo na kupelekea mapigo ya moyo ya mbwa huyo kwenda mbio sana, na kumfanya hapoteze hamu ya kula, joto kushuka sana.
Hizi ndio dalili kubwa sana za ugonjwa huu wa Parvo ni Kuharisha damu, Kutapika, kukosa hamu ya kula, kupungua uzito ghafla. Mara umuonapo mbwa wako ana dalili hizi basi unashauriwa kuwasiliana na mtaalamu wako wa wanyama kwaajili ya ushauri na matibabu zaidi ijapokuwa kama mbwa huyo hakuwahi kupatiwa chanjo ya Ugonjwa huo tokea utotoni basi asilimia ya kupona ni ndogo sana kwa maana unapoona dalili za ugonjwa huu basi ni dhahiri unakuwa ushamshambulia sana mbwa huyo.
Nini husababisha ugonjwa huu wa Parvo?
Mara nyingi ugonjwa huu usababishwa na mbwa aliyehathirika moja kwa moja na ugonjwa huu japokuwa kuna sababu nyingine kama endapo mbwa aliyeathirika na ugonjwa huu anapojisaidia haja kubwa na mbwa mwingine akapita kunusa basi mbwa huyo anakuwa anaambukizwa moja kwa moja. Inasemekana virus vya ugonjwa huu vinauwezo wa kuishi kwenye udongo kwa takribani mwaka mmoja na ugonjwa huu unaweza kuambukizwa moja kwa moja kutoka kwa mbwa mmoja kwenda kwa mbwa mwingine.
Vilevile Ugonjwa huu unaweza kuletwa na viatu endapo mtu amekanyanga kinyesi cha mbwa aliyeathirika na ugonjwa huu basi anapoingia nyumbani au kwenye mazingira ya mbwa ni rahisi sana kuacha virusi hivyo na ikumbukwe kuwa virusi hivi huishi kwa takribani mwaka mzima kwenye udongo.
Unapohisi umekanyaga kinyesi au kitu chochote ambacho kinaweza kuwa na virusi vya parvo basi unashauriwa kusafisha eneo hilo kwa kutumia madawa ya kuua virusi kwaajili ya kujirinda na ugonjwa huo hatari.
Vilevile Kutompa chanjo sahihi mbwa wako na kwa wakati kunaweza kupelekea kusababisha mbwa wako kupata ugonjwa huo, Kama unavyofahamu kuwa mbwa wanatabia ya kunusa kila sehemu endapo bahati mbaya kanusa sehemu ambayo tayari kuna virusi vya ugonjwa huo na hana chanjo basi ni rahisi kushambuliwa na virusi hivyo.
Tiba ni Ipi kwa Ugonjwa Huu?
Inavyosemekana mpaka sasa hakuna tiba sahihi ya ugonjwa huu lakini Mbwa anapozaliwa tu na kufikisha muda wa wiki moja hadi mwezi unashauriwa kumpatia chanjo mbalimbali kwaajili ya kumkinga na magonjwa kama haya na chanjo hio sio ya mara moja tu anapochomwa mwanzoni basi unatakiwa kufata ushauri wa mtaalamu wa wanyama kwa ratiba tena ya kurudia kumchoma chanjo katika kipindi kijacho.
Aina hizi za mbwa ndio aina rahisi sana kushambuliwa sana na ugonjwa huu Rottweilers, Doberman Pinschers, Pit Bulls, Labrador Retrievers, German Shepherds.
Tukutane tena siku ijayo.
Je umeipenda makala hii?Basi unaweza kushare na Wenzako
Tu follow instagram kwa jina la @lukazablog @lukazablog @lukazablog