Michezo : Waziri, Nape akagua marekebisho ya Miundombinu iliyoharibiwa Uwanja wa Taifa - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


12 Dec 2016

Michezo : Waziri, Nape akagua marekebisho ya Miundombinu iliyoharibiwa Uwanja wa Taifa





Na Benedict Liwenga-WHUSM.
Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye leo ametembelea Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam ili kukagua shughuli za marekebisho ya miundombinu inayoendelea uwanjani hapo ikiwemo kukagua ufanisi wa Kamera za kufuatilia matukio Uwanjani pamoja na marekebisho ya viti vya kwenye majukwaa.

Katika ziara yake Waziri Nape amekagua namna Kamera za CCTV zinavyokuwa na uwezo wa kubaini matukio mbalimbali yanayoendelea uwanjani ambapo ameridhika na utendaji kazi wa kamera hizo na kusisitiza zitumike ipasavyo ili kuwabaini wahusika wanaoharibu miundombinu ya uwanja.


Amesema kwamba kazi ya kubaini waharibifu wa miundombinu kwa sura katika uwanja huu kwa kutumia hizi kamera yataongeza hali ya usalama kwenye uwanja na pia kusaidia kufuatilia matukio ya kihalifu Uwanjani kama vile kuvunja viti”, alisema Mhe. Nape.


Aidha, amesema kwamba ukarabati wa uwanja unaoendelea sasa pinid utakapokamilika utaufanya uwanja huo kuwa salama zaidi na ndiyo maana kamera nyingi zimeweka ili kuendelea kubaini matukio yanayoendelea ndani na nje ya mipaka ya uwanja ikiwemo milangoni.


“Kwa sasa uwanja wetu utaweza kushughulika na mtu mmoja mmoja anayehujumu miundombinu yetu, kwasababu kamera zetu zina uwezo mkubwa wa kumtambua mtu kwa sura pindi awapo uwanjani kuanzia magetini”,alisema Mhe. Nape.


Ameagiza ukarabati wa miundombinu uendelee ikiwemo mageti na viti uendelee kufanyika kwani yeye anachosubiria ni kukabidhiwa uwanja huo siku ya tarehe 13 Desemba mwaka huu na siku hiyo ndiyo itafahamika thamani ya ukarabati uliofanyika kwa ujumla.


Aidha, amegusia suala la Mkataba ulioingiwa kati ya Serikali na Klabu ya Yanga African ambapo amesema kwamba, Serikali iliingia Mkataba na Klabu ya Yanga African ya kutumia uwanja wake wa Taifa pamoja na uwanja wa Uhuru tarehe 1 Desemba, 2016 kwa muda wa mwaka mmoja yaani mpaka tarehe 30 Novemba,2017.


Amesema kwamba, kutokana masharti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF), vilabu vyote vinavyoshiriki michezo ya Kimataifa vinatakiwa kuonyesha uthibitisho wa umiliki wa uwanja au viwanja vitakavyotumika katika mechi zao au kuonyesha mkataba walioingia ambapo mechi hizo zitachezwa.


“Kwa kuwa klabu ya Yanga haina Uwanja wake, walileta ombi Wizarani, la kuingia Mkataba na Mmiliki wa Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Uhuru yaani Serikali. Serikali iliona ni busara kuingia mkataba na Klabu ya Yanga African ili pale ambapo watahitajika kutaja uwanja watakaotumia waweze kutaja Uwanja wa Uhuru au Uwanja wa Taifa”, alisema Mhe. Nape.


Kwa muktadha huo, Klabu ya Yanga itaendelea kutumia uwanja wa Uhuru ambao haukujumuishwa katika maamuzi ya kufungiwa na hauna tatizo la kukarabatiwa.


Amesisitiza kuwa, Serikali ina nia njema kwa vilabu vyake na wadau wote wa Michezo na Serikali inafanya shughuli zake kwa kuzingatia Sheria, Taratibu na Kanuni, hivyo amevitaka Vilabu vyote viwe na utamaduni wa kufuata sheria, taratibu na Kanuni katika kutekelea majukumu yao.


Kaimu Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw. Julius Mgaya (kushoto) akimuonyesha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye jinsi Kamera za CCTV zinavyoweza kumnasa mtu akifanya jambo lolote baya ndani ya Uwanja wa Taifa wakati alipotembelea kukagua marekebisho ya miundombinu ya uwanja huo leo 11 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye, Kaimu Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw. Julius Mgaya pamoja na Waandishi wa habari wakiangalia hatua iliyofikiwa ya urekebishaji wa viti na miundombinu mingine ya uwanjani hapo wakati alipotembelea kukagua marekebisho ya miundombinu ya uwanja huo leo 11 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye (kulia) akiwa ameongozana na Kaimu Meneja wa Uwanja wa Taifa Bw. Julius Mgaya pamoja na Waandishi wa habari wakielekea kuangalia hatua iliyofikiwa ya urekebishaji wa viti na miundombinu mingine ya uwanjani hapo wakati alipotembelea kukagua marekebisho ya miundombinu ya uwanja huo leo 11 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Moses Nnauye akiangalia namna Kamera za CCTV zinavyofanya kazi ya kubaini matukio yanayoendelea ndani ya Uwanja wa Taifa wakati alipotembelea kukagua marekebisho ya miundombinu ya uwanja huo leo 11 Desemba, 2016 Jijini Dar es Salaam.

Post Top Ad