Serikali
imepata gawio la shilingi Bil. 23 kutoka Kampuni tatu za NMB Bank PLC,
Puma Energy na Tiper (T) ikiwa ni faida iliyotokana na biashara
iliyofanyika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016, ambazo
imewekeza hisa zake kati ya asilimia 31 na 50.
Mfano
wa hundi zenye thamani ya kiasi hicho cha fedha zimekabidhiwa kwa Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, katika Ofisi za Hazina Ndogo
Mjini Dodoma, leo Juni 9, 2016
Kampuni
ya kwanza kukabidhi gawio (dividends) ni Puma Energy, inayojihusisha na
biashara ya kuuza mafuta, ambayo serikali ina hisa zake asilimia 50
iliyokabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya shilingi Bil. 4.5 (Bilioni 4
nukta 5) baada ya kampuni hiyo kupata faida ya shilingi Bil. 9 katika
kipindi kinachoishia Desemba mwaka jana
Kampuni
ya Tiper (T) inayofanya biashara ya uhifadhi wa mafuta (storage),
ambayo serikali ina hisa ya asilimia 50 pia, imekabidhi gawio la
shilingi Bil 2.0 (Bilioni 2 nukta 0) na kufuatiwa na Benki ya NMB PLC,
iliyomkabidhi Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango, hundi kifani yenye
thamani ya shilingi Bilioni 16.5 (Bilioni 16 nukta 5)
Serikali
imepata kiasi hicho cha fedha kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina,
inayosimamia Mashirika, Taasisi za Umma na Kampuni zenye hisa na
serikali.
Akizungumza
baada ya kupokea hundi hizo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip
Mpango, amezishukuru kampuni hizo kwa kuiwezesha serikali kupata kiasi
kikubwa cha fedha zitakazotumika kuwahudumia wananchi.
"leo
ni siku yangu ya furaha sana kwa kupata kiasi kikubwa cha fedha kiasi
hiki ikiwa ni siku moja tu tangu niwasilishe Bajeti Kuu ya Serikali
Bungeni hapa Mjini Dodoma" aliongeza Dkt. Mpango
Amemwagiza
Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru, kuhakikisha kuwa kampuni zote
ambazo serikali ni mbia zianze kulipa gawio kwa serikali na kuacha
visingizio vya kutangaza kupata hasara kila mwaka wakati hawafungi
biashara zao.
"Naomba
vyombo vinavyohusika na ukusanyaji wa mapato ya serikali pamoja na
Msajili wa Hazina kuzifuatilia na kuzikagua kampuni ambazo serikali ina
hisa ili kubaini ukweli ni kwanini hazitoi gawio zikisingizia kupata
hasara kwenye biashara wakati hawafungi biashara hizo" Alisisitiza Dk.
Mpango
Dk.
Mpango pia amevitaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi, ili kubaini
mianya ya upotevu wa mafuta bandarini na kuagiza wale wote walihusika na
upotevu huo wachukuliwe hatua.
"
Haiwezekani wajanja wachache wanafaidika halafu wananchi wanyonge
wanalala chini hospitalini, Nilisema jana na leo narudia yeyote
anayetukwamisha kwenye maendeleo ni msaliti lazima washughulikiwe kwa
mujibu wa sheria bila huruma,” alisema.
Awali
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani, amezipongeza
kampuni hizo kwa kutoa gawio hilo na kumhakikishia Waziri wa Fedha na
Mipango, Dokta Philip Mpango, kuwa gawio litaongezeka kwa kasi kubwa
katika miaka ijayo ili kuiwezesha serikali kuwa na uwezo zaidi wa
kuwahudumia wananchi.
“Mwaka
2014 tulipata gawio la Sh bilioni 3 kutoka Kampuni ya PUMA Energy,
mwaka huu tumepata bilioni 4.5 ni matarajio ya Serikali kwa mwendo huu
mwakani tunaweza kupata bilioni 6" alisema Dkt. Kalemani.
Alitoa
wito pia kwa kampuni nyingine zenye ubia na Serikali ambazo hazitoi
gawio zianze sasa kutoa akieleza kuwa mantiki ya gawio ni kwamba kampuni
inafanya kazi na inapata faida, inapokuwa haitoi gawio mantiki yake ni
kwamba kampuni inafanya kazi haipati faida.
“Lakini
ni vigumu kuamini kama kampuni hazipati faida kwa mfululizo wa miaka 10
na inafanya kazi, sisi tunaamini wanapata faida, na zipo kampuni nyingi
ambazo si busara kuzitaja hapa zinadai kupata hasara kila mwaka,”
alisema.
Kuhusu
upotevu wa mafuta bandarini, Dk. Kalemani alisema tatizo hilo hivi sasa
limedhibitiwa, baada ya Serikali kuanzisha chombo maalumu kinachoratibu
na kudhibiti upotevu huo.
Alikuwa
akijibu changamoto iliyotolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Puma Energy,
Dkt. Ben Moshi, aliyeelezea kuwa katika kipindi cha mwaka 2014/2015
kampuni hiyo imepata hasara ya Dola za Marekani milioni 1.4 ambazo ni
zaidi ya Sh bilioni 2.5 kutokana na upotevu huo wa mafuta.
Kwaupande
wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Tiper (T),
inayojihusisha na uhifadhi wa mafuta, ambapo amesema tangu mwaka 2010,
kampuni hiyo imetoa gawio la shilingi Bil. 6.4 kwa serikali na kuahidi
kuwa gawio hilo litaongezeka siku za usoni.
Naye
Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Ineke Bussemaker, amesema kuwa benki yake
inajisikia fahari kubwa kugawa faida iliyopata katika biashara zake kwa
mbia wake ambaye ni serikali.
Amesema
kuwa pamoja na serikali kuwa mbia kwa hisa ya asilimia 31.8, lakini pia
ni mteja mkubwa wa benki hiyo ambayo hurudisha faida ya uwekezaji kwa
wananchi kupitia gawio hilo na kutoa wito kwa watanzania kuitumia benki
hiyo kuweka amana na kukopa
Hafla
hiyo imehudhuriwa pia na Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji,
Charles Mwijage ambaye ametoa wito kwa wawekezaji wakiwemo wale
wanaofanya biashara zao kwa kushirikiana na serikali kufanyakazi zao kwa
uaminifu kwa kutangaza faida wanazopata kihalali ili serikali iweze
kupata mapato yake yatakayosaidia kuboresha maisha ya wananchi
Naye
Msajili wa Hazina, Laurence Mafuru, ameahidi kuyafuatilia na kuyasimamia
mashirika yote ya umma na yale ambayo serikali imewekeza, ili
kuhakikisha kuwa hawakwepi kulipa gawio ili kuiwezesha serikali kupata
mapato yake
Imetolewa na
Benny Mwaipaja
Kaimu Msemaji wa Wizara ya Fedha na Mipango.
Msajili
wa Hazina, Laurence Mafuru, akifafanua jambo wakati wa Hafla fupi ya
serikali kukabidhiwa Hundi za Mfano zenye thamani ya shilingi Bilioni 23
kutoka kwa Kampuni za Puma Energy, Tiper (T) na NBC Bank PLC, ambazo
imewekeza hisa zake, katika ukumbi wa Hazina Mjini Dodoma
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni ya Puma Energy Dkt Ben Mosha,
akizungumza Jambo wakati wa Hafla fupi ya serikali kukabidhiwa Hundi za
Mfano zenye thamani ya shilingi Bilioni 23 kutoka kwa Kampuni za Puma
Energy, Tiper (T) na NBC Bank PLC, ambazo imewekeza hisa zake, katika
ukumbi wa Hazina Mini Dodoma
Naibu Waziri wa Nishati na Mdini Dk. Medard Kalemani, akizungumza jambo wakati
wa Hafla fupi ya serikali kukabidhiwa Hundi za Mfano zenye thamani ya
shilingi Bilioni 23 kutoka kwa Kampuni za Puma Energy, Tiper (T) na NBC
Bank PLC, ambazo imewekeza hisa zake, katika ukumbi wa Hazina (Treasury
Squire) Mjini Dodoma
Waziri
wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango(Mb), (Katikati) akimwelekeza
jambo Msajili wa Hazina Laurence Mafuru, wakati wa Hafla fupi ya
serikali kukabidhiwa Hundi za Mfano zenye thamani ya shilingi Bilioni 23
kutoka Kampuni
za Puma Energy, Tiper (T) na NBC Bank PLC, ambazo imewekeza hisa zake,
katika ukumbi wa Hazina (Treasury Squire) Mjini Dodoma
Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhe. Charles Mwijage (Mb)
akizungumza jambo wakati wa Hafla fupi ya serikali kukabidhiwa Hundi za
Mfano zenye thamani ya shilingi Bilioni 23 kutoka Kampuni za Puma
Energy, Tiper (T) na NBC Bank PLC, ambazo imewekeza hisa zake, katika
ukumbi wa Hazina (Treasury Squire) Mjini Dodoma
No comments:
Post a Comment