Na Mwandishi Maalum, New York
Umoja
wa Mataifa na Shirika la Afya Duniani ( WHO), ni baadhi ya Taasisi
za Kimataifa ambazo zimeanza kutekeleza kwa vitendo sehemu ya
mapendekezo na ushauri uliotolewa na Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu
Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya.
“
Tumeanza kutekeleza baadhi ya mapendekezo ya Jopo lililokuwa chini ya
Uenyekiti wa Rais Mstaafu wa Tanzania, Mhe, Jakaya Mrisho Kikwete.
Mhe. Rais nakushukuru sana kwa uongozi wako, ushiriki wako na mchango
wako. Nimefarijika kwamba umeweza kuungana nasi katika mkutano huu
kutokea Senegal, kuzungumzia mapendeko ya Jopo lako”. Akasema Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Ban
Ki Moon, ameyasema hayo, jana ( jumatatu) wakati wa mkutano usio
rasmi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ulioandaliwa na Rais wa
Baraza hilo, Bw Mogens Lykketoft kwa lengo la kupokea Ripoti ya
Katibu Mkuu kuhusu uimarishaji na usanifu wa huduma za Afya Kimataifa:
utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo la Ngazi ya juu kuhusu Mwitikio wa
Kimataifa wa Majanga ya Kiafya.
Baadi
ya mambo ambayo yameanzwa kutekelezwa kwa mujibu wa Katibu Mkuu
yanahusu Shirika la Afya Duniani ambapo katika mapendekezo yake, Jopo
limeainisha kutambua kuwa WHO inabaki kuwa taasisi kiongozi
linapokuja suala la afya wakati wote na hususani wakati wa majanga ya
dharura ya milipuko ya magonjwa.
“
Jopo limependekeza kuwa uwezo wa WHO katika kuitika yanapotokea
majanga ya dharura ya kiafya unatakiwa kuimarishwa wakati wote na
kutokana na mapendekezo ya Jopo WHO imeanzisha mpango wa dharura,
unaokipa chombo hicho uwezo wa kuwajibika kwa haraka na kwa wakati
pale unapotokea mlipuko wa ugonjwa”. Amebainisha Ban Ki Moon.
Pendekezo
la pili mbalo limeanza kufanyiwa kazi na Umoja wa Mataifa ni lile la
kuimarisha mifumo ya Umoja wa Mataifa hususani wakati wa matukio ya
dharura yanayohusu milipuko ya magonjwa hivyo kuwa na uwajibikaji
wa pamoja kupita Taasisi zake.
“
Tatu nimeridhishwa na hatua ya Banki ya Dunia ya kuzindua mpango wa
dharura wa uwezeshaji wa kifedha pale yanapotokea majanga ya dharura
ya kiafya, ni mpango ambao utatoa uhakika fedha dhidi ya majanga na
utafanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na WHO”. Ameeleza Ban Ki
Moon.
Akielezea zaidi kuhusu mapendekezo yaliyopendekezwa na Jopo lililoongozwa na Rais mstaafu Kikwete. Ban Ki Moon amesema.
“
Mwezi April mwaka jana, niliunda Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu ya
Mwitikio wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya ili litoe mapendekezo
ya namna ya kuimarisha mifumo ya kitaifa na kimataifa katika kuzuia
na kudhibiti changamoto za majanga ya kiafya katika siku za
baadaye.Mwezi februari mwaka huu, Jopo liliwasilisha Ripoti yake
ikianisha mapendekezo 27 yanayotakiwa kufanyiwa kazi kuanzia ngazi ya
taifa, kanda na kimataifa”.
Mkuu
huyo wa Umoja wa Mataifa, ameyataja baadhi ya maeneo ambayo
yamesisitizwa na Jopo kuwa ni pamoja na, kuifanya mifumo na miundo
mbinu ya utoaji wa huduma za afya kuwa imara na katika hali ya
utayari wakati wote kukabiliana na majanga ya dharura, umuhimu wa
tafiti za kisayasi, uhakika wa raslimali fedha ya kutosha na uwezeshaji
kupitia miradi ya maendeleo.
Kwa
mujibu wa Ban Ki Moon, mapendekezo ya Jopo hilo yamepitiwa kwa
uangalifu mkubwa kupitia majadiliano miongoni mwa, na baina ya
Taasisi za Umoja wa Mataifa.
Na
baada ya majadiliano hayo, Mkuu huyo wa UM ameandaa taarifa yake
ambayo imepewa kichwa cha : Uimarishaji wa Mifumo ya Afya ya Kidunia:
Utekelezaji wa Mapendekezoya Jopo la Ngazi ya Juu kuhusu Mwitikio
wa Kimataifa wa Majanga ya Kiafya.
“
Jopo lililongozwa na Mhe Kikwete limetupatia mapendekezo ya msingi
na yenye tija ambayo kwayo ni kwa namna gani mifumo ya kijamii,
kitaifa na kimataifa itakavyoweza kwa njia sahihi kujiandaa kukabiliana
na majanga ya dharura ya kiafya katika siku za usoni. Mimi binafsi
ninataka kujihusisha kikamilifu katika utekelezaji wa mapendekezo ya
Jopo hili” akasisitiza Katibu Mkuu.
Na
katika kuhakikisha kwamba utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo
yanasimamiwa na kufuatiliwa kwa ukaribu, Ban Ki Moon ameunda Kikundi
kazi kitakachojulikana kama Global Health Crises Task Force ambacho
moja ya majukumu yake makuu yatakuwa ni pamoja na kufuatilia, ku-
ratibu na kuunga mkono utekelezaji wa mapendekezo ya Jopo.
Kikundi
kazi hicho kitaongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw,
Jan Eliasson, Mkurugenzi Mkuu wa WHO. Dr. Margareth Chan, Dr. Jim Yong
Kim Rais wa Banki ya Dunia, na Dr. David Nabarro, ambaye ni Mshauri
Maalum wa Katibu Mkuu kuhusu utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo
Endelevu ( Agenda 2030) na Makubalino kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi
( Paris Agreement ).
Kwa
upande wake, akiongea kwa njia ya mtandao video ( Video Conference)
kutoka nchini Senegal,Mwenyekiti wa Jopo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho
Kikwete pamoja na kumshukuru, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kwa
kumkabidhi jukumu hilo pia alianisha baadhi ya mambo kadhaa ambayo
Jopo lake liligundua wakati wa utekelezaji wa hadidu za rejea.
Baadhi
ya mambo ni pamoja na, WHO kuchelewa kutamka haraka na kwa wakati
kwamba kuibuka kwa ugonjwa wa Ebola kulikuwa ni janga la kimataifa na
lilotakiwa kuchukuliwa hatua za haraka kuzuia maafa yaliyojitokeza.
Kwamba, WHO haina raslimali fedha jambo ambalo inabidi itegemee zaidi michango na hisani za mataifa makubwa.
Kwamba,
nchi nyingi hususani zile zinazoendelea mifumo na miundo mbinu ya
utoaji wa huduma za afya zikiwamo za afya ya msingi bado ni dhaifu mno
kiasi kwamba kwa vyovyote vile ilishindwa , inashindwa na itashindwa
kukabiliana na changamoto za majanga ya dharura ya milipuko ya
magonjwa kama vile ilivyokuwa kwa Ebola na sasa Zika na tishio la Homa
ya ugonjwa wa manjano.
Rais
Mstaafu Kikwete katika maelezo yake, amesititiza kwamba, udhaifu
huo hauishi katika nchi moja moja bali pia unakwenda hadi ngazi ya
Kikanda na Kimataifa.
“
Jopo letu limegundua kwamba, maisha ya mamilioni ya watu yatakuwa
katika hatari kubwa sana na dunia itakuwa katika mashaka makubwa pale
ambapo janga kubwa la magonjwa ya dharura yatakapoibuka na kukuta
mifumo na miundo mbinu ya utoaji wa huduma za afya haijaimarishwa
vya kutosha kukabili changamoto hiyo”. Amesisitiza Rais Mstaafu
Akaongeza
Kikwete kwa kusema “ Ni matumaini yangu kuwa mapendekezo 27
yaliyotolewa na Jopo nililoliongoza yatatusaidia kufika huko tunakotaka
kufika. Uungaji mkono wako binafsi Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa, pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu la Umoja
wa Mataifa, ukichagizwa na utashi wa kisiasa wa viongozi mbalimbali
katika ngazi ya juu kadri itakavyowezekana utasaidia sana katika ufanya
mambo yaende”.
Ni
katika kutambua uzito wa dharura itokanayo na magonjwa ya milipuko,
MwenyeKiti wa Jopo Kikwete amesema Jopo limependekeza pia kwamba
kwanza, kuanzishwe Baraza la Ngazi ya Juu Kuhusu Majanga ya Dharura
ya Afya ya Jamii, na pili, kuitishwa kwa Mkutano wa Ngazi ya Juu
kuhusu Majanga ya Kiafya mwaka 2018.
No comments:
Post a Comment