Na Jacquiline Mrisho-MAELEZO.
Baada
ya mtafaruku mkubwa kutokea katika Kijiji cha Chasimba kilichopo katika
Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam na kuwaacha wakazi wa eneo hilo
katika hali ya sintofahamu juu ya maisha yao ya siku zijazo, wakazi wa
eneo hilo wamepata ahueni baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Mhe.Willium Lukuvi kuingilia kati na kutoa suluhu ya mtafaruku
huo.
Mgogoro
huu baina ya wananchi wa Kijiji cha Chasimba na mwekezaji wa Kiwanda
cha Saruji cha Twiga, Bw. Alfonso Rodriguez kilichopo Wazo Hill ambao
ulianza takribani miaka 15 iliyopita baada ya Mkurugenzi huyo kugundua
kuwa wananchi wamevamia eneo lake na kujenga makazi yao.
Hayo
yalitokea baada ya kiwanda hicho kushindwa kuilinda mipaka yake kwa muda
mrefu na kusababisha wananchi kujenga maeneo hayo na kukaa kwa muda
mrefu sana hali iliyowapelekea kujiona kama wana haki na eneo hilo na
kukataa kuhama.
Mkurugenzi
Msaidizi Usanifu wa Miji na Uendelezaji Upya Maeneo wa Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bi. Immaculata Senje alisema kuwa eneo
hilo ni mali ya mwekezaji wa Kiwanda hicho.
"Ni
ukweli usiofichika kuwa eneo hili la Chasimba ni mali ya mwekezaji na
ana hati ya mwaka 1957 aliyopewa na Wizara yetu inayoonyesha ukubwa na
mipaka ya eneo lake kwahiyo wananchi ndio wavamizi wa eneo hilo".anakiri
Bi. Senje.
Mgogoro
huo ulileta tafrani kubwa baada ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi William Lukuvi kutoa agizo kuwa wananchi waliojenga katika
eneo hilo wahame mara moja na kwenda eneo ambalo wamepangiwa na Wizara
ambapo takribani wakazi 30 waligoma kuondoka katika eneo hilo na kuamua
kwenda mahakamani kudai haki yao, hatua ambayo haiukupata suluhu ya
mgogoro.
Ili
kuwasaidia wakazi wa Chasimba, Waziri Lukuvi aliamua kuingilia kati kwa
kufanya mazungumzo ya amani na muwekezaji wa kiwanda hicho ambapo
alimuomba Mkurugenzi huyo kuwaachia wakazi wa Chasimba sehemu hiyo kwa
makubaliano maalumu watakayoafikiana.
Hatimaye
mazungumzo baina ya wawili hao yalileta picha mpya kwa wakazi wa
Chasimba baada ya Muwekezaji kukubali kuachia sehemu ya eneo lake kwa
ajili ya makazi ya wananchi hao.
Mnamo
Mei 13 mwaka 2015 ulifanyika Mkutano wa hadhara wa kutangaza kurudisha
eneo hilo kwa wananchi, mkutano huo uliokutanisha uongozi wa wizara,
uongozi wa kiwanda cha saruji, uongozi wa Manispaa ya Kinondoni, Shirika
la Umeme Tanzania, Idara ya Maji, Polisi, Mbunge wa Kawe Halima Mdee
ambao walipewa maagizo mbele ya wakazi wa Chasimba ya kupanga eneo hilo
kuwa la makazi.
"Sasa
natamka rasmi kuwa ardhi hii imerudishwa kwa wananchi na
imeshabadilishwa kutoka kuwa ardhi ya biashara na kuwa ardhi ya makazi
kwahiyo nimeongozana na wahusika ambao watalipanga eneo hili kwa
kuzingatia dhana ya mpango shirikishi ambapo kamati ya wananchi
itashirikiana na wataalamu wa wizara yetu katika upangaji wa eneo hilo
ili kuwezesha uwekaji wa huduma za jamii",alisema Lukuvi.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bw. Rodriguez anakiri kuwa
mgogoro huo ulikuwa ni wa mda mrefu na umekuwa ukiwanyima usingizi
kwahiyo, alimpongeza Waziri Lukuvi kwa kumaliza mgogoro huo na
kuwaahidi wakazi hao kushiriki katika ujenzi wa miundombinu.
Hatimaye
eneo la Chasimba sasa limekuwa rasmi la wakazi wa Chasimba, eneo hilo
lina takribani Kaya 4,096, wastani wa watu watano kila kaya na jumla ya
takribani watu 20,480.
Akizungumzia hatua hiyo, Mkazi mmoja wa Chasimba Juma Athumani alieleza kufurahi baada ya mgogoro huo kuisha.
"Nimeishi
hapa kwa miaka 30, sasa nina watoto 11 na wajukuu kadhaa katia eneo
hili, hapo awali mwekezaji aliposema tutoke kuwa eneo hili ni lake
nilikua sielewi kabisa lakini nimefurahi sana kwa hatua hii
iliyofikiwa". Alisema Athumani.
Tangu
kuisha kwa mgogoro huu Mwezi Mei mwaka 2015, wizara inajitahidi kuendana
na kasi ya "hapa kazi tu" iliyotolewa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano
wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuanza kupima viwanja kwa
ajili ya wananchi hao ambapo hadi kufikia Mei 31 mwaka 2016 jumla ya
viwanja 491 vimeshapimwa kati ya viwanja 2180 vinavyotarajiwa kupimwa
katika eneo hilo.
Wizara
ina malengo ya kumaliza kupima viwanja hivyo ifikapo mwishoni mwa mwezi
Septemba mwaka huu na baada ya hapo wananchi hao wataletewa huduma za
kijamii zikiwemo za Afya, shule,sehemu za kuabudu,viwanja vya
michezo,miundombinu ya umeme, maji pamoja na barabara.
Wizara
inawataka wananchi kuwa wavumilivu na kuacha kulalamika kwa kuwa wizara
inaendelea na kazi katika eneo hilo na kila kitu kinaenda kwa wakati
kwamba baada ya upimaji wa maeneo kuisha ndipo huduma za kijamii
zitafuata.
Mkurugenzi
Immaculata alisema "wakazi wa Chasimba mnatakiwa kuelewa kuwa kila kitu
kinatakiwa kufanywa kwa kufuata sheria kwahiyo lazima twende taratibu
ili kuepuka migogoro mingine kutokea, tunawasihi wakazi wa kijiji hicho
kusubiri upimaji uishe ndipo huduma za kijamii zifuate".
Kila
Mtanzania anahitaji kuishi kwa amani na utulivu katika sehemu
aliyoichagua na kuiridhia lakini kutokana na nchi kuongozwa na sheria
katika kila jambo basi hakuna budi kufuata sheria za ardhi zilizowekwa
ili kuepuka usumbufu pamoja na migogoro inayopelekea kuwa na ugomvi na
mauaji yanayosababisha amani kutoweka na kurudi nyuma kwa maendeleo ya
mtu mmoja au Taifa zima.
Wahenga
wanasema,"heshimu wenzio ili nawe uheshimiwe", shukrani kwa wakazi wa
Chasimba kuwa wavumilivu wakati Serikali inakamilisha taratibu za
kuendeleza eneo hilo kwa kupima viwanja halali na baadae kuwekewa
miundombinu ya kijamii .
Lakini
pia ni vyema wakazi hao wakafuata sheria ili kuhakikisha kwamba hakuna
mtu au mamlaka yoyote itakayowasumbua kwenye eneo lao ambalo watakuwa
wakilimiki kihalali.
No comments:
Post a Comment