HOTUBA YA WAZIRI MKUU, MHE. KASSIM M. MAJALIWA (MB), KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA 2016/2017
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, naomba
kutoa Hoja kwamba kutokana na taarifa zilizowasilishwa leo katika Bunge
lako Tukufu na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na
Sheria na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI
zilizochambua Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Bunge
lako sasa lipokee na kujadili Taarifa ya Mapitio ya Utekelezaji wa Kazi
za Serikali kwa Mwaka 2015/2016 na Mwelekeo wa Kazi za Serikali kwa
Mwaka 2016/2017. Vilevile, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na
Taasisi zilizo chini yake kwa mwaka 2016/2017.
2. Mheshimiwa Spika, huu
ni Mkutano wa Bunge wa kujadili Bajeti ya Serikali baada ya Uchaguzi
Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba, 2015. Hivyo naomba nitumie fursa hii
kuwashukuru Watanzania kwa kuendelea kuwa na imani na Chama Cha
Mapinduzi na hivyo kukiwezesha kushinda na kukipa tena ridhaa ya kuunda
Serikali na kuiongoza Nchi yetu. Aidha, kwa njia ya pekee napenda
kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa
kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuongoza Serikali ya Awamu
ya Tano. Pia, nampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuchaguliwa
kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile,
nampongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Aidha, nampongeza
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa
Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Nawapongeza Mawaziri na Naibu
Mawaziri kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo muhimu.
Nawahakikishia
wananchi wote kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itawatumikia kwa nguvu
zake zote bila kujali itikadi zao za kisiasa.
3. Mheshimiwa Spika, kipekee
naomba kutumia fursa hii kumshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa
kuniteua kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
na uteuzi huo kuungwa mkono na Waheshimiwa Wabunge kwa asilimia 73.
Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais na Waheshimiwa Wabunge pamoja na
wananchi kwamba sitawaangusha.
4. Mheshimiwa Spika, napenda kukupongeza wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha,
nampongeza Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson Mwansasu (Mb.), kwa kuchaguliwa
kuwa Naibu Spika. Pia, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa
kuchaguliwa kuwa Wawakilishi wa Wananchi katika Bunge hili. Jukumu
lililo mbele yetu sote ni kuwatumikia wananchi waliotuchagua ili
kuwaletea maendeleo.
5. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2015/2016, Nchi yetu imekumbwa na majanga mbalimbali
yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali. Nitumie fursa hii kumuomba
Mwenyezi Mungu awajalie wale walioumia kupona haraka na kurejea katika
shughuli za ujenzi wa Taifa. Ninawapa pole wote waliofiwa na ndugu,
jamaa na marafiki. Tunamuomba Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu
mahali pema peponi. Amina!
6. Mheshimiwa Spika, nawashukuru
Wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge kwa kupitia kwa kina Makadirio ya
Matumizi ya Wizara, Mikoa, Wakala, Idara za Serikali zinazojitegemea na
Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kipekee, nitumie nafasi hii, kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Katiba na
Sheria inayoongozwa na Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa
Rufiji; Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na
Mheshimiwa Hasna Sudi Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini na Kamati ya
Bajeti inayoongozwa na Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa
Mtwara Vijijini. Kamati hizo zimetoa mchango mkubwa wakati wa maandalizi
ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu.
Pia, naomba niwapongeze Wenyeviti na Makamu wenyeviti wa Kamati za
Kudumu za Bunge kwa kazi kubwa ya kupitia makadirio ya sekta zote. Maoni
na ushauri wao umesaidia sana katika kuboresha Makadirio ya bajeti ya
Serikali.
7. Mheshimiwa Spika, makadirio ya bajeti ninayowasilisha leo ni
mwendelezo wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi
ya mwaka 2015. Ilani hiyo, imeainisha ahadi ambazo Serikali ya Chama Cha
Mapinduzi itazitekeleza katika miaka mitano
ijayo. Aidha, makadirio ya Bajeti yamezingatia ahadi za Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
alizotoa wakati wa Kampeni na katika uzinduzi wa Bunge la Kumi na Moja,
tarehe 20 Novemba 2015. Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kufikia
malengo yaliyokusudiwa ya kujenga Taifa imara kiuchumi na maendeleo ya
watu katika Kanda ya Afrika Mashariki na Barani Afrika kwa ujumla.
MWELEKEO WA SERIKALI YA AWAMU YA TANO
8. Mheshimiwa Spika, kabla
ya kuwasilisha mapitio ya kazi za Serikali kwa mwaka 2015/2016 na
mwelekeo kwa mwaka 2016/2017, niruhusu kupitia Bunge lako Tukufu
niwakumbushe Watanzania wote kuhusu dhima ya Serikali ya Awamu ya Tano
yenye falsafa ya “Hapa Kazi Tu”. Sote tunatambua kwamba ili Tanzania
ifikie Nchi yenye Uchumi wa Kipato cha Kati ifikapo mwaka 2025 ni sharti
kila mmoja wetu afanye kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu wa hali ya
juu.
9. Mheshimiwa Spika, ili
yawepo mapinduzi ya kweli ya kuelekea kwenye uchumi wa kati
tunaodhamiria ni lazima tuimarishe uwajibikaji na maadili kwa Viongozi,
Watendaji na kwa kila Mtanzania. Sote tumeshuhudia hatua zinazochukuliwa
na Serikali dhidi ya Watumishi wasio waadilifu wanaotumia fedha za umma
au madaraka yao vibaya na kukwamisha utekelezaji wa mipango ya
maendeleo tunayojiwekea. Hatutaweza kufikia uchumi wa kati unaoendeshwa
kwa viwanda kama tutaendelea kulea uzembe, ubadhirifu, uvivu na kukwepa
wajibu wetu. Ndiyo maana, tumeanza kwa nguvu kuimarisha nidhamu,
uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma ili zielekezwe kwenye
shughuli zenye manufaa kwa Watanzania walio wengi na siyo vinginevyo.
10. Mheshimiwa Spika, pamoja
na kuimarisha ufanisi na tija ndani ya utumishi wa umma, tumebaini kuwa
changamoto ya utamaduni usioridhisha wa ufanyaji kazi upo katika sekta
zote, za umma na binafsi. Wizi, uzembe, udhuru wa kila siku na huduma
mbaya kwa wateja ni baadhi ya malalamiko ya wawekezaji hapa nchini.
Tabia hizi ni lazima zikemewe kama tunataka nguvu kazi yetu ipate ajira
katika zama hizi tunazohamasisha mapinduzi ya viwanda. Hivyo, ni wajibu
wa kila mmoja wetu katika jamii kusimamia maadili na makuzi ya vijana
ili nguvu kazi hii iweze kutumika ipasavyo kuchangia ukuaji wa uchumi.
11. Mheshimiwa Spika, imani
yetu ni kwamba tumeanza vizuri kwenye suala la kuongeza uwajibikaji na
maadili ndani ya Serikali. Serikali itaendelea kuwawajibisha wale wote
ambao hawataendana na Falsafa na Mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Jambo la msingi ni kwamba tutachukua hatua kwa kufuata Sheria, Kanuni na
Taratibu za Utumishi wa Umma. Niwahakikishie Watanzania kwamba hakuna
mtumishi au mwananchi atakayeonewa au kunyanyaswa katika zoezi hili.
Hivyo, wale wote ambao wako safi waendelee kutimiza wajibu wao bila
woga. Kazi zifanyike kwa weledi na kwa kasi bila urasimu.
12. Mheshimiwa Spika, Serikali
inachukua hatua za kuongeza mapato na kuziba mianya ya ukwepaji kodi
ambazo zimeonesha manufaa makubwa. Mathalan, hatua tulizochukua za
kubana mianya ya ukwepaji kodi zimeimarisha makusanyo ya mapato ya ndani
kutoka wastani wa Shilingi Bilioni 870 mwezi Novemba, 2015 na kufikia
Shilingi trilioni 1.3 mwezi Machi, 2016. Tunaendelea kuimarisha ukusanyaji mapato kwa njia za kielektroniki, kuziba
mianya ya ukwepaji kodi na kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kila
anayetakiwa kulipa kodi alipe na fedha hizo zitumike kutekeleza mipango
ya maendeleo. Vilevile, Serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za
kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kusimamia matumizi sahihi ya rasilimali. Fedha zinazopatikana zitaelekezwa kwenye miradi ya kipaumbele yenye kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.
13. Mheshimiwa Spika, uchumi
wa viwanda utajengwa na Sekta Binafsi. Kazi ya Serikali ni kuhakikisha
kunakuwa na mazingira rafiki kwa sekta hiyo kuwekeza. Hivyo, Serikali
itaendelea kubuni na kutekeleza miradi itakayowezesha sekta binafsi
kuwekeza bila vikwazo. Miradi hiyo ni pamoja na miundombinu muhimu ya
uchukuzi na usafirishaji, umeme, mawasiliano na maji kwa ajili ya
uzalishaji na biashara. Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia
wawekezaji wote nchini na wengine wanaokusudia kuwekeza kwamba Serikali
imedhamiria kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi. Hatua zote
zinazochukuliwa sasa ni za kuhakikisha kwamba sekta binafsi inawekewa
mazingira wezeshi na yenye ushindani wa haki ili iweze kuimarika.
SIASA
14. Mheshimiwa Spika, mtangamano
wa kisiasa ni nguzo muhimu katika kujenga Nchi yenye maendeleo makubwa
na ya uhakika. Mtangamano wa kisiasa unajumuisha siasa safi,
za kiustaarabu na zinazoheshimu mawazo ya kila mmoja wetu. Siasa za
aina hii ndiyo chimbuko la mustakabali wa amani na utulivu wa Taifa letu
tangu tujipatie uhuru. Ni jambo la faraja na kufurahisha kwamba, pamoja
na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kujaa tashwishwi na ushindani mkubwa,
Taifa letu limeendelea kuwa na amani, utulivu na mshikamano mkubwa
Kitaifa kiasi cha kupigiwa mfano Barani Afrika na dunia kwa ujumla. Hali
hii inaonesha kukua na kuimarika kwa demokrasia ya vyama vingi vya
siasa nchini ambapo hadi sasa vipo vyama 22 vyenye usajili wa kudumu na
vyama vitatu vyenye usajili wa muda na vingine sita vimewasilisha maombi
ya usajili wa muda.
15. Mheshimiwa Spika, Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2015 umesaidia kupima namna demokrasia inavyozidi kukua
na kupanuka kwani kwa mara ya kwanza kulikuwa na mwitikio mkubwa wa
kujitokeza kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi na wananchi
wengi kujiandikisha kupiga kura. Vyama nane vilisimamisha wagombea wa
nafasi ya Urais na vyama 22 Ubunge na Udiwani. Idadi ya wapiga kura
walioandikishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilikuwa 23,161,440, sawa na
asilimia 96.9 ya makadirio. Idadi ya watu waliopiga kura ilikuwa ni
15,596,110, sawa na asilimia 67.3 ya waliojiandikisha. Hii ni idadi
kubwa ya wapiga kura ikilinganishwa na chaguzi zote zilizopita. Hivyo,
naomba nichukue fursa hii kuipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kazi
kubwa na nzuri waliyoifanya kuanzia katika uboreshaji wa Daftari la
Wapiga Kura, ugawaji wa majimbo mapya ya uchaguzi, kutoa elimu kwa umma,
uandikishaji wa wapiga kura na kuusimamia kwa umakini mkubwa uchaguzi
wenyewe na kutangaza matokeo. Tume ilifanya kazi yake kwa uhuru na kwa
weledi mkubwa. Niwapongeze viongozi na wananchi wote walioshiriki
uchaguzi huo kwa amani na utulivu.
16. Mheshimiwa Spika, pamoja
na kazi nzuri iliyofanywa na Tume na wananchi kuitikia wito wa
kujiandikisha na kupiga kura, bado kulikuwa na idadi kubwa ya
waliojiandikisha lakini hawakupiga kura. Naiagiza Tume ya Uchaguzi
kufanya tathmini ya kina kubaini sababu zilizofanya wapiga kura zaidi ya
Milioni saba waliojiandikisha kupiga kura kutoitumia haki yao ya
Kikatiba. Hii itasaidia
kuboresha chaguzi zijazo kwani wananchi wana wajibu wa kutumia haki yao
ya msingi kuchagua viongozi wanaowataka. Aidha, tathmini itasaidia
kubaini iwapo kuna vikwazo vinavyowazuia baadhi ya watu kupiga kura ili
kwa pamoja tuviondoe. Ndani ya Bunge hili tupo wabunge wa Vyama
mbalimbali lakini kwa lengo moja tu la kuwawakilisha wananchi wetu na
kuishauri Serikali ili ipange mipango mizuri itakayoharakisha maendeleo
yao. Niseme tu kwamba sasa Uchaguzi Mkuu umekwisha na Serikali zetu zipo
madarakani kwa mujibu wa Katiba. Hivyo, tuienzi falsafa ya Mheshimiwa
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ya “Hapa Kazi Tu!” kwa kuchapa kazi na tusitoe nafasi kwa tofauti zetu
za kisiasa na kiitikadi kuwa kisingizio cha kukwamisha shughuli za maendeleo ya Nchi yetu.
17. Mheshimiwa Spika, dhamira
ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuendelea kukuza Demokrasia ili
kuwezesha ushiriki mpana wa wananchi katika kufanya maamuzi ya maendeleo
yao katika Taifa letu chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa. Hivyo,
Serikali inaandaa mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya
Siasa ya mwaka 1992 na Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010 kwa
lengo la kuondoa changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wake na
kuzifanya ziendane na hali halisi ya siasa nchini na kwa mtazamo wa
baadaye.
UCHUMI
Ukuaji wa Uchumi
18. Mheshimiwa Spika, malengo
yetu ya kufikia Nchi ya kipato cha kati na kufanyika mapinduzi makubwa
ya viwanda yanategemea sana utulivu wa uchumi. Kwa ujumla, ukuaji wa
uchumi umekuwa wa kuridhisha kwani mwaka 2015, uchumi ulikua kwa
asilimia 7.1 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.0 mwaka 2014. Sekta
zilizochangia katika ukuaji huo ni pamoja na Ujenzi, Mawasiliano, Fedha,
Uchukuzi na Nishati. Pamoja na ukuaji huu mzuri wa ujumla, Sekta ya
Kilimo inayoajiri zaidi ya asilimia 66.3 ya Watanzania wote wanaofanya
kazi ilikua kwa asilimia 3.4 tu mwaka 2014. Ukuaji huo mdogo unamaanisha
kwamba juhudi za ziada na kubwa zinahitajika ili sekta hii muhimu iweze
kutoa mchango mkubwa zaidi wakati tunapotekeleza Mpango wa Pili wa
Maendeleo. Historia ya maendeleo ya uchumi inatuambia kwamba, Sekta ya
Kilimo ina mchango mkubwa na muhimu kwenye mapinduzi ya viwanda. Hivyo
hatuna uchaguzi mwingine bali kuelekeza nguvu zaidi kwenye sekta hii ya
kilimo.
19. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla tutahitajika
kuongeza ufanisi na tija katika sekta zote za uzalishaji na utoaji
huduma ili malengo yetu ya ukuaji uchumi yafikiwe katika kipindi cha
miaka mitano ijayo. Katika kufikia azma hiyo, tutatekeleza sera
madhubuti za fedha na kodi zitakazowezesha mfumuko wa bei kuendelea
kushuka na kubaki katika tarakimu moja kama ilivyo sasa. Mathalan,
mfumuko wa bei mwaka 2015 ulifikia wastani wa asilimia 5.6
ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.1 kwa mwaka 2014. Mwelekeo huu
wa utulivu wa uchumi utavutia mitaji mingi kutoka Sekta Binafsi kuwekeza
kwenye sekta za kipaumbele, kuwezesha ongezeko la ajira na kupanua wigo
wa ulipaji kodi.
Mazingira Wezeshi ya Uwekezaji
20. Mheshimiwa Spika, awali
nilidokeza kwamba, uwekezaji kwenye viwanda na sekta nyingine za
kiuchumi utafanywa na sekta binafsi na jukumu la msingi la Serikali ni
kuweka mazingira wezeshi. Kwa msingi huo, Serikali ya Awamu ya Tano
itachukua hatua madhubuti na za haraka kupunguza muda, gharama na idadi
ya taratibu za kiutawala ambazo Wafanyabiashara na Wawekezaji hulazimika
kuzifuata ili kufanya biashara nchini. Taratibu zinapokuwa ngumu na
ndefu husababisha ongezeko la gharama za kufanya biashara na hivyo
kuwakatisha tamaa wawekezaji. Taarifa ya Wepesi wa Kufanya Biashara
duniani inayotolewa na Benki ya Dunia iliyochapishwa mwezi Novemba, 2015
inaonesha kwamba katika mwaka 2016, Tanzania imeshika nafasi ya 139
kati ya Nchi 189 Duniani. Hali hii haikubaliki kabisa. Hivyo, eneo hilo
litafanyiwa kazi haraka ili kuharakisha mapinduzi ya viwanda.
21. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali
itaimarisha utekelezaji wa Mpangokazi wa Kuboresha Mazingira ya
Biashara na Uwekezaji Nchini. Utekelezaji huo utazingatia maelekezo
aliyoyatoa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania, wakati wa mkutano na Wafanyabiashara
uliofanyika mwezi Desemba, 2015. Katika mkutano huo, pamoja na mambo
mengine, Mheshima Rais aliwataka watendaji kupunguza urasimu usio wa
lazima kwa wafanyabiashara na wawekezaji. Nitumie fursa hii kuwataka
Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuyatumia mabaraza ya biashara ya
Mikoa na Wilaya ili kuhakikisha juhudi shirikishi za uboreshaji wa
mazingira ya biashara zinatekelezwa hadi ngazi ya chini. Pia, nawataka
watumishi wa umma kuepuka kuwachelewesha kwa uzembe au makusudi
wawekezaji wenye nia njema ya kuwekeza nchini ili kuleta maendeleo
endelevu kwa wakati. Mtumishi yeyote wa umma atakayeendeleza urasimu
usio wa lazima hatavumiliwa.
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
22. Mheshimiwa Spika, azma
ya kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda
ni jambo la msingi. Hivyo, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya
ujasiriamali na kuwadhamini wajasiriamali wenye miradi inayokidhi vigezo
kwenye Taasisi za Fedha ili wapate mikopo yenye masharti nafuu. Pamoja
na hatua hizo, Mpango Maalum wa Ushiriki wa Watanzania katika miradi
mikubwa ya uwekezaji ulioandaliwa utatekelezwa. Mpango huo unalenga
kuhakikisha kwamba Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali za Nchi
yao kwa njia ya ubia kwenye miradi ya uwekezaji, ajira na kandarasi
mbalimbali zitakazotolewa na kampuni kubwa kwa Wazawa. Wananchi pia
wataendelea kuwezeshwa kupitia mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi
mbalimbali vya kiuchumi vya wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara
na wachimbaji wadogo wa madini inayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya
Jamii. Serikali imeruhusu Mifuko hiyo kutoa mikopo nafuu kwa wanachama
wa vikundi vinavyojiunga na Mifuko kunufaika na mafao ya afya na
pensheni yanayotolewa na mifuko husika.
23. Mheshimiwa Spika, Serikali
imehamasisha uanzishaji na usajili wa Vikundi vya Kiuchumi kama vile
Vyama vya Ushirika vya Kuweka na Kukopa (SACCOs) na Benki za Jamii
Vijijini (VICOBA). Serikali pia imesimamia uanzishwaji wa Taasisi
Mwavuli ya kusimamia VICOBA inayoitwa VICOBA FETA. Takwimu zilizotolewa
mwezi Februari 2016 na Taasisi hiyo zinaonesha kuwa kuna vikundi 100,000
vya VICOBA vyenye wanachama Milioni 2.2 na mtaji wa Shilingi trilioni
1.2. Ni jambo la kujivunia kwamba asilimia 79 ya wanachama wa VICOBA ni
wanawake.
24. Mheshimiwa Spika, moja
ya ahadi muhimu iliyopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015
ni kutenga Shilingi Milioni 50 kwa kila kijiji nchini zitakazotumika kwa
utaratibu wa mzunguko (Revolving Fund). Lengo ni kuwawezesha wananchi
kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji kupitia Ushirika wa
Kuweka na Kukopa na vikundi vingine vya kiuchumi. Uhakiki wa Vyama vya
Ushirika wa Kuweka na Kukopa uliofanywa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika
unaonesha kwamba idadi ya SACCOs zinazokidhi vigezo vya usajili nchini
imepungua kutoka 5,559 mwaka 2013 hadi 3,856 mwaka 2015. Kati ya hizo,
SACCOs 2,125 sawa na asilimia 55 zipo Vijijini na 1,740 zipo Mijini. Ni
dhahiri kwamba Mpango wa Shilingi Milioni 50 kwa kila Kijiji unahitaji
maandalizi mazuri, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uanzishaji na usajili
wa SACCOs na vikundi vya kiuchumi vinavyokidhi
vigezo, ili kuhakikisha kwamba fedha zinazotolewa zinawafikia walengwa
na zinatumika kwa shughuli zilizokusudiwa. Ninaziagiza Halmashauri zote
nchini ziweke orodha sahihi ya Vyama vya Ushirika wa Kuweka na Kukopa
vilivyosajiliwa kwa kila Kijiji na kuchukua hatua za kuwezesha
uanzishaji na usajili wa SACCOs zinazokidhi vigezo kulingana na shughuli
za uzalishaji katika Halmashauri husika.
25. Mheshimiwa Spika, napenda
kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba, maandalizi ya utekelezaji wa
Mpango huo yanaendelea vizuri katika kila Halmashauri. Tutatumia uzoefu
uliopatikana kwenye utekelezaji wa mifuko mingine, ukiwemo Mfuko wa
Kuwawezesha Wananchi na Kuongeza Fursa za Ajira maarufu kama “Mabilioni
ya JK”, ili changamoto zilizojitokeza zitusaidie kuboresha Mpango huu
mpya.
26. Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kuziwezesha Kaya maskini ili ziweze kupata mahitaji yao ya
msingi na kuongeza kipato kupitia Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya
Jamii (TASAF III). Tangu utekelezaji wa Mpango huo uanze kaya maskini
1,099,289 zimepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 164.8 kama ruzuku katika
Halmashauri 159 za Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Aidha,
kupitia Mpango wa Ajira za Muda kwa Kaya Maskini, iliandaliwa miradi
1,880 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 42.6 kutoka Halmashauri 40 za
Tanzania Bara na Zanzibar. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea
kufanya utambuzi na uandikishaji wa kaya maskini katika maeneo ambayo
hayakufikiwa.
Ajira
27. Mheshimiwa Spika, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015 imeweka umuhimu katika kupanua
fursa za ajira kwa kutumia rasilimali zilizopo nchini ili kila mwenye
uwezo wa kufanya kazi achangie kwenye uchumi na kupata kipato halali.
Msisitizo huo wa Ilani ya Uchaguzi unatokana na ukweli kwamba Utafiti wa
Hali ya Ajira Nchini wa mwaka 2014 umeonesha kuwa kiwango cha ukosefu
wa ajira kimepungua kutoka asilimia 11.7 mwaka 2006 hadi asilimia 10.3
mwaka 2014. Aidha, ukosefu wa ajira kwa vijana umepungua kutoka asilimia 14.2 mwaka 2006 hadi asilimia 11.7 mwaka 2014. Kiwango hicho bado ni kikubwa na tunaweza kufanya vizuri zaidi. Jitihada za Serikali za
kuvutia uwekezaji kwenye sekta mbalimbali na urasimishaji wa sekta
isiyo rasmi zitaendelezwa ili kupunguza zaidi kiwango cha ukosefu wa
ajira nchini.
28. Mheshimiwa Spika, moja
ya changamoto zinazosababisha ukosefu wa ajira ni vijana wetu
kutojengewa maarifa na ujuzi wa kuajiriwa na kuajirika. Hivyo, Serikali itaendelea kutekeleza Programu ya Miaka Mitano ya Kukuza Ujuzi Nchini
(2015/2016 – 2019/2020). Programu hiyo inalenga kuongeza idadi ya watu
wenye kiwango cha juu cha ujuzi kutoka asilimia 3 ya sasa hadi asilimia
12 inayotakiwa kuendesha uchumi wa viwanda. Vilevile, kupunguza idadi ya
watu wenye kiwango cha ujuzi wa chini kutoka asilimia 75 ya sasa hadi
54. Utekelezaji wa Programu hiyo utasaidia kupunguza pengo la mahitaji
ya rasilimali watu nchini ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya haraka ya
uchumi wa viwanda. Serikali itahakikisha kuwa suala la ukuzaji ajira linazingatiwa katika mipango yote ya uwekezaji
pamoja na mipango ya maendeleo ya kisekta katika ngazi zote. Hivyo,
nazielekeza Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi
za Umma, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha ukuzaji wa
ajira unakuwa ni agenda ya
msingi ya kudumu katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya maendeleo.
Tayari Mheshimiwa Rais amewaagiza Wakuu wa Mikoa kuhakikisha kwamba
vijana ambao ndiyo nguvu kazi kuu ya Taifa wanatumia fursa
itakayopatikana kutokana na Shilingi Milioni 50 zitakazotolewa kwa kila
kijiji kuanzisha miradi ya maendeleo ya kujipatia kipato.
VIJANA
29. Mheshimiwa Spika, vijana ni hazina na rasimali watu muhimu
kwa maendeleo ya Taifa letu. Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012,
inaonesha kuwa idadi ya vijana wenye umri kati ya miaka 15 na 35 ni
takribani Milioni 16.2, sawa na asilimia 35.1 ya Watanzania wote. Aidha,
Utafiti wa Nguvu Kazi wa mwaka 2014 unaonesha kuwa vijana ni asilimia
59 ya nguvu kazi ya Taifa. Matokeo ya tafiti hizo yanathibitisha kuwa
kuna umuhimu wa kuzingatia mahitaji ya vijana na ushirikishwaji wao
katika mipango ya maendeleo. Katika
mwaka 2014/2015 hadi 2015/2016, Serikali imewawezesha vijana kiuchumi
kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Hadi kufikia mwezi Machi 2016,
mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.6 imetolewa na Mfuko huo kwa
vikundi vya vijana 284 na mafunzo yametolewa kwa viongozi wa vikundi 2,552 kutoka Halmashauri
59. Vilevile, Serikali imetenga maeneo maalum ya shughuli za kiuchumi
na huduma kwa vijana katika Halmashauri 30 nchini.
30. Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha
dhana ya ushiriki na ushirikishwaji wa vijana katika shughuli za
maendeleo, Bunge la Kumi lilitunga Sheria Na. 12 ya Baraza la Taifa la
Vijana ya mwaka 2015. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba sasa Kanuni za utekelezaji wa Sheria hiyo zimekamilika. Hivyo, katika mwaka
2016/2017, Serikali itaendelea kuratibu uanzishwaji wa Baraza la Vijana
la Taifa na kuhimiza uanzishaji na uimarishaji wa SACCOs za vijana katika Halmashauri zote nchini na kuziwezesha kupitia Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Vijana na Taasisi za fedha.
31. Mheshimiwa Spika, Maadili
na Makuzi ya Vijana ni suala linalopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu
ya Tano. Hatuwezi kujenga uchumi imara wa viwanda, kuongeza fursa za
ajira na kuwa na matumizi sahihi ya rasilimali za umma kama jamii yetu,
hasa vijana hawatajitambua kwa kuwa waadilifu, wazalendo na wachapakazi. Serikali, itaendelea kuratibu utekelezaji wa Programu
ya Stadi za Maisha na Programu ya kujitolea kwa vijana ili kukuza
maadili, uzalendo na kujenga utamaduni wa kuchapa kazi kwa vijana.
WATU WENYE ULEMAVU
32. Mheshimiwa Spika, Serikali
inathamini mchango mkubwa wa watu wenye ulemavu katika maendeleo na
kwamba wana haki sawa ya kutumia fursa mbalimbali za kiuchumi, kijamii
na kisiasa. Katika kuzingatia azma hiyo, Serikali inatekeleza Sheria ya
Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010, ambayo, imewezesha kuundwa kwa
Baraza la Kitaifa la Ushauri la Watu wenye Ulemavu ili kuongeza ushiriki
wa Watu wenye Ulemavu katika maamuzi. Aidha, Kamati za kushughulikia
masuala ya watu wenye ulemavu zimeundwa katika ngazi za Mikoa,
Halmashauri, Kata, Mitaa na Vijiji kwa ajili ya kuratibu masuala muhimu
kwa watu wenye ulemavu katika maeneo husika.
33. Mheshimiwa Spika, pamoja
na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kuwalinda na kuwapatia fursa,
kumekuwepo na matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya watu wenye ulemavu
hususan watu wenye ualbino. Ukatili huo umesababisha watu wenye ualbino
kupoteza maisha na wengine kupata aina nyingine ya ulemavu wa kudumu.
Hali hiyo haikubaliki na haivumiliki katika jamii ya Watanzania.
Serikali inafanya jitihada kubwa kukomesha vitendo hivyo ikiwa ni pamoja
na kuwakamata wote wanaojihusisha na vitendo hivyo na kuwafikisha
katika vyombo vya sheria. Aidha, itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili
kubadili mitazamo na imani potofu kuhusu watu wenye ualbino na ulemavu
kwa ujumla. Napenda kusisitiza kwamba watu wenye ulemavu wana haki ya
kuthaminiwa utu wao na kulindwa dhidi ya ukatili na aina yoyote ya
ubaguzi.
34. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali itaviboresha Vyuo vya Ufundi na Marekebisho (Vocational and Rehabilitation Training Centres) vya
watu wenye ulemavu nchini ili kutoa ujuzi unaoendana na mahitaji yao
katika soko la ajira. Serikali pia, itaandaa walimu wa elimu maalum na
kutoa vifaa saidizi kwa walimu na wanafunzi wenye ulemavu mashuleni. Kwa
sasa Serikali imeanzisha utaratibu wa kuwahabarisha watu wenye usikivu
hafifu kwa kuanzisha tafsiri za matangazo kwa njia za alama. Hivyo,
wamiliki wote wa Televisheni wametakiwa kuajiri wakalimani.
KAZI NA HIFADHI YA JAMII
Kazi
35. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na viwango vya kazi kwa
kufanya kaguzi ili kuhakikisha waajiri wanazingatia mikataba ya ajira,
masaa ya kazi, likizo na ujira kwa lengo la kupunguza migogoro na
kuongeza tija. Hadi kufikia Machi 2016, jumla ya kaguzi za
kazi 1,305 zilifanyika na migomo 23 katika sekta za usafirishaji,
viwanda, ujenzi na kwenye migodi ilisuluhishwa na kupatiwa ufumbuzi.
Aidha, kaguzi za kawaida 4,670 na kaguzi maalum 17,005 zilizojumuisha
kaguzi za umeme, mitambo na vipimo vya mazingira ili kuhakikisha
wafanyakazi wanakuwa na afya njema na usalama mahala pa kazi
zilifanyika.
36. Mheshimiwa Spika, Sheria
ya Kuratibu Ajira ya Wageni Na. 1 ya Mwaka 2015 ilitungwa na kumpa
Kamishna wa Kazi mamlaka ya kutoa vibali vya kazi nchini ili kukuza
fursa za ajira kwa Watanzania. Tangu Sheria hiyo ianze kutumika rasmi
tarehe 15 Septemba 2015 hadi mwezi Machi 2016, mapato yaliyopatikana
kutokana na vibali vya kazi vilivyotolewa nchini ni Shilingi Bilioni
21.01, sawa na asilimia 356 ya lengo la makadirio ya Shilingi Bilioni
7.5 kwa mwaka 2015/2016. Serikali pia imefanya kaguzi katika Makampuni
na Taasisi 400 zenye jumla ya wageni 3,939 na kubaini wageni 779 hawana
vibali vya kuishi na kufanya kazi nchini. Kati ya hao, wageni 29
waliondolewa nchini, 317 walipewa hati maalum (special pass), 77
walifikishwa mahakamani na 356 walielekezwa kukamilisha taratibu za
ukaazi wao kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Sheria ya Uhamiaji. Katika
mwaka 2016/2017, Serikali
itafanya kaguzi za kazi 56,200 katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini
na itaanzisha Bodi mbili za kupanga kima cha chini cha mishahara kwa
sekta ya umma na binafsi.
Hifadhi ya Jamii
37. Mheshimwa Spika, Sekta
ya Hifadhi ya Jamii ina mchango mkubwa katika uchumi wa Nchi yetu. Kwa
kutambua hilo, Serikali imeifanyia tathmini mifuko sita ambayo ni GEPF,
LAPF, NHIF, NSSF, PPF na PSPF kwa lengo la kupima uendelevu wake.
Tathmini hiyo imebainisha kuwa mifuko hiyo bado ni endelevu na
rasilimali zake zimefikia Shilingi trilioni 8.8. Aidha, Mamlaka ya
Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii imetoa miongozo ya
kupunguza gharama za uendeshaji wa Mifuko hiyo itakayoanza kutumika
Julai, 2016. Serikali imekamilisha uhakiki wa madeni ya PSPF
yaliyokuwepo kabla ya kuanzishwa kwa Mfuko huo mwaka 1999 yenye thamani
ya Shilingi trilioni 2.9. Hadi sasa,
Serikali imelipa
sehemu ya deni la PSPF kiasi cha Shilingi Bilioni 180 ili kuhakikisha
kwamba mafao ya wastaafu wa Mfuko huo yanalipwa kwa wakati. Serikali pia
itaendelea kulipa deni la Shilingi Bilioni 840.4 linalotokana na miradi
ya Serikali iliyogharamiwa na mifuko ya GEPF, LAPF, NHIF, NSSF na PPF.
38. Mheshimiwa Spika,
hadi sasa asilimia 6.5 ya Watanzania wote ndiyo wanaofikiwa na huduma
ya Hifadhi ya Jamii. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea
kutekeleza Programu ya Maboresho ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwa
kuongeza wigo wa wanaofikiwa na huduma hiyo. Hii ni pamoja na kujumuisha
makundi mengine katika jamii kama vile wazee na watu wenye ulemavu
ambapo rasimu ya andiko la mpango wa pensheni kwa makundi hayo
imekamilika. Hatua inayoendelea hivi sasa ni ushirikishwaji wa wadau na
taasisi zitakazohusika katika kutekeleza mpango huo. Aidha, Serikali
itaendelea kuhamasisha uchangiaji wa hiari na kusimamia uendeshaji wa
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuhakikisha inaendeshwa kwa kuzingatia
misingi ya utawala bora na kuchangia zaidi katika ukuzaji wa uchumi bila kuathiri mifuko.
SEKTA ZA UZALISHAJI MALI
Uzalishaji wa Mazao na Akiba ya Chakula
39. Mheshimiwa Spika,
sekta ya kilimo inayojumuisha uzalishaji wa mazao ya kilimo, mifugo,
uvuvi na mazao ya misitu ndio tegemeo la maisha ya watanzania walio
wengi. Hata hivyo, ukuaji wa sekta hiyo umekuwa siyo wa kuridhisha
kutokana na matumizi ya teknolojia isiyoendana na wakati na pia
kutegemea majaliwa ya Mwenyezi Mungu ya hali ya hewa. Pamoja na
changamoto hizo, hali ya upatikanaji wa chakula imeendelea kuwa ya kuridhisha katika maeneo mengi hapa nchini. Katika msimu wa 2014/2015, wakulima walizalisha
Tani Milioni 15.5 za mazao ya chakula. Kutokana na uzalishaji huo, Nchi
imejitosheleza kwa chakula kwa asilimia 120 kwani mahitaji ya chakula
kwa mwaka 2015/2016 ni Tani Milioni 12.95. Hali hii pia imetuwezesha
katika msimu huu kutoa chakula cha msaada na cha bei ya chini katika
maeneo yaliyopata upungufu wa chakula. Aidha, Wakala wa Taifa wa Hifadhi
ya Chakula - NFRA
iliuza jumla ya Tani 239,322 ya akiba yake kwa wafanyabiashara nchini
ili kukabiliana na mfumuko wa bei za vyakula hususan unga wa sembe
katika masoko ya mijini. Hadi
kufikia mwezi Aprili 2016, NFRA ilikuwa na akiba ya Tani 67,895 za
chakula. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itanunua Tani 100,000 kwa
ajili ya hifadhi ya chakula.
40. Mheshimiwa Spika,
Serikali imedhamiria kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa
kupanua na kuimarisha kilimo cha umwagiliaji ili kuzalisha zaidi kwa
ajili ya usalama wa chakula, kuuza ziada nje na kupata malighafi za
viwandani. Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015, inalenga kuongeza
eneo la umwagiliaji kutoka Hekta 461,326 za sasa hadi Hekta Milioni moja
ifikapo mwaka 2020. Ili kufikia lengo hilo, Serikali itashirikiana na
sekta binafsi katika kujenga, kukarabati na kuboresha miundombinu ya
umwagiliaji nchini.
Ruzuku za Pembejeo
41. Mheshimiwa Spika, ongezeko la tija katika uzalishaji wa mazao unategemea kwa kiasi kikubwa matumizi ya pembejeo zikiwemo mbolea na mbegu bora zenye ukinzani na ustahimilivu wa magonjwa na ukame; na zenye uwezo mkubwa wa kutoa mavuno. Katika
msimu wa 2015/2016, Serikali imetoa vocha milioni tatu za pembejeo za
kilimo zikiwemo Tani 10,271 za mbegu bora za mahindi na mpunga na Tani
99,923 za mbolea ambazo zimesambazwa katika mikoa 24 ya Tanzania Bara na
kunufaisha kaya 999,926. Ninawaagiza Wakuu wa Mikoa hiyo kuhakikisha
kuwa pembejeo hizo zinawafikia walengwa kwa wakati na zinatumika kama
ilivyotarajiwa na kuwachukulia hatua wale wote watakaohujumu mpango huu.
Benki ya Maendeleo ya Kilimo
42. Mheshimiwa Spika, mwezi
Agosti 2015, Serikali ilizindua Benki ya Maendeleo ya Kilimo ili
kuwawezesha wakulima kupata mikopo yenye riba nafuu. Benki hiyo inatoa
mikopo ya muda mfupi na muda mrefu kwa riba kati ya asilimia saba na 12
imeanza na mtaji wa Shilingi Bilioni 60. Mikopo inayotolewa na Benki
hiyo inalenga kusaidia kugharamia uandaaji wa mashamba, ununuzi wa
pembejeo za kilimo, usindikaji wa mazao pamoja na hifadhi ya mazao.
Serikali itaendelea kuiongezea mtaji Benki hiyo ili ikopeshe wakulima
wengi zaidi hasa kupitia vikundi vya wanawake na vijana vinavyojihusisha
na kilimo. Benki hiyo itasimamia kiasi cha Dola za Marekani Milioni 25
kwa ajili ya kudhamini mabenki ya biashara ili yaongeze ukopeshaji
kwenye miradi ya miundombinu ya masoko na kuendeleza
ubunifu kwenye miradi ya maendeleo vijijini chini ya Programu ya
Miundombinu ya Masoko, Uongezaji wa Thamani na Huduma za Kifedha
Vijijini (MIVARF). Vilevile, Benki hiyo itakuwa Wakala wa Serikali wa kusimamia fedha za ruzuku ya pembejeo.
Miundombinu ya Masoko
43. Mheshimiwa Spika, Serikali
itaimarisha utekelezaji wa Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji
Thamani na Huduma za Kifedha Vijijini (MIVARF) inayotekelezwa katika
mikoa yote ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar. Programu hiyo
inasaidia kuboresha miundombinu ya masoko, zikiwemo barabara na maghala
ya kuhifadhia mazao; kuwawezesha wananchi waishio vijijini kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo; kuwajengea wananchi uwezo wa kuyafikia
masoko na kupanua wigo wa huduma za kifedha vijijini.
44. Mheshimiwa Spika, chini
ya Programu hiyo katika mwaka 2015/2016, Serikali imekarabati barabara
za vijijini zenye urefu wa kilomita 180 kwa kiwango cha changarawe
zikiwemo kilomita 63.6 za Zanzibar. Aidha, imejenga maghala matano yenye
uwezo wa kuhifadhi Tani 1,000 za mazao kila moja na kuvijengea uwezo wa
kufikia masoko vikundi 780, vikiwemo vikundi 101 vya Tanzania Zanzibar.
Vilevile, imezijengea uwezo Asasi ndogo za Kifedha, zikiwemo SACCOs 291
na Benki tisa za Wananchi ili ziweze kutoa huduma endelevu za kifedha.
Katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea na uboreshaji wa miundombinu
ya masoko katika Halmashauri 38 za Tanzania Bara na Wilaya 10 za
Zanzibar. Aidha, itaendelea kuwajengea wazalishaji wadogo uwezo wa
kuhifadhi na kusindika mazao, mbinu za kufikia masoko na Mfumo wa
Stakabadhi za Ghala.
Mifugo
45. Mheshimiwa Spika,
tunayo fursa ya kufanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya mifugo kama
tutawekeza kwenye viwanda vya kusindika nyama ili kuongeza thamani na
kuzalisha bidhaa za aina mbalimbali kutokana na mifugo iliyopo nchini. Hali
ilivyo sasa siyo nzuri kwani tunauza mifugo mingi nje ya nchi
ikilinganishwa na nyama. Mathalan, katika mwaka 2015/2016 hadi kufikia
mwezi Machi 2016, ng’ombe milioni 1.5, mbuzi milioni 1.2 na kondoo
253,243 wenye thamani ya Shilingi Bilioni
976.5 waliuzwa nje ya nchi. Hii ina maana kuwa mazao kama ngozi, kwato
na damu za wanyama hao, ambazo zingeweza kutumika kuzalisha bidhaa
nyingine za viwandani, yamekwenda nje badala ya kutumika hapa nchini. Tunaweza kabisa kugeuza hali hii haraka kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani mifugo. Nashauri wawekezaji binafsi kwenye sekta ya mifugo kuchangamkia fursa ya kufufua viwanda vya nyama vilivyopo na kujenga vingine vipya ili kuongeza thamani ya mazao ya mifugo.
Mheshimiwa Spika, ni
lazima tuanze kubadili fikra za wafugaji wetu ili ufugaji uwe na tija
kwa kuwa na idadi ndogo ya mifugo yenye ubora wa kisasa na inayoendana
na uwezo wa eneo la malisho. Serikali itaweka msisitizo wa kipekee katika kuboresha
kosaafu za mifugo ili kuzalisha mifugo yenye tija kwa kusambaza ng’ombe
bora kwa ajili ya uzalishaji wa maziwa na nyama kutoka katika mashamba
ya kuzalisha mifugo na kuimarisha uwekezaji katika viwanda vya kuchakata
mazao ya mifugo. Vilevile, juhudi za kudhibiti magonjwa ya mifugo
yasiyokuwa na mipaka na yenye athari kubwa katika uchumi wa Taifa
zitaongezwa. Serikali itaendelea kufanya tathmini ya uendeshaji wa
ranchi za Taifa zilizobinafsishwa ili kuhakikisha kwamba wale waliopewa
vitalu vya mifugo wanavitumia kwa mujibu wa mikataba ya mauzo au
vinginevyo kuwanyang’anya na kuwapa wengine wenye uwezo.
Viwanda
46. Mheshimiwa Spika, Serikali
imedhamiria kuweka nguvu kubwa katika sekta ya viwanda ili kufikia
lengo la kuwa Nchi ya uchumi wa viwanda. Azma hiyo imesisitizwa sana na
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015. Ili
kufikia uchumi wa viwanda, kuanzia mwaka 2016/2017 jitihada kubwa
itawekwa katika kutenga na kuendeleza maeneo maalum ya viwanda; kuweka
miundombinu muhimu ya nishati, usafirishaji, maji na maghala. Aidha,
tutaweka utaratibu endelevu wa upatikanaji mitaji na teknolojia ikiwemo kuanzisha dirisha maalum katika Benki ya Maendeleo TIB na Benki
ya Maendeleo ya Kilimo. Serikali pia itapitia mifumo ya kodi, tozo na
taratibu mbalimbali kwa lengo la kuzipunguza na kuondoa urasimu ili
kupunguza gharama za uzalishaji wa ndani na kuwezesha bidhaa zetu
kushindana katika soko la ndani na kimataifa. Aidha, Serikali itaifanyia
mapitio ya Sera ya Uwekezaji ya mwaka 1996 na Sheria yake ya mwaka 1997
ili kuendana na wakati.
Masoko
47. Mheshimiwa Spika, upatikanaji
wa masoko ya uhakika unategemea mambo makuu manne. Ubora wa bidhaa au
mazao; uhakika wa kupatikana kwa mazao au bidhaa wakati wote; unafuu
wa bei dhidi ya washindani wengine katika soko; na ufungashaji na
ujenzi wa jina la bidhaa (branding). Hivyo, ni lazima mlolongo wote wa
uzalishaji, uongezaji thamani na usafirishaji uwe mzuri kuwezesha uwepo
wa soko la uhakika. Mtiririko huo katika mnyororo wa thamani wa bidhaa
zenye uhakika wa soko ndio msisitizo wa Serikali ya Awamu ya Tano na
msingi wa kuhamasisha mapinduzi ya viwanda kwa lengo la kuongeza thamani
bidhaa zetu kabla ya kuuzwa. Msukumo
mkubwa utawekwa katika uendelezaji na upatikanaji wa soko la ndani na
nje kwa bidhaa zinazozalishwa nchini, hususan katika masoko ya upendeleo
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na masoko mengine ya kimkakati ya
Kikanda na Kimataifa. Vivyo hivyo, uondoaji wa vikwazo vya kibiashara
pamoja na kusimamia viwango na ubora wa bidhaa za ndani na nje ya nchi
utaendelezwa.
48. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha mwaka 2015/2016, Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki
ikiwemo Tanzania zimekamilisha mkataba mwingine wa kutumia Soko la
Marekani bila ushuru chini ya Mpango wa AGOA, kwa kipindi kingine cha miaka
10 kuanzia tarehe 30 Septemba, 2015 hadi 30 Septemba, 2025. Ni muhimu
sana kutumia fursa hii mpya ya AGOA kufanya biashara na Marekani katika
kipindi cha miaka 10 ijayo. Vyama vya wafanyabiashara ni lazima
viwaandae wanachama wao kupata taarifa kamili kuhusu bidhaa
zinazohitajika na ubora unaotakiwa. Aidha, Serikali itasimamia uzalishaji wa bidhaa bora kulingana na ubora unaotakiwa na masoko.
Madini
49. Mheshimiwa Spika, Serikali
inatambua umuhimu wa uchimbaji madini mdogo kama kichocheo cha kuongeza
ajira na kukuza kipato cha wachimbaji wadogo wa madini na wananchi
wanaozunguka maeneo husika ya madini. Aidha, uchimbaji mdogo wa madini
unachangia kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Kwa kuzingatia umuhimu
huo, Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuwaendeleza wachimbaji
wadogo kwa kuwatengea maeneo, kuwapatia ruzuku na kutoa mafunzo ya
kuwawezesha kutekeleza kazi zao kwa ufanisi na tija. Katika mwaka
2015/2016, Serikali ilitenga Hekta 7,731 kwa ajili ya uchimbaji madini
mdogo katika maeneo ya Nyamongo (Tarime) na Muhintiri (Singida). Aidha,
Serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya TIB imetoa mikopo ya masharti
nafuu yenye thamani ya Shilingi Bilioni 7.2 kwa ajili ya kukuza mitaji
ya wachimbaji wadogo. Pia mafunzo yametolewa kwa wachimbaji wadogo
1,520. Mikoo hiyo pia inaweza kutolewa kupitia benki ya TIB Corporate.
50. Mheshimiwa Spika,
katika mwaka 2016/2017, Serikali itatenga zaidi maeneo tengefu kwa
ajili ya uchimbaji madini mdogo na kuongeza kiasi cha ruzuku inayotolewa
kwa Wachimbaji Wadogo. Serikali imetenga Shilingi Milioni 900 kwa ajili
ya ruzuku na Benki ya Dunia imeridhia kutoa Dola za Marekani Milioni
Tatu kuchangia kwenye ruzuku hiyo. Aidha, Serikali itaimarisha usimamizi
katika biashara ya madini ya Tanzanite na kutoa mwongozo mpya wa namna
ya kuendesha uchimbaji madini mdogo kwa tija. Mafunzo
kuhusu namna ya kufanya utafiti wa awali wa madini na uchenjuaji bora
wa madini yataendelezwa ili kazi za wachimbaji madini wadogo zifanyike
kwa ufanisi na tija.
Utalii
51. Mheshimiwa Spika, Sekta
ya Utalii ni moja ya sekta muhimu ambazo fursa zilizopo zikitumika
vizuri zitasaidia sana kukuza ajira na kupunguza umaskini. Juhudi
kubwa ambazo zimefanywa na Serikali katika kuboresha huduma na
miundombinu ya kitalii pamoja na kutangaza vivutio vya utalii
zimeiwezesha Sekta ya Utalii kuchangia asilimia 17 ya Pato la Taifa na zaidi ya asilimia 25 ya mapato yanayotokana na mauzo ya nje mwaka 2015. Aidha,
mwezi Julai 2015 Serikali ilizindua Kampeni Maalum ya Kukuza Utalii wa
Ndani ili kuhamasisha wananchi kutembelea vivutio vilivyopo katika
Hifadhi zetu. Kampeni hiyo imeongeza idadi ya watalii wa ndani kutoka
watalii 115,913 mwezi Septemba 2014 hadi 148,406 Septemba 2015.
Mafanikio hayo yanadhihirisha kwamba Sekta ya Utalii ikiboreshwa ina fursa nyingi za kuchangia Pato la Taifa na kuongeza ajira na kipato cha wananchi. Hata hivyo, unahitajika
uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya utalii ikiwemo hoteli,
usafirishaji na rasilimali watu imara na yenye weledi katika kuwahudumia
watalii wa ndani na nje.
52. Mheshimiwa Spika, tunahitaji
kufanya vizuri zaidi kwa kupanua vyanzo vya utalii na kuhakikisha fedha
nyingi wanazotumia watalii kuja Tanzania zinalipwa hapa nchini badala
ya utaratibu wa sasa wa malipo hayo kufanyika Nchi wanazotoka watalii.
Tunahitaji pia kupanua na kuvutia utalii wa kihistoria na malikale kama
vile miji mikongwe ya Kilwa, Mikindani, Bagamoyo na Mjimkongwe Zanzibar
na vivutio vingine visivyo na mfano Barani Afrika; kuliko kuegemea tu utalii wa wanyamapori na maliasili nyingine. Katika
mwaka 2016/2017, Serikali itaandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza
Utalii Nchini pamoja na kuendelea kutangaza vivutio maafufu kama Mlima
Kilimanjaro, Mbuga za Serengeti na Mapango ya Olduvai.
Kudhibiti Ujangili
53. Mheshimiwa Spika, Nchi
yetu inakabiliwa na tatizo la ujangili hasa wa tembo, faru na biashara
haramu ya nyara za Serikali. Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali
ilizindua Mkakati wa Kupambana na Ujangili na Biashara haramu ya Nyara
za Serikali ulioanza kutekelezwa mwaka 2015, kwa kuchukua hatua
mbalimbali. Hatua hizo ni pamoja na kutumia vifaa na teknolojia ya
kisasa kama vile “Geographical Information System - GIS” na “Global Positioning System - GPS”;
kuimarisha mfumo wa mawasiliano ya radio kutoka mfumo wa analogia
kwenda kidigitali; na kuanza kutekeleza Mpango wa Kikanda wa kukusanya
taarifa za kiintelijensia zinazoongoza doria katika kukamata watuhumiwa
na wahalifu.
54. Mheshimiwa Spika, Serikali
itaimarisha utekelezaji wa Mkakati huo hususan kwa kuzingatia ukubwa wa
changamoto ya vitendo vya uwindaji haramu vinavyofanywa na majangili
kwa kushirikiana na baadhi ya watumishi wa Idara ya Wanyamapori wasio
waaminifu na baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka mapori.
Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha kwamba ujangili huu unakomeshwa
haraka. Nichukue fursa hii kuziomba jamii zinazozunguka hifadhi zetu
kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali katika vita hii.
HUDUMA ZA KIUCHUMI
Ardhi
55. Mheshimiwa Spika, ili
azma yetu ya kufanya mapinduzi ya viwanda ifanikiwe, inahitajika ardhi
iliyopimwa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Changamoto tuliyonayo hivi
sasa ni kwamba sehemu kubwa ya ardhi yetu haijapimwa na kupatiwa
hatimiliki. Hivyo, tumeanza kuchukua hatua za haraka zitakazowezesha
kupatikana kwa ardhi ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa viwanda. Wakuu wa
Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa walishaagizwa
kutenga maeneo ya viwanda na biashara katika Mipango Miji. Napenda
kutumia fursa hii kuitaka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kutopitisha maombi yoyote ya Mipango Miji yasiyokuwa na maeneo ya
Viwanda na Biashara. Nimefarijika kuona kwamba chini ya Mpango wa Maeneo
Huru ya Biashara, baadhi ya mikoa imeshatenga ardhi ambayo itaweza
kuanza kutumika mara moja kutekeleza Mpango huo kwa kuwekewa miundombinu
muhimu na kukamilisha upimaji. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji zishirikiane kufanya
uhakiki wa haraka wa maeneo hayo ili wawekezaji watakaoonesha nia ya
kuwekeza kwenye viwanda wapatiwe maeneo yenye hatimiliki kwa haraka.
56. Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kwamba kuna migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo nchini. Migogoro
hiyo, wakati mwingine imesababisha uharibifu wa mali, majeruhi na
mauaji ya binadamu na mifugo. Njia muafaka ya kudhibiti migogoro hiyo ni
kupima kila kipande cha ardhi, kukimilikisha kwa mtumiaji kwa kumpatia
hatimiliki na kusimamia matumizi yake. Kwa kutambua hilo, mwezi Februari
2016, Serikali ilizindua Programu ya Kuwezesha Umilikishaji Ardhi (Land
Tenure Support Programme) ambayo imeanza kutekelezwa kwa majaribio
katika Wilaya za Ulanga, Kilombero na Malinyi mkoani Morogoro. Programu
hiyo imelenga kuongeza kasi ya kupima ardhi na kutoa hakimiliki za
kimila ambazo zinaweza kutumika kama dhamana kwa wakulima na wafugaji
kupata mikopo; kupunguza au kuondoa migogoro ya ardhi baina ya watumiaji
mbalimbali wa ardhi; na kuhifadhi kumbukumbu za ardhi kwa matumizi
sahihi ya rasilimali hiyo. Programu
hiyo itatekelezwa kwa muda wa miaka mitatu kwa gharama Dola za Marekani
Milioni 15.2. Baada ya majaribio hayo, na mafanikio kuonekana katika
wilaya hizo, Programu itatekelezwa katika wilaya zote nchini.
Ninawaagiza viongozi wa Mkoa wa Morogoro na wilaya zinazohusika,
kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Programu hiyo kwani matokeo yake ni
ya muhimu sana kwenye mustakabali wa upimaji na matumizi endelevu ya
ardhi yetu.
57. Mheshimiwa Spika, mwaka
2015, Serikali iliwaomba Waheshimiwa Wabunge kuainisha na kuwasilisha
Serikalini migogoro ya ardhi iliyopo kwenye majimbo yao. Napenda kutumia
fursa hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge walioitikia wito huo.
Mchango wao katika kipindi cha Julai 2015 hadi Machi 2016, umewezesha
jumla ya migogoro 1,130 ya ardhi kupokelewa Serikalini kutoka katika
Halmashauri zote nchini. Uchambuzi wa migogoro hiyo unaendelea ambapo
taarifa za awali zinaonesha kwamba migogoro mingi iliyopo ni kati ya
wakulima na wafugaji, uvamizi wa mashamba na viwanja, migogoro kati ya
Mamlaka za Hifadhi za Taifa na wananchi na kati ya wawekezaji na
wananchi.
58. Mheshimiwa Spika,
kutokana na hali hiyo, tayari Serikali imechukua hatua kali dhidi ya
maafisa ardhi waliokiuka sheria na taratibu za usimamizi wa ardhi
nchini. Hii ni pamoja na kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Kwa
mfano, hatua kali zimechukuliwa katika Halmashauri za Majiji ya Mwanza
na Arusha, Manispaa za Bukoba na Kahama na kutengua madaraka kwa afisa
ardhi mteule wa Manispaa ya Temeke. Ninaendelea
kuwaomba Waheshimiwa Wabunge kushirikiana na Halmashauri zao hususan
Maafisa Ardhi na kutumia Dawati Maalum la Kuratibu Migogoro ya Ardhi
lililoanzishwa katika kila Halmashauri nchini ili kuendelea kubaini
migogoro iliyopo na kuitafutia ufumbuzi.
59. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali itaifanyia mapitio Sera ya Taifa ya Ardhi ya
mwaka 1995 ili kuweka vipengele muhimu vya kudhibiti migogoro baina ya
watumiaji wa ardhi na kuunda na kuzipa nguvu zaidi Ofisi
za Ardhi za Kanda zitakazosaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kupima na
kupanga matumizi ya ardhi na kutoa hati karibu zaidi na wananchi. Aidha, Serikali itapitia upya Sheria
ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Ardhi ya Vijiji Namba 5 ya
mwaka 1999 ili kuzifanyia marekebisho muhimu kuendana na wakati.
Barabara
60. Mheshimiwa Spika, miundombinu
imara ni msingi muhimu wa maendeleo ya sekta nyingine zote, ikiwemo
Sekta ya Viwanda na Biashara. Katika miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia
uwekezaji mkubwa katika ujenzi wa barabara nchini. Mathalan katika
mwaka 2015/2016, Serikali ililenga kujenga kilometa
523 za barabara kuu kwa kiwango cha lami. Hadi kufikia mwezi Machi,
2016, jumla ya kilometa 414.3 za barabara zilikuwa zimekamilishwa kwa
kiwango cha lami, sawa na asilimia 79 ya lengo lililowekwa. Aidha, jumla
ya kilometa 82.4 za barabara kuu zilikarabatiwa kwa kiwango cha lami,
ikiwa ni sawa na asilimia 73 ya lengo la kilometa 113. Kwa
upande wa barabara za mikoa, jumla ya kilometa 52.19 zilijengwa kwa
kiwango cha lami, sawa na asilimia 68 ya lengo la kilometa 77 na jumla
ya kilometa 676 za barabara za mikoa zilifanyiwa ukarabati kwa kiwango
cha changarawe, sawa na asilimia 54 ya lengo la kilometa 1,252. Ujenzi
wa madaraja makubwa 11 uliendelea ambapo Daraja la Kigamboni
limekamilika na kufunguliwa rasmi.
Reli
61. Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mradi
wa Uboreshaji wa Miundombinu na Huduma za Reli ya Kati, lengo likiwa ni
kuboresha reli iliyopo kwa kutandika reli mpya na nzito zaidi;
kuimarisha matuta, mifereji na tabaka la kokoto. Aidha, tunaendelea na utekelezaji
wa makubaliano baina ya Serikali yetu na Serikali za Rwanda na Burundi
kuhusu ujenzi wa reli ya Dar es Salaam – Isaka – Keza - Kigali (Km.
1,464); na Keza – Musongati (Km. 197) kwa kiwango cha Standard Gauge. Mkakati
wa ndani ni pamoja na kujenga reli ya Standard Gauge kuanzia Dar es
Salaam –Kigoma yenye matawi mawili ya Kaliua-Mpanda-Karema na …..(Haijamalizika NB Nasubiri HANSARD)
Bandari
62. Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2015/2016, Serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha
ufanisi wa bandari zetu kwa kuanzia na Bandari ya Dar es Salaam ambayo
ni lango kuu la biashara katika Afrika Mashariki na Kati na kufuatiwa na
Bandari za Mtwara na Tanga. Tumeanza kwa kuondoa watumishi wote wasio
waaminifu ambao wanachangia kupoteza mapato ya Serikali yanayohitajika
sana katika kutoa huduma muhimu kwa wananchi wetu. Vilevile, tumefanya
kazi kubwa ya kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa kuhakikisha kwamba malipo yote yanafanyika benki na kuoanisha mifumo ya Mamlaka ya Bandari Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania. Niwahakikishie
wananchi na wafanyabiashara kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma
katika bandari zetu na hususan Bandari ya Dar es Salaam kwa kupunguza
idadi ya siku za kutoa mizigo bandarini li tufikie siku mbili au chini
ya siku hizo. Aidha, tutaziondoa kero zote zilizoainishwa na Mawakala wa
Forodha nilipokutana nao tarehe 21 Machi, 2016 Jijini Dar es Salaam.
Vilevile, Serikali itaziba mianya yote ya upotevu wa mapato bandarini na
wale wote watakaobainika kushiriki kwenye wizi wa aina yoyote
wataondolewa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Mawasiliano
63. Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kukamilisha mradi wa ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano nchini ikiwemo ujenzi wa Kituo Mahiri cha Kutunzia Kumbukumbu katika Jiji la Dar
es Salaam. Aidha, Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya
mawasiliano vijijini ambapo hadi sasa tumefanikisha ujenzi wa kilometa
18,000 kati ya kilometa 20,000 za miundombinu ya mkongo katika wilaya
zote nchini. Kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na ujenzi wa
miundombinu ya mawasiliano katika vijiji 4,000 visivyokuwa na
mawasiliano, kuunganisha Ofisi zote za Wakuu wa Wilaya, Hospitali za
Wilaya, Mahakama, Vituo vya Polisi vya Wilaya, Ofisi za Posta na
kuziwesha shule 431 kupata huduma ya intaneti bila malipo.
Nishati
(a)Umeme
64. Mheshimiwa Spika, Serikali
ya Awamu ya Tano imedhamiria kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika,
unaokidhi mahitaji na wenye gharama nafuu ili kusukuma mapinduzi ya
viwanda kwa kasi zaidi. Ili kutekeleza azma hiyo, katika mwaka
2015/2016, Serikali imeongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme kutoka
Megawati (MW) 1,226.24 mwaka 2015 hadi kufikia MW 1,516.24 mwezi Januari
2016, sawa na ongezeko la Asilimia 24. Ongezeko hilo limetokana na uamuzi sahihi wa Serikali wa kutekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa Bomba la Gesi pamoja na mradi wa kufua umeme wa Kinyerezi-I wenye uwezo wa kuzalisha MW 150. Mradi
huo baadaye utapanuliwa na kuweza kufikia MW 335 ifikapo mwaka
2017/2018. Sambamba na hatua hiyo, tarehe 16 Machi 2016, Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo kingine cha Kinyerezi-II cha
kufua umeme kutokana na gesi asilia ambao utakapokamilika utazalisha MW
240. Lengo la Serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo ni kuongeza
uwezo wa uzalishaji umeme hadi kufikia MW 4,915 na hivyo, kuwezesha
asilimia 60 ya watanzania kupata umeme wa uhakika ifikapo mwaka 2020 na
kutekeleza ipasavyo azma ya kuongeza uwekezaji mkubwa kwenye viwanda.
65. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha mwaka 2015/2016, Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
umeendelea kusambaza na kuunganisha umeme kwa wananchi waishio vijijini.
Katika kipindi hicho,
idadi ya wananchi waliopata umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Pili ni
71,724 katika vijiji 1,669. Aidha, hadi mwezi Januari, 2016 Serikali
imekamilisha ujenzi wa kilometa 12,193 za njia za msongo wa kati na
kilometa 1,830 za msongo mdogo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Awamu
ya Pili ya Usambazaji wa Umeme Vijijini. Vilevile, umeme umefikishwa
kwenye Makao Makuu ya Wilaya mpya 12 za Buhigwe, Busega, Chemba,
Itilima, Kakonko, Kalambo, Kyerwa, Mkalama, Mlele, Nyasa, Nanyumbu na
Uvinza. Utekelezaji wa miradi hiyo umeongeza kiwango cha wananchi
wanaopata huduma ya umeme kufikia asilimia 40.
66. Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2016/2017, Serikali itaendelea kutekeleza Mradi wa Kinyerezi-II pamoja na kuimarisha
na kujenga njia za usafirishaji umeme katika Gridi ya Taifa za Msongo
mkubwa wa kiloVolts 400 kutoka Iringa kupitia Dodoma na Singida hadi
Shinyanga na kutoka Dar-es-Salaam kupitia Chalinze na Tanga hadi Arusha
pamoja na mradi wa kiloVolts 220 kutoka Makambako hadi Songea. Aidha,
Serikali itakamilisha Awamu ya Pili ya mradi wa usambazaji umeme
vijijini na kuanza utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya miradi ya REA.
(b) Gesi Asilia na Mafuta
67. Mheshimiwa Spika, baada
ya ugunduzi mkubwa wa Gesi Asilia nchini, mikakati ya Serikali
inayoendelea ni kubuni miradi mbalimbali hasa ile itakayoendeshwa na
wafanyabiashara wazawa ili rasilimali hiyo iweze kuwanufaisha Watanzania
na kuwawezesha kumiliki uchumi wa Taifa lao. Serikali imetenga eneo la
ardhi huko Likongo Mkoani Lindi kwa ajili ya kujenga miundombinu ya
kuchakata Gesi Asilia ikiwa ni sehemu ya kutekeleza azma hiyo ya
kuwawezesha wazawa. Serikali itaanza utekelezaji wa mradi huo katika
mwaka 2016/2017.
68. Mheshimiwa Spika, katika
kuhakikisha kwamba Nchi inakuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta kwa
ushindani na gharama nafuu, Serikali imeanzisha Wakala wa Uagizaji
Mafuta kwa Pamoja yaani Petroleum Bulk Procurement Agency, ulioanza
kazi rasmi mwezi Januari, 2016. Utaratibu huo utaiwezesha Serikali
kusimamia vizuri udhibiti wa uagizaji wa mafuta nchini na kuwawezesha
Wananchi kuwa na uhakika wa kupata mafuta bora yenye viwango
vinavyokubalika kimataifa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo
na kijamii.
HUDUMA ZA JAMII
Elimu
69. Mheshimiwa Spika, kwa
kutambua umuhimu wa elimu kama nyenzo imara ya maendeleo ya kiuchumi na
kijamii, Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kuchukua hatua madhubuti za
kuboresha na kuimarisha elimu ya awali, msingi, sekondari, ufundi na
elimu ya juu. Hatua zinazochukuliwa zinalenga kuhakikisha kwamba elimu
ya Tanzania ni ya viwango vya ubora wa hali ya juu ili kuwawezesha
vijana wetu kukabiliana na changamoto za maisha kwa kujiari wenyewe na
kumudu ushindani katika soko la ajira la ndani, kikanda na kimataifa.
Aidha, hatua hizo zitatuwezesha kuwa na rasilimali watu yenye weledi wa
kutosha kujenga uchumi wa viwanda nchini. Moja ya hatua kubwa
iliyochukuliwa na Serikali ni utekelezaji wa ahadi ya utoaji wa elimu
bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne kwa shule za umma
kuanzia mwezi Januari 2016. Ahadi hiyo ilitolewa na mgombea Urais
kupitia CCM wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwezi Oktoba,
2015 ambaye kwa sasa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Vilevile, ni matakwa ya Kifungu cha 52(a) cha Ilani ya Uchaguzi wa CCM
ya mwaka 2015 ambacho kinasisitiza kwamba Serikali itaandaa mfumo,
muundo na taratibu nyumbufu za kutoa elimu ya awali na elimumsingi bila
malipo ili kila Mtanzania apate fursa sawa ya kupata elimu.
70. Mheshimiwa Spika, naamini
kabisa kuwa hatua hiyo nzuri iliyochukuliwa na Serikali ya Awamu ya
Tano, itawapunguzia wazazi na walezi hasa wananchi maskini mzigo wa
kugharamia elimu ya vijana wao. Kupitia Waraka wa Elimu Na. 5 wa mwaka
2015, Serikali imefuta michango ya maji, umeme, ulinzi, mitihani na ada iliyokuwa inachangishwa shuleni kwa idhini ya Kamati na Bodi za Shule. Hata
hivyo, yapo majukumu yanayohusu mahitaji ya msingi ya mtoto ambayo
yataendelea kutekelezwa na wazazi na walezi kama ilivyokuwa inafanyika
awali. Majukumu hayo ni pamoja
na kumnunulia mtoto sare za shule na michezo, madaftari, kalamu na
chakula kwa wanafunzi wa shule za kutwa kwa utaratibu utakaowekwa na
wazazi na walezi wenyewe. Maeneo mengine ni kulipia nauli ya kwenda na
kurudi shule mwanafunzi na mahitaji mengine kama vile kununua godoro,
shuka na vifaa vya usafi binafsi. Vilevile, mzazi au mlezi ana wajibu wa
kugharamia matibabu ya mtoto wake.
71. Mheshimiwa Spika, baada
ya kuanza utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo, kumejitokeza
changamoto kadhaa. Baadhi ya changamoto hizo ni uelewa wa jamii juu ya
umuhimu wa kuweka utaratibu muafaka wa kutoa chakula cha mchana kwa
wanafunzi wa kutwa na uendeshaji wa mabweni ambayo wazazi na walezi au
jamii walikuwa wanachangia fedha za chakula. Changamoto nyingine ni
pamoja na upungufu wa miundombinu kama madarasa, mabweni, maabara,
nyumba za walimu na vyoo. Napenda kuwahakikishia wananchi kwamba
Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo na jitihada kubwa
zimewekwa katika kuielimisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu mpango
mzima wa utoaji elimu bila malipo.
72. Mheshimiwa Spika, tunayo
changamoto ya upungufu mkubwa wa madawati baada ya kuanza kuandikisha
watoto shule bila malipo. Hili ni jambo kubwa na tulishatoa agizo kwa
Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuhakikisha kuwa kila
Halmashauri inatumia rasilimali zake kutengeneza madawati kwa kila
shule. Nitumie nafasi hii kuwashukuru wadau walioanza kuchangia madawati
katika maeneo mbalimbali na ninawasihi wengine waendelee kuunga mkono
jitihada hizi za Serikali. Kuanzia leo hii, nawaagiza Wakuu wa Wilaya na
Wakurugenzi waliokamata mbao ndani ya Halmashauri zao kuzitumia
kutengenezea madawati na siyo kuzipiga mnada. Natumia nafasi hii
kukushukuru wewe Mheshimiwa Spika na Watendaji wa Bunge kwa Mkakati wa
kubana matumizi uliowezesha kupata Shilingi Bilioni sita zitakazotumika
kutengeneza madawati. SUMA JKT na Magereza wameanza kazi ya kutengeneza
madawati hayo. Tunatarajia kupata madawati 80,000 ambayo tutawagawia
Wabunge wa Majimbo yote na kwa wastani kila Jimbo litaweza kupata
madawati 300.
73. Mheshimiwa Spika, napenda
nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane
katika juhudi za kuunga mkono uamuzi wa Serikali kuhusu elimu bila
malipo. Aidha, nawaomba wote
kwa ujumla wetu kushirikiana katika kuwaelimisha wananchi kuhusu mpango
huu na wajibu wa kila mmoja wetu katika kuhakikisha kwamba watoto wetu
wanapata fursa za kupata elimu bora. Tukifanya hivyo, tutaweza kufikia
lengo letu la kuwa Nchi yenye uchumi wa kipato cha kati kwa haraka
zaidi.
74. Mheshimiwa Spika, elimu
ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ni nguzo muhimu ya kuwapatia ujuzi
na kuwajengea uwezo na uzoefu wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi na
sekondari. Uzoefu wa Nchi za Asia zilizowekeza katika elimu ya ufundi na
ufundi stadi unaonesha kwamba maendeleo ya haraka waliyoyapata na
hususan kufikia uchumi wa kati na wa viwanda umechangiwa sana na elimu
ya ufundi. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali itaelekeza nguvu zake
katika kujenga na kuimarisha miundombinu ya elimu ya ufundi na kuboresha
mitaala ili iendane na mahitaji ya sasa ya uchumi wa viwanda. Kwa
kuanzia, Serikali imeridhia vyuo vya maendeleo ya wananchi kuhamishiwa
Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi na kufanyiwa ukarabati
kwa ushirikiano na Sekta Binafsi ili viweze kutoa mafunzo ya ufundi.
Hatua hiyo itaharakisha kufikiwa kwa lengo la Serikali la kuwa na chuo
cha ufundi kwa kila Wilaya.
75. Mheshimiwa Spika, udahili katika vyuo vya elimu ya juu umeongezeka kutoka wanafunzi 214,722 mwaka 2014 hadi kufikia wanafunzi 220,531 mwaka 2015. Aidha, hadi kufikia Februari 2016, idadi ya wanafunzi waliopewa mikopo ya elimu ya juu ilifikia 122,886. Kiasi
cha fedha za mikopo kilichotolewa kwa wanafunzi hao ni Shilingi Bilioni
207. Hata hivyo, hali ya urejeshaji wa mikopo iliyotolewa hairidhishi.
Hivyo, naiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kufuatilia urejeshaji wa
mikopo hiyo ili fedha hizo zitumike kuwakopesha wanafunzi wengine.
Afya
76. Mheshimiwa Spika,
uimarishaji wa huduma za afya nchini, kwa maana ya kinga na tiba ni
muhimu sana. Nguvukazi yenye afya njema hutoa mchango mkubwa kwenye
uchumi ikilinganishwa na nguvukazi dhaifu kiafya. Kwa kuzingatia umuhimu
huo, Serikali imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma za kinga,
uchunguzi na upatikanaji wa dawa na vifaa-tiba katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali Maalum,
Hospitali za Rufaa za Mikoa, Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na
Zahanati. Aidha, Serikali imetoa maelekezo kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD)
kufungua na kuendesha maduka ya dawa katika Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, Hospitali za Rufaa za Kanda, Hospitali za Rufaa za Mikoa na
Hospitali za Wilaya ili kuhakikisha kwamba dawa za kutosha zinapatikana
wakati wote na kwa bei nafuu.
77. Mheshimiwa Spika, napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Bohari Kuu ya Dawa imefungua na
inaendesha maduka ya dawa yanayouza bidhaa zake kwa bei nafuu ndani ya
maeneo ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Sekou Toure (Mwanza), Mawenzi
(Kilimanjaro) na Mount Meru (Arusha). Pamoja na juhudi hizo za Serikali
za kuimarisha huduma za afya nchini, milango ipo wazi kwa sekta binafsi
ya ndani na nje ya nchi kuwekeza katika sekta ya afya.
78. Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na huduma za Bima ya Afya ili
kuongeza na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya afya kwa watu wote.
Idadi ya wanufaika wa Bima ya Afya tangu kuanzishwa kwake ni 11,729,281,
sawa na asilimia 27 ya watanzania wote kulingana na Sensa ya mwaka
2012. Kati ya hao, wanufaika 8,390,550 wako katika Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF) na 3,338,755 ni wanachama wa Mfuko wa Afya ya Jamii
(CHF). Hata hivyo, idadi ya
wanufaika wa Bima bado ni ndogo, hivyo naagiza viongozi wa Mifuko hiyo
kushirikiana pamoja kutoa elimu na kuhamasisha wananchi wengi zaidi
kujiunga na Mifuko hiyo. Serikali inaendelea kuangalia uwezekano wa
Hospitali za Rufaa za Mikoa kuwa chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ili Katibu Tawala wa Mkoa aratibu
maendeleo ya Hospitali za Wilaya, Vituo vya Afya na Zahanati.
Maji
79. Mheshimiwa Spika, Serikali
inaendelea kutekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa lengo
la kuwapatia wananchi huduma ya maji safi, salama na ya kutosha. Hadi
kufikia Desemba 2015, Serikali imefikisha huduma ya maji safi na salama
kwa asilimia 72 katika maeneo ya vijijini, asilimia 86 miji mikuu ya
mikoa na asilimia 60 katika miji mikuu ya wilaya na miji midogo.
Mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa miradi ya maji 1,143 kati ya
miradi 1,855 ya maji mijini na vijijini ambayo imetekelezwa chini ya
Awamu ya Kwanza ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Aidha, huduma
ya maji katika Jiji la Dar es Salaam na miji ya Bagamoyo na Kibaha
imeongezeka na kufikia asilimia 68, lengo likiwa kufikia asilimia 95
ifikapo mwaka 2025. Katika mwaka 2016/2017, Serikali itatekeleza Awamu
ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji pamoja na kukamilisha
miradi 712 ambayo haikutekelezwa katika Awamu ya Kwanza. Natoa wito kwa
wananchi wote kutunza vyanzo vya maji pamoja na miundombinu yake ili
kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji vijijini na mijini.
80. Mheshimiwa Spika, sote
tunafahamu kwamba maji ni moja ya vigezo muhimu katika kuanzisha na
kuendeleza viwanda. Hivyo hatua zinazochukuliwa na Serikali katika
kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji nchini, pamoja na kuongeza
huduma ya maji safi na taka, ina lengo la kuongeza mchango wa Sekta ya
Maji katika Sekta ya Viwanda. Mathalan, ongezeko la maji kutokana na
utekelezaji wa miradi ya kuboresha miundombinu ya maji ya Ruvu
Juu na Ruvu Chini umesaidia kupunguza tatizo la maji katika Jiji la Dar
es Salaam. Serikali itahakikisha kuwa maeneo yenye viwanda na
yanayotegemewa kuwa na viwanda yanaunganishwa na miradi mikubwa ya maji
ili kuongeza kasi ya uzalishaji.
SHERIA, ULINZI NA USALAMA
Sheria
81. Mheshimiwa Spika,
ni dhamira ya Serikali kuona kwamba kero ya mlundikano wa mashauri
Mahakamani inakuwa historia na kwamba wananchi wanapata haki kwa wakati.
Katika kufanikisha dhamira hiyo, Serikali imeimarisha utendaji wa
Mhimili wa Mahakama kwa kuongeza rasilimali watu na fedha. Aidha,
Serikali imeboresha na kuongeza ufanisi katika upelelezi na uendeshaji
wa mashauri kwa kutenganisha jukumu la upelelezi na uendeshaji wa
mashauri. Vilevile, uongozi wa Mahakama umejiwekea utaratibu wa Majaji
na Mahakimu kuwa na malengo ya idadi ya mashauri ambayo wanapaswa
kuyasikiliza kila mwaka.
82. Mheshimiwa Spika, katika
juhudi za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa majengo ya Mahakama na
vitendea kazi katika ngazi zote, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ametekeleza ahadi yake
aliyoitoa tarehe 4 Februari 2016 ya kutoa fedha zote za maendeleo za
Mahakama kiasi cha Shilingi Bilioni 12.3 kwa mwaka 2015/2016. Hatua
hiyo imeiwezesha Mahakama kuendelea na ukarabati na ujenzi wa Mahakama
katika ngazi mbalimbali na pia ununuzi wa vitendea kazi. Tunamshukuru
sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi huo.
83. Mheshimiwa Spika,
wakati akihutubia Bunge lako Tukufu mwezi Novemba, 2015 Mheshimiwa Rais
aliahidi kuwa katika mwaka 2016/2017, Serikali itaanzisha Mahakama
Maalum ya Ufisadi. Napenda kuliarifu Bunge lako kwamba, Serikali
imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama
Kuu itakayoanza kufanya kazi mwezi Julai 2016. Aidha, Serikali
itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu
wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki.
Ulinzi na Usalama
84. Mheshimiwa Spika, vyombo
vya ulinzi na usalama vimeendelea na jukumu la kulinda mipaka, raia na
mali zao. Kwa jumla, hali ya ulinzi na usalama wa Nchi yetu ipo shwari.
Napenda kutumia fursa hii kuvipongeza vyombo vyote vya ulinzi na usalama
kwa kazi yao nzuri, weledi na uzalendo wa hali ya juu katika
kuhakikisha Taifa letu lina usalama wa kutosha pia kuchangia usalama wa
mataifa mengine duniani yenye migogoro ya kisiasa. Mambo yote haya
yanatokana na ukweli kwamba Serikali imekuwa ikiviwezesha vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama kuwa na uwezo wa kulinda mipaka ya Nchi, raia na
mali zao. Katika kujenga utayari wa Majeshi wakati wote, askari wetu
wameshiriki kwa ufanisi katika majukumu ya kimataifa ya kulinda amani
katika Nchi zenye migogoro duniani, hususan Darfur, Sudan, Lebanon na
Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
85. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2015/2016, jumla ya vijana 27,463 walipatiwa mafunzo ya kujenga
uzalendo, ukakamavu, maadili mema, utaifa pamoja na stadi za kazi na za
kimaisha. Kati yao, vijana 7,517 ni wa kujitolea na 19,946 ni wa mujibu
wa sheria. Ni jambo la kutia moyo kwamba vijana 5,453 waliopitia mafunzo
ya Jeshi la Kujenga Taifa wamenufaika na utaratibu wa kuajiriwa na
vyombo vya ulinzi na usalama. Kati ya hao, Vijana 3,521 wameajiriwa na
JWTZ; Polisi 1,185; Usalama wa Taifa 106, Takukuru vijana 24 na Jeshi la
Zimamoto vijana 617.
Aidha, Serikali inaendelea
kuboresha mazingira ya kuishi kwa watumishi wa vyombo vya ulinzi na
usalama ambapo ujenzi wa nyumba 4,744 za makazi zimekamilishwa kati ya
nyumba 6,064 za awamu ya kwanza kwenye mradi wa nyumba 10,000
zinazotarajiwa kujengwa Nchi nzima.
86. Mheshimiwa Spika, Serikali
italiimarisha Jeshi letu kwa kulipatia mafunzo, zana bora na za kisasa
zaidi; kuboresha mazingira ya kufanyia kazi; na maslahi. Aidha,
itaimarisha uwezo wa Jeshi katika utafiti na kuendeleza teknolojia kwa
madhumuni ya kuongeza ubunifu katika kuzalisha bidhaa bora zaidi na
huduma kwa ajili ya matumizi ya jeshi na raia nchini na nje ya nchi.
Udhibiti wa Uhalifu Nchini
87. Mheshimiwa Spika, Jeshi
la Polisi limeendelea kulinda usalama wa raia na mali zao na kudumisha
amani na utulivu nchini. Katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2015,
jumla ya makosa makubwa ya jinai 68,814 yaliripotiwa katika Vituo vya
Polisi kote nchini ikilinganishwa na makosa 70,153 yaliyoripotiwa katika kipindi
kama hicho mwaka 2014, sawa na upungufu wa asilimia 1.9. Upungufu huo
wa makosa umetokana na kuongezeka kwa ushirikishwaji wa wananchi katika
vita dhidi ya uhalifu na kuongezeka kwa taarifa za kiintelijensia.
Aidha, Jeshi limeimarisha doria za Nchi kavu na majini pamoja na kufanya
misako na operesheni maalum kwa ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, Tarafa,
Kata na Shehia. Katika mwaka 2016/2017, Jeshi la Polisi litaendelea
kutoa elimu ya Ulinzi Shirikishi kwa wananchi ili waweze kuongeza
ushirikiano na Jeshi la Polisi katika utekelezaji wa jukumu la kupambana
na uhalifu.
MICHEZO
88. Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa michezo katika kuimarisha afya, kuongeza ajira, kujenga udugu na mshikamano miongoni mwa jamii na mataifa mbalimbali duniani, Serikali
itaendelea kuimarisha michezo nchini ili wanamichezo wetu waweze
kufanya vizuri katika medani za michezo ndani na kimataifa. Katika kufikia azma hiyo, mwaka 2016/2017, Serikali itakamilisha
mapitio ya Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 na kuendelea
kutoa mafunzo ya michezo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari ili
kuibua vipaji. Serikali pia itaendelea kusimamia maendeleo ya michezo
katika shule, vyuo, taasisi na vilabu. Lengo ni kuhakikisha kuwa michezo
inatoa fursa kwa vijana kupata ajira na kuendeleza vipaji vyao.
HABARI
89. Mheshimiwa Spika, Serikali
inatambua kwamba Sekta ya Habari ni nguzo muhimu katika kuelimisha,
kuhabarisha na kuburudisha umma. Kutokana na umuhimu huo, Serikali
imeendelea kusimamia
Sekta ya Habari kikamilifu na kuhakikisha vyombo vya habari
vinatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili na
Weledi. Uhuru wa vyombo vya habari ni mkubwa na wigo wa ushiriki
wa Sekta Binafsi umeongezeka sana. Hadi kufikia mwezi Machi, 2016
Serikali ilikuwa imesajili Vituo vya Televisheni 26, Vituo vya Redio 126
na Magazeti 833. Muhimu hapa ni matumizi mazuri ya kalamu na kuweka
uzalendo wa Nchi mbele.
90. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2016/2017, Serikali itawasilisha Bungeni Muswada wa Sheria ya
Huduma za Habari kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa vyombo vya
Habari. Aidha, itaboresha Idara ya Habari- Maelezo ili itimize jukumu
lake kama Msemaji Mkuu na Mratibu wa Mawasiliano Serikalini. Vilevile,
itaendelea kufuatilia
kwa karibu maudhui ya vituo vyote vya utangazaji kupitia mtambo maalum
wa ufuatiliaji wa maudhui na kuhakikisha vituo vya utangazaji vinakuwa
na wakalimani wa lugha ya alama. Napenda nitumie fursa hii kuvitaka
vyombo ya habari nchini, kufanya kazi zake kwa weledi na kwa mujibu wa
Sheria na Taratibu zilizopo, mambo ambayo ni muhimu sana katika tasnia
ya habari kama wafanyavyo wenzao katika Nchi zote duniani yaani
uzingatiaji wa maadili katika tasnia ya habari. Aidha, niwaombe wamiliki
wa vyombo vya habari na wanahabari kutanguliza uzalendo wa Nchi yao
mbele.
MASUALA MTAMBUKA
Lishe
91. Mheshimiwa Spika, lishe
bora ni nguzo muhimu katika kujenga Taifa lenye rasilimali watu wenye
afya bora na uwezo mkubwa wa kufikiri na kufanya kazi. Ukosefu wa lishe
bora husababisha utapiamlo ambao una madhara makubwa kiuchumi na kijamii
kwa kaya, jamii na Taifa kwa ujumla. Hali hiyo ikitokea ndani ya
kipindi cha siku 1,000 kuanzia ujauzito hadi miaka miwili ya ukuaji wa
mtoto husababisha udumavu ambao madhara yake hayawezi kurekebishwa
katika maisha yake yote. Udumavu unaathiri mwili na akili ya mtoto na
hivyo hawezi kujifunza vizuri darasani na pia hupunguza uwezo wake
katika kuchangia maendeleo ya Taifa lake hapo baadaye.
92. Mheshimiwa Spika, athari
nyingine za utapiamlo ni pamoja na watoto kuugua mara kwa mara, hali
inayochangia ongezeko la gharama za matibabu kwa familia, jamii na
Taifa; na wazazi kutumia muda mwingi kuuguza watoto badala ya kufanya
shughuli za kukuza uchumi. Hali hiyo inatutaka sote tuwe mabalozi wa
kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa lishe bora. Vilevile, ni muhimu kwa
wajawazito kuhudhuria kliniki ili kuchunguzwa afya zao na pia kupata
ushauri wa kitaalam utakaowawezesha kupata
watoto wenye afya njema. Wakina mama waelimishwe kunyonyesha watoto wao
kwa kipindi kisichopungua miezi sita mfululizo na kuwapatia vyakula
vyenye viini lishe vya kutosha baada ya hapo. Masuala haya yanahitaji
elimu zaidi kwa sababu vyakula hivyo vinapatikana kwenye jamii na kaya
zetu na siyo ghali kuvipata.
Vita Dhidi ya Rushwa
93. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kupambana na rushwa kwa kuchunguza tuhuma za rushwa na
kuwafikisha watuhumiwa mbele ya vyombo vya sheria. Katika mwaka
2015/2016, Serikali imeshughulikia tuhuma 3,911 ambapo uchunguzi wa
tuhuma 324 ulikamilika. Kati ya tuhuma hizo, majalada 252 yaliombewa
kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo majalada 156 yalipata kibali
cha kuwafikisha watuhumiwa Mahakamani. Aidha, Majalada 329 yaliyotokana
na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
yalichunguzwa. Majalada 19 yalikamilika na kuombewa kibali kwa
Mkurugenzi wa Mashtaka ambapo majalada 12 yalipata kibali cha
kuwafikisha watuhumiwa mahakamani. Vilevile, majalada nane yaliyohusu
tuhuma za rushwa kubwa yalifikishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Kati ya
hayo, majalada mawili yamepata kibali na watuhumiwa wamefikishwa
Mahakamani.
94. Mheshimiwa Spika, Miradi
ya Maendeleo 284 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 41.63 ilikaguliwa
kupitia ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo katika Serikali za Mitaa.
Miradi 69 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 8.32 ilibainika kuwa na
kasoro ambapo miradi 10 wahusika walishauriwa namna ya kurekebisha
kasoro zilizojitokeza wakati miradi 59 uchunguzi wa kina umeanzishwa ili
wahusika wachukuliwe hatua. Aidha, ufuatiliaji maalum wa miradi ya afya
inayofadhiliwa na Benki ya Dunia unaendelea kufanyika ambapo hatua
mbalimbali zimechukuliwa kwenye maeneo yaliyobainika kuwa na kasoro,
ikiwemo kuanzisha uchunguzi wa awali ambapo majalada 85 yamefunguliwa.
95. Mheshimiwa Spika, Serikali
itaendelea kuchunguza tuhuma 3,444 zilizopo na mpya zitakazojitokeza na
kukamilisha uchunguzi wa tuhuma 10 za rushwa kubwa. Aidha, itawajengea
uelewa wa masuala ya rushwa makundi mbalimbali katika jamii na hususan
Asasi za Kiraia, madhehebu ya dini na wanahabari ili washiriki
kikamilifu kuwaelimisha wananchi kuhusu kudhibiti rushwa na kuendelea
kufungua na kuimarisha klabu za wapinga rushwa katika shule za msingi,
sekondari na vyuo ili kuendelea kujenga jamii inayochukia rushwa.
Kudhibiti UKIMWI
96. Mheshimiwa Spika, maambukizo mapya ya Virusi vya UKIMWI yanaendelea kupungua kutoka asilimia
5.7 mwaka 2008 hadi 5.1 kwa takwimu za 2011/2012. Vifo vitokanavyo na
UKIMWI navyo vimeendelea kupungua kutoka wastani wa vifo 79,338 mwaka
2012/2013 hadi vifo 50,219 mwaka 2014/2015. Maambukizi mapya ya UKIMWI
nayo yamepungua kutoka wastani wa 78,843 mwaka 2012/2013 hadi 69,000
mwaka 2014/2015. Idadi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI
inakadiriwa kuwa milioni 1.4 kwa mwaka 2012/2013 na watu milioni 1.5
mwaka 2014/2015.
97. Mheshimiwa Spika, pamoja na kupungua kwa kasi ya maambukizi, UKIMWI bado ni tishio linaloathiri maendeleo na maisha ya wananchi. Hatuna
budi kuendelea kuchukua hatua za dhati na madhubuti za kudhibiti
maambukizi mapya, kutoa huduma za afya na matibabu kwa wale
walioambukizwa na kuwahudumia wale wenye mahitaji kutokana na vifo vya
wazazi hususan watoto yatima. Hatua hizo ni pamoja na kutekeleza
Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI wa mwaka 2013/2014 hadi
2017/2018 unaolenga kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 50,
kupunguza vifo vitokanavyo na UKIMWI na kuondoa unyanyapaa na ubaguzi
dhidi ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI ifikapo 2018.
98. Mheshimiwa Spika, huduma za upimaji wa virusi vya UKIMWI na uingizwaji kwenye mpango wa matunzo na matibabu kwa wale wanaogundulika na maambukizi
ya VVU zinaendelea kutolewa. Jumla ya watu wanaoishi na virusi vya
UKIMWI wanaopata dawa za ARV ni 640,084, sawa na asilimia 43 ya watu
wote wenye maambukizi. Kati yao, asilimia 69 ni wanawake na watoto.
Serikali imeanza utaratibu mpya wa kutoa dawa za kufubaza virusi vya
UKIMWI kwa yeyote atakayepimwa na kukutwa na maambukizi ya virusi vya
UKIMWI tofauti na utaratibu wa awali ambao mwathirika alianzishiwa dawa
kutegemea idadi ya CD4. Utaratibu huo umeanza katika Halmashauri 48
zenye kiwango kikubwa cha maambukizi na hatimaye kueneza huduma hii Nchi
nzima. Katika juhudi za kupunguza maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama
kwenda kwa mtoto, Serikali imeendelea kutoa huduma katika vituo 5,361 kati ya 5,863 vinavyotoa huduma ya Afya ya Uzazi na Mtoto nchini. Vilevile, Serikali
imeendelea kutoa elimu kwa umma katika masuala ya VVU, UKIMWI, Afya ya
Uzazi na Ujinsia. Kuanzia mwezi Julai 2016, Serikali itaanza zoezi la
kupima kiwango cha maambukizi kwa Nchi nzima, kila Mkoa, ikiwa ni mara
ya nne zoezi hili kufanyika nchini.
Hifadhi ya Mazingira
99. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka na kutekeleza mipango na mikakati thabiti ya kutunza mazingira kwa lengo la kutunza vyanzo vya maji, Bioanuai, kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa na uharibifu wa misitu. Aidha, Serikali
imeandaa Kanuni mpya ya Mifuko ya Plastiki ya mwaka 2015 inayokataza
kuzalishwa na kuingizwa nchini matumizi ya mifuko ya plastiki yenye
unene chini ya mikroni 50. Vilevile, Serikali imeendelea kufanya kaguzi
katika maeneo mbalimbali ili kubaini iwapo sheria za mazingira
zinazingatiwa na kuchukua hatua za kuvifungia viwanda tisa na kutoa onyo
kwa viwanda 63. Taasisi zinazohusika na usimamizi wa Sheria ya
Mazingira hazina budi kuvisaidia kiufundi viwanda husika ili visifungwe kwa muda mrefu kwani ni hasara kwa Taifa.
100. Mheshimiwa Spika, wakati
wa maadhimisho ya 54 ya Uhuru, tarehe 9 Desemba, 2015 Mheshimiwa Rais
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alifanya uamuzi wa busara wa kuwataka
wananchi wote kuyatumia maadhimisho hayo kwa kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao yanayowazunguka na maeneo ya Taasisi za Umma. Napenda
kutumia fursa hii kuwapongeza kwa dhati wananchi wote, Taasisi za Umma
na Sekta Binafsi na Asasi za kiraia kwa mwitikio mkubwa waliouonesha
katika kushiriki na kufanikisha zoezi hilo la usafi.
101. Mheshimiwa Spika, kwa
kuzingatia umuhimu wa usafi wa mazingira, Serikali imeamua kwamba zoezi
la usafi wa mazingira litakuwa endelevu. Hivyo, Ofisi ya Makamu wa Rais
kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, tayari zimetoa Waraka
maalum wa kuifanya kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa siku maalum ya
wananchi wote kufanya usafi wa mazingira nchini kote. Napenda kuwahimiza
Viongozi na Watendaji wote wa Wizara, Mashirika na Taasisi za Umma na
Sekta Binafsi, Mikoa, Wilaya
na Halmashauri zote nchini pamoja na Watendaji wa Mitaa, Kata na Vijiji
na Vitongoji na Wakuu wa Kaya kusimamia usafi wa mazingira katika
maeneo yao. Aidha, nawasihi Wananchi wote kudumisha utamaduni na tabia
nzuri ya kuhakikisha kuwa maeneo yao yanakuwa safi wakati wote ili
kuboresha afya zao na kuleta maendeleo endelevu nchini.
Menejimenti ya Maafa
102. Mheshimiwa Spika, Serikali
imeendelea kutekeleza jukumu la kuwalinda na kuwasaidia wananchi dhidi
ya maafa yaletwayo na matukio mbalimbali ya kiasili. Miongoni mwa hatua
zilizochukuliwa ni pamoja na Serikali kutoa Tani 31,184 za chakula kwa
halmashuri 69 zilizokumbwa na tatizo la upungufu wa chakula katika mwaka
2015/2016. Kati ya hizo, Tani 7,727 zilitolewa bure kwa kaya zisizo na
uwezo na Tani 23,457 zilitolewa kwa bei nafuu ya Shilingi 50 kwa Kilo.
103. Mheshimiwa Spika, Serikali pia imetoa misaada mbalimbali ya kibinadamu yenye thamani ya Shilingi Milioni 42.5 na
kiasi cha Shilingi Milioni 143.5 kwa ajili ya ununuzi wa mbegu za
mihogo na mtama kwa waathirika wa maafa ya mafuriko, mvua ya mawe na
upepo mkali. Mikoa iliyopata misaada hiyo ni Mtwara, Mara, Dodoma,
Shinyanga, Iringa, Tanga, Pwani, Lindi na Tabora. Pia Shilingi Milioni
516 zilitolewa kama fidia kwa watu waliotakiwa kupisha ujenzi wa upanuzi
wa mtaro katika eneo la Buguruni - Mnyamani. Serikali
imeimarisha Mfumo wa Upatikanaji wa Taarifa za Tahadhari za majanga kwa
haraka kwa kujenga vituo 16 vya upimaji wa hali ya hewa na kuweka vifaa
vya kupima wingi na kasi ya maji katika vituo 10 vilivyopo katika
mabonde ya mto Pangani na mto Ruvuma. Aidha, Serikali imetoa mafunzo kwa
Kamati za Maafa katika wilaya 14 za mikoa mitano nchini. Katika mwaka
2016/2017, Serikali itaendelea kuimarisha uratibu na menejimenti ya
maafa nchini kwa kuanzisha Wakala wa Usimamizi wa Maafa, kuzijengea
uwezo Kamati za Maafa za Mikoa na Wilaya na kuendelea kuimarisha Mfumo
wa Taarifa za Tahadhari ya Awali.
Kudhibiti Dawa za Kulevya
104. Mheshimiwa Spika,
dawa za kulevya ni changamoto kubwa kwani huwaathiri watu wengi hasa
vijana ambao ni nguvu kazi ya Taifa. Katika kukabiliana na changamoto
hiyo, Serikali kupitia Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya
ilifanya marekebisho ya Sera ya Kupambana na Dawa za Kulevya na
kuwasilisha Bungeni Muswada wa Sheria Mpya ya Kudhibiti
na Kupambana na Dawa za Kulevya na kupitishwa na Bunge lako Tukufu na
kuanza kutumika tarehe 15 Septemba 2015. Sheria hiyo inaipa Tume nguvu
zaidi ya kudhibiti na kupambana na tatizo hilo.
105. Mheshimiwa Spika,
Tume imeendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu athari za biashara na
matumizi ya dawa za kulevya na kutoa huduma za matibabu kwa waathirika.
Hadi kufika mwezi Februari 2016, zaidi ya watumiaji 2,223 wamepata
huduma katika Hospitali za Muhimbili, Temeke na Mwananyamala. Tume kwa
kushirikia na Jeshi la Polisi wameendesha misako, doria na operesheni
nchini kwa lengo la kudhibiti uuzaji, utumiaji na usafirishaji wa dawa
za kulevya, ambapo wamefanikiwa kuteketeza mashamba ya bangi na mirungi
katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Mara. Katika mwaka 2015/2016,
jumla ya watuhumiwa 43 walikamatwa na kiasi cha kilo 37.2 na kete 156 za
dawa aina ya heroin na bangi. Pamoja na ukamataji huo, Mahakama Kuu ya
Tanzania imetoa hukumu kwa kesi kubwa nne za dawa za kulevya. Katika
mwaka 2016/2017, Serikali itakamilisha utaratibu wa kuanzisha Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ili kuongeza ufanisi. Mamlaka
itashirikiana na Jeshi la Polisi kubaini mtandao wa wahalifu wa ndani
na nje ya nchi unaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa dawa za
kulevya nchini na kuwafikisha wahusika Mahakamani.
USTAWISHAJI MAKAO MAKUU DODOMA
106. Mheshimiwa Spika, mwaka 2015/2016, Mamlaka
ya Ustawishaji Makao Makuu imepima viwanja 957 katika maeneo ya
Mkalama, Nkuhungu Kusini na Mahungu. Vilevile, jumla ya viwanja 6,599
vilisanifiwa katika eneo la ukubwa wa Hekta 493 na kutoa vibali 275 vya
ujenzi. Katika mwaka 2016/2017, Mamlaka inatarajia kuandaa ramani za
jumla na ramani za kina katika maeneo ya Ihumwa na Hombolo pamoja na
kupima viwanja vipya 4,000 katika maeneo mbalimbali ya Mji wa Dodoma na
kujenga kwa kiwango cha lami barabara zenye urefu wa kilometa 23.
USHIRIKIANO WA KIMATAIFA
107. Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushiriki kwenye utengamano wa kikanda na kimataifa na kuendeleza Diplomasia ya
Uchumi na Siasa kwa kuzingatia maslahi muhimu ya Nchi yetu. Mathalani,
Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Miaka Mitatu (2016-2018) wa Ushirikiano
kati ya Tanzania na China. Mpango huo umeainisha miradi ya kipaumbele
ya uwekezaji wa viwanda mbalimbali nchini. Ushirikiano huo umelenga
kutumia fursa ya Dola za Marekani Bilioni 10 zitakazotolewa na Serikali
ya China chini ya Mpango wa kuzisaidia Nchi nne za Afrika, ikiwemo
Tanzania. Makubaliano hayo yalifikiwa katika Mkutano wa Sita wa Wakuu wa
Nchi wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika
Jijini Johannesburg, Afrika Kusini tarehe 5 Desemba 2015. Nchi nyingine
zitakazofaidika na Mpango huo ni Afrika Kusini, Ethiopia na Kenya. Serikali
pia imesaini Mkataba wa ushirikiano na Serikali ya Japan kwa ajili ya
ujenzi wa Gridi ya umeme na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kusaidia
mpango wa maboresho ya Terminal Two ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
108. Mheshimiwa Spika, ili
kuwezesha Nchi kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025, Serikali itaendelea
kusimamia na kutekeleza diplomasia thabiti ambayo itachangia katika
kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu ya Tanzania. Aidha, itakuza
ubia wa kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa kikanda, Barani Afrika na
wadau wengine wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa Tanzania inapata
manufaa ya fursa za utandawazi.
URATIBU WA SHUGHULI ZA SERIKALI
109. Mheshimiwa Spika, ili
kazi zote zilizopangwa kutekelezwa zifanyike kwa ufanisi, tunahitaji
uratibu mzuri wa sekta zote ili kila mmoja atekeleze wajibu wake
kikamilifu. Hivyo, kuanzia mwezi Julai, 2016 Serikali itaanza kutumia
mfumo wa wazi wa kielektroniki wa kufuatilia uwajibikaji na utendaji
kazi kwa mujibu wa Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu. Mfumo huo ni muhimu ili kuhakikisha kuwa utendaji
kazi unaendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kufikia
malengo yaliyopangwa. Mfumo huo utarahisisha ufuatiliaji wa utekelezaji
wa shughuli za Serikali kulingana na Ilani ya Chama Mapinduzi ya mwaka
2015, Mipango ya Maendeleo ya Kitaifa, Ahadi na Maagizo ya Viongozi
Wakuu. Aidha, Mfumo huo utapunguza ucheleweshaji wa utekelezaji,
mwingiliano wa majukumu na gharama zisizo za lazima katika utendaji
kazi.
HITIMISHO
110. Mheshimiwa Spika, nimetumia muda mrefu kuelezea baadhi ya shughuli ambazo Serikali ya Awamu ya Tano itazipatia kipaumbele. Kabla ya kuhitimisha Hotuba yangu, napenda kusisitiza masuala machache yafuatayo:-
(i) Tunayo
changamoto kubwa ya kutumia rasilimali fedha kidogo tuliyonayo kukidhi
mahitaji makubwa ya kutoa huduma bora kwa wananchi. Mathalani, upo upotevu wa mapato kwa kushindwa kudhibiti na kusimamia mapato na matumizi ya fedha za umma. Serikali
ya Awamu ya Tano itasimamia na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato
na kuhakikisha kwamba fedha za umma zinatumika kulingana na sheria na
kanuni za matumizi ya fedha za Serikali;
(ii) Tumedhamiria kufanya mapinduzi ya viwanda ili kujenga uchumi imara kwa faida ya wananchi. Hata
hivyo, tunalo jukumu kwa kila mmoja wetu kuunga mkono dhamira ya kweli
ya Serikali ili kufikia lengo hili. Tuungane na Mheshimiwa Rais kuondoa
kasoro zilizopo kwa kupunguza urasimu katika kuwawezesha wawekezaji wa
ndani na nje; kuimarisha huduma na miundombinu ya kiuchumi kama vile
umeme, barabara, reli, maji na rasilimali watu yenye ujuzi kuhakikisha
viwanda vilivyobinafsishwa na ambavyo havifanyi kazi vianze kufanya
kazi. Ni muhimu kuhimiza na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vyenye kutumia
malighafi iliyopo nchini kwa faida na maendeleo ya wananchi wetu.
Watanzania na wawekezaji kutoka nje mnakaribishwa kuwekeza;
(iii) Tunahitaji
kuboresha Sekta za Kilimo, Mifugo, Uvuvi na bidhaa za masoko kama njia
ya kujenga muunganisho wa sekta hizi na viwanda ili kuongeza thamani kwa
lengo la kuondoa umaskini
kwa wananchi wetu ambao wengi wao ni wakulima, wafugaji na wavuvi.
Tutumie akili, maarifa na nguvu zetu kuhakikisha kwamba wananchi
wanapata nyenzo na pembejeo za kuwaongezea uwezo wa uzalishaji wenye
tija kwa mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na misitu. Tumedhamiria kuupitia
mfumo wa masoko ya mazao yetu ili wakulima wauze kwa faida mazao yao;
(iv) Tunalo
jukumu kubwa la kuboresha huduma za jamii, ikiwemo elimu, afya,
upatikanaji wa maji safi na salama na miundombinu ya umeme hasa
vijijini. Tumeanza utaratibu wa kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi, kuanzia darasa la awali hadi kidato cha nne;
(v) Bado tunalo tatizo kubwa la biashara na matumizi ya Dawa za Kulevya. Tuunge
mkono juhudi za Serikali katika vita hii kubwa ya kupambana na tatizo
la Dawa za Kulevya ambazo zinaleta athari kubwa kwa wananchi hususan
vijana;
(vi) Umuhimu
wa kurejesha maadili katika utumishi wa umma ni suala la kipaumbele. Ni
vyema kila mtumishi wa umma kuzingatia sera, sheria na kanuni kuhusu
Maadili ya Viongozi na Watumishi wa Umma. Aidha, ni vyema viongozi na
watumishi wa umma kila mmoja kwa nafasi yake, awajibike kwa cheo na
dhamana aliyopewa katika kuwatumikia wananchi. Dhana ya “Kutumbua Majipu” iwe
kichocheo cha kuwabaini na kuwarekebisha wale wote wenye dhamira ya
kukiuka maadili kwenye nyadhifa zao na katika kuwatumikia wananchi;
(vii) Tunayo changamoto ya ukuaji wa uchumi ambao hauendi sambamba na kasi ya upatikanaji wa ajira. Aidha,
zipo dalili kwamba vijana wetu wamekuwa wakitumia muda mwingi kufanya
shughuli ambazo hazichangii sana katika ukuaji wa uchumi wa Taifa letu.
Tuendelee kuwahimiza vijana na kujenga utamaduni kwa kila mwananchi
kufanya kazi kwa bidii ili kujenga uchumi kwa maendeleo yetu. Tuunge mkono falsafa ya “Hapa Kazi Tu” na kwamba Asiyefanya kazi na Asile; na
(viii) Mwisho,
niwaombe Watanzania wote kuendelea kuishi kwa amani na utulivu. Tunayo
Nchi nzuri na Watanzania wote ni watu wenye upendo. Tudumishe amani,
umoja na mshikamano kwa kuwaunga mkono viongozi wetu ili tuongeze kasi
ya kuleta maendeleo katika Nchi yetu kwa maana Umoja ni Nguvu.
Sekta Binafsi, ambayo ndiyo Injini ya Ukuzaji Uchumi wa Taifa letu,
isiwe na tashwishwi hata kidogo. Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea
kuienzi na kuisaidia Sekta Binafsi katika kuchangia maendeleo ya Taifa
letu.
SHUKRANI
111. Mheshimiwa Spika, nitumie
fursa hii sasa kuwashukuru Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ushirikiano
walionipa tangu wateuliwe. Aidha, nawashukuru Wafanyakazi wote wa
Serikali na Taasisi zake chini ya Uongozi wa Katibu Mkuu Kiongozi, kwa
kukamilisha Bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017. Nawashukuru
Watanzania wote kwa kushiriki katika ujenzi wa Taifa.
112. Mheshimiwa Spika, vilevile, napenda kuwashukuru Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama,
Mbunge wa Peramiho, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge,
Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu); Mheshimiwa Dkt. Abdallah Saleh
Possi, Mbunge, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye
Ulemavu); Mheshimiwa Anthony Peter Mavunde, Mbunge wa Dodoma Mjini na
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Vijana) kwa
msaada na ushirikiano wao
mkubwa katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Nawashukuru vilevile Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Waziri Mkuu, chini ya
Uongozi wa Makatibu Wakuu, Dkt. Hamisi H. Mwinyimvua; Bwana Uledi A.
Mussa na Bwana Eric F. Shitindi kwa ushauri wao wa kitaalam ambao
wamenipa mimi na Waheshimiwa Mawaziri wa Nchi katika kipindi hiki.
Nawashukuru kwa kukamilisha kwa wakati maandalizi yote ya Makadirio ya
Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2016/2017.
113. Mheshimiwa Spika, katika
mwaka 2015/2016, Nchi yetu imepata misaada na mikopo kutoka kwa
Wahisani wetu mbalimbali. Misaada na mikopo hiyo imetoka kwa Nchi
rafiki, Nchi fadhili, Taasisi za Fedha duniani, Mashirika ya Umoja wa
Mataifa, Mifuko mbalimbali ya Fedha duniani, madhehebu ya dini na
Mashirika yasiyo ya Kiserikali. Misaada na mikopo hiyo imechangia sana
katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuboresha utoaji wa
huduma kwa wananchi. Napenda kuwashukuru wote kwa dhati na
kuwahakikishia kuwa Watanzania tunathamini misaada na mikopo
waliyotupatia na tutaendelea kushirikiana nao katika harakati za kuleta
maendeleo ya Taifa letu.
114. Mheshimiwa Spika, napenda
kutumia fursa hii kuwashukuru kwa dhati wapiga kura wangu wa Jimbo la
Ruangwa kwa imani na heshima kubwa waliyonipa ya kunikubali na
kunichagua kuwa Mbunge wao. Napenda kuwaahidi kuwa sitawaangusha.
Ninawashukuru viongozi wenzangu wote wa Kitaifa
na wa ngazi nyingine zote kwa ushirikiano mkubwa ninaoupata kutoka kwao
ambao umeniwezesha kutekeleza jukumu hili kubwa la kusimamia utendaji
wa Serikali katika sekta zote na kuwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali
Bungeni. Asanteni sana!
115. Mheshimiwa Spika, mwisho
napenda kuishukuru familia yangu hususan mke wangu Mary Majaliwa na
watoto wangu wote kwa kuniombea na kunipa moyo mara baada ya kuteuliwa
kushika wadhifa huu. Maombi yao yamenipa nguvu ya kutekeleza majukumu
yangu.
MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA ZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MWAKA 2016/2017
116. Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2016/2017, Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zake inaliomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi Bilioni Mia Mbili Thelathini na Sita, Milioni Mia Saba Hamsini na Tisa, Mia Nane Sabini na Nne Elfu, Mia Saba na Sita (236,759,874,706). Kati ya fedha hizo, Shilingi Bilioni Sabini na Moja, Milioni Mia Tano Sitini na Nne, Mia Mbili Tisini na Tatu Elfu, Mia Saba Sabini na Tatu (71,564,293,773) ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni Mia Moja Sitini na Tano, Milioni Mia Moja Tisini na Tano, Mia Tano Themanini Elfu, Mia Tisa Thelathini na Tatu (165,195,580,933) ni kwa ajili ya Matumizi ya Maendeleo.
117. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment