Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na
Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga (Mb.) (kulia), akizungumza na
Waandishi wa Habari kuhusu ziara ya kitaifa ya siku 4 ya Rais wa Vietnam
nchini, Mhe.Truong Tan Seng kuanzia tarehe 08 hadi 11 Machi, 2016.
Ziara hiyo itakuwa ni ziara ya kwanza ya kuja Tanzania pia Afrika.
Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga
naye akisikiliza kwa makini mazungumzo ya Waziri na Waandishi wa
Habari.
Waandishi wa Habari wakimsikiliza kwa makini Balozi Mahiga (hayupo pichani).
Bi. Mindi Kasiga naye akitolea ufafanuzi ratiba nzima ya ziara ya Rais huyo wa Vietnam.
Sehemu nyingine ya waandishi wa Habari wakinukuu baadhi ya pointi wakati mkutano ukiendelea. Picha na Reginald Philip
Rais
wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam, Mhe. Truong Tan Sang atakuwa Rais
wa kwanza kufanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania katika Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Rais Sang
atawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere siku ya
Jumanne tarehe 08 Machi 2016 saa mbili usiku na kupokelewa na Waziri wa
Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Mhe. Dkt. Augustine Mahiga ambapo mapokezi rasmi yatafanywa siku ya pili
na mwenyeji wake, Rais Dkt. Magufuli katika Viwanja vya Ikulu.
Akiongea
na Waandishi wa Habari Ofisini kwake leo, Waziri Mahiga alieleza kuwa
Rais Sang atafutana na mke wake, Mama Mai Thi, Mawaziri watano na
Wafanyabiashara 51 katika ziara hiyo. Dkt. Mahiga alieleza kuwa Serikali
inaupa uzito wa pekee ugeni huo kwa sababu ni ziara ya kwanza ya
kitaifa katika Awamu ya Tano kufanywa na Mkuu wa Nchi. “Wakuu wa Nchi
kadhaa walishakuja hapa nchini lakini kwa ziara za kikazi, sio za
kiserikali, hivyo Vietnam imetupa heshima kubwa sana”. Waziri Mahiga
alisema.
Rais
Sang ni mara ya kwanza kufanya ziara katika Bara la Afrika na Tanzania
ambapo pia atazuru nchi ya Msumbiji baada ya kuondoka hapa nchini tarehe
11 Machi 2016.
Dkt.
Mahiga aliwambia Waandishi wa Habari kuwa Tanzania ina mambo mengi ya
kujifunza kutoka Vietnam namna ilivyopiga hatua kubwa ya maendeleo
katika kipindi kifupi, licha ya kuendesha vita kubwa ya mapambano ya
kupigania uhuru dhidi ya Ufaransa na baadaye dhidi ya Marekani. Alisema
nchi hiyo imepiga hatua katika sekta za viwanda, kilimo, mawasiliano na
uvuvi. Kwa upande wa kilimo, nchi hiyo ni ya kwanza kwa kuuza kahawa
aina ya robusta na korosho duniani ingawa mbegu za mazao hayo
zimechukuliwa Tanzania.
Aidha, Vietnam ni maarufu duniani kwa kuuza samaki aina ya sato ambao walichukuliwa kutoka Ziwa Victoria.
Waziri
wa Mambo ya Nje alieleza kuwa ili Tanzania nayo ifike ilipo Vietnam ni
lazima ifuate mambo matatu ambayo Vietnam inayazingatia. Mambo hayo ni
kufanya kazi kwa bidii katika mazingira ya aina zote, utekelezaji wa
maamuzi wanayofanya na kuwekeza katika mafunzo ya ufundi, miundombinu
kama ya umeme, barabara, reli, bandari na mabemki kwa ajili ya mitaji na
huduma nyingine za kifedha.
Katika
ziara hiyo, Rais wa Vietnam pamoja na mambo mengine atafanya mazungumzo
rasmi na mwenyeji wake; Rais wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Ali Mohammed Shein;
Mwenyekiti wa CCM, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Spika wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai; Kuongea na
wafanyabiashara na kutembelea eneo la uwekezaji la EPZA, Ubungo Jijini
Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment