Makala : Nani anafaidika na rasilimali za Tanzania? - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Tuesday, 19 January 2016

Makala : Nani anafaidika na rasilimali za Tanzania?


Tanzania ni miongoni nchi chake katika bara la Arfica  iliojaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii.Tofauti na nchi nyengine nyingi za Africa na hata dunia kwa ujumla.miongoni mwa vivutio hivo vya utalii nchini Tanzania ni mbuga za wanyama.

Katika mkoa wa Iringa ambao unapatikana nyanda za juu kusini mwa Tanzania umejaliwa kuwa na mbuga ya wanyama ‘Ruaha Nationa park’mbuga hii ipo magharibi mwa Iringa katika kijiji cha tunga malenga kata ya Idodi kilimota 128 kutoka Iringa mjini.

Mbuga hii ni ya kipekee yenye wanyama wa kila aina na adimu kupatikana kuonekana sehemu nyengine ulimwenguni wanyama hao ni kama vile ‘kadu’ni aina ya wanyama ambao kisura wameshabihiana sana na swala lakini sio swala na ndio maana mwandishi wa makala hii anasema mbuga hii ni ya kipekee, Kijografia mbuga hii ya Ruaha imepakana na mikoa kadhaa ya Tanzania,miongoni mwa mikoa hio ni singida,Dodoma,mbeya na ina ukubwa wa kilomita za mraba 1300.
mwandishi wa makala hii Muhamed Khamis akizungumza na chifu wa kabila la kimasai katika kata ya idodi wilaya ya Iringa vijijini Chif Lameck mtemisika.
Wakaazi wa kijiji cha karibu na eneo hili’tungamalenga’wameleza kusikitishwa kwao licha ya uwepo wa kivutio kikubwa cha wageni lakini kwa upande wao wanaeleza hawafaidiki na lolote lile kupitia mbuga hio.

Kwa nyakati tofauti wakizungumza na mwandishi wa makala haya walisema uwepo wa mbuga hio kwao ni kama mzigo kwani haina faida kwao,bali ni  hasara inayotokana na wanyama hao kwa vipando vyao mashambani.

Wamesema haina faida kwa sababu hakuna kijana hata mmoja kutoka maeno hayo ambae ameajiriwa badala yake huajiriwa zaidi wageni kutoka mikoa mengine jambo ambalo linawalenga kuona uwepo wa mbuga hio ni kama mzigo na faida kwa wageni.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho Bwana Silasi mgeza  alisema tokea kuanza  uongozi wake takribani mwaka mmoja sasa hajawahi kuskia wala kuona uwepo wa ajira kwa vijana wake bali anachokijua yeye wanaoajiriwa wote ni wageni wa eneo hilo.

Alisema hio ni changamoto kubwa kwa wanakijiji hicho kwani matumaini yao waliamini uwepo wa mbuga hio wangeweza kuajiriwa vijana wao lakini hali ni kinyume na ndio maana wanasema mbuga hio ni mzigo kwao.
‘’licha ya uwepo wa kivutio hichi lakini hadi barabara  hii ni mbovu nadhani umeona ndugu mwandishi wakati unafunga safari ya kuja kijijini hapa’’alieleza mwenyekiti huyo.

Licha ya tatizo hili la barabara lakini pia suala la elimu bado kabisa miundombinu mibovu katika suala la elimu katika kijiji hichi,wananchi waliamini uwepo wa secta hii ya utalii kwa kiasi kikubwa ungesaidia secta hii ya elimu kwa kiasi kikubwa ikiwa ni kujenga skuli ya kileo na kusaidia kupatikana kwa walimu.

Rashid Salehe ni mwanafunzi aliehitimu kidato cha nne kwa sasa anasubiri matokeo yake alisema anashangazwa hadi leo hii shule yao ni mbovu huku kukiwa na uhaba mkubwa wawalimu shuleni hapo,anaamini iwapo mbuga za wanyama zingetumiwa vyema zingewasaidia wanafunzo mashuleni kusoma katika mazingira bora.

Alieleza tayari amemaliza kidato cha nne lakini hana imani kama anaweza kufaulu kutokana na ukosefu wawalimu waliokuwa nao jambo ambalo linamkatisha matumaini makubwa alikuwa nayo ya kufika chuo kikuu.
Aliamini kupitia waandishi wa habari kufichua yanayowakabili kijiji kwao hwenda siku moja kijiji hicho kikapiga hatua kimaendeleo kama vijiji vyengine Tanzania.

‘’Wakati mwengine natamani hata kuwalaumu wazazi wetu ni kwanini walikubali uwepo wa hifadhi hii bila kutoa masharti maalumu,angalia sasa watoto wao tunafeli kwa kukosa walimu huku watoto wa wengine wanasoma vizuri kupitia rasilimali zetu’’alieleza Rashid.

Tukizungumzia suala la afya katika kijiji hichi nalo pia limeonekana kuwa mtihani mkubwa mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Tungamalenga alinileza wana uhaba mkubwa wa madaktari hospitalini hapo,jambo ambalo linawawia vigumu sana kina mama wanaotaka kujifungua .

‘’Wake zetu wanalazimika kujifungulia Iringa mjini jambo ambalo ni shida sana kutoka hapa mpaka Iringa mjini ni karibu masaa manne,hali hii inaweza hata kupelekea kufariki dunia wakati mwengine ukizingatia njia mbovu tulionayo alinieleza mwenyekiti huyo.

Wahusika wakuu wa suala hili ni kina mama nao hawakuwa kimya walipaza sauti zao wakati wakizungumza na mwandishi wa makala hii ingawa hawakupenda kutajwa majina yao kwa kuhofia kile kilichowakuta wenzao mwaka jana ambapo walitoa taarifa kwa moja ya chombo cha habari na wakapata matatizo makubwa kijijini hapo ingawa hawakuwa tayari kueleza matatizo hayo.

Waliniambia changamoto kubwa wamekuwa wakizipata wanapokwenda hospitali ya kijiji hicho ambacho dawa ni kwa uchache sana lakini pia uhaba wa wauguzi hospitalini hapo.

‘’Tunaiomba Serikali ichukue tatizo hili tukiwa kama wananchi wa Tanzania ambao tunahitaji msaada wa kutatuliwa changamoto zetu’’walieleza kina mama hao kwa nyakati tofauti.

Wakazi wengi wa kijiji hichi cha tungamalenga ni wakulima na wafugaji ingawa yapo makabila kadhaa yanayoishi hapa,mwandishi wa makala hii alizungumza na mwenyeti wa kijiji na kuelezwa makabila hayo ni wahehe,wangoni,wamasai na nk.

Kwa nyakati tofauti baadhi ya kina mama ambao wanajishughulisha na shughuli za kilimo walinieleza wanatamani angalau kupatiwa nyezo za kilimo chao ili watimize ndoto zao siku moja kuwa wakulima bora kama walivo wengine.Walieleza wanatamani kuona angalau uwongozi wa mbuga ya wanyama katika kijiji hicho wanawapa kipaombele zaidi kutoka na shida walizonazo.

‘’Chakushangaza hawajali kabisa hata jitihada zetu na ndio maana wanyama wao wanakuja hapa kila mda kuharibu mazao yetu na wanajua kila kitu hatuna lakuwafanya’’walieleza kina mama hao.

Jitihada za mwandishi wa makala hii zilikwenda mbali zaidi kwa kufanikiwa kuonana na mmoja miongoni mwa walinzi wa mbuga hio ambae hakupenda kutajwa jina lake kwenye makala hii alisema ni kweli wananchi wa kijiji jirani hakuna hata mmoja anaefanya kazi hapa(Tungamalenga).

Alisema wakuu wa sehemu hio wamekuwa wakitumia kigenzo cha elimu katika ajira zao jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa wakaazi wa hapo ingawa wapo wachache waliosoma lakini pia hawakuajiriwa.

Mlinzi huyo alieleza kuskitishwa kwake na utaratibu huo ingawa yeye pia si miongoni mwa wananchi wa kijiji hicho lakini alidai anaona uchugu zaidi kuona hakuna hata mtu mmoja kutoka Tungamalenga alieajiriwa ingawa nafasi ni nyingi zisizohitaji elimu.

‘’Zipo kazi tele hapa za kufanya kwa kutumia nguvu zaidi na sio akili,aina hii ya kazi haihitaji elimu sijui ni kwanini uongozi wa hapa unabaguwa katika ajira’’alieleza mlinzi huyo kwa masikitiko.

Kuhusiana na suala la mapato yanayotokana na mbuga hio mlinzi huyu alisema hana uhakika juu ya matumizi yake sahihi inga wa anaamini ni lazima ubadhilifu uwepo kutokana na hali halisi ilipo mbugani hapo na Tanzania kwa ujumla.

Upande wa pili kwa wakaazi wa kijiji hichi ni kutoka katika kabila la kimasaid ambapo mwanidishi wa makala hii alikutana na kiongozi wa kabila hilo kuzungumzia uwepo wa tatizo hili la ajira kwa vijana wa kijiji hichi.
Alisema hata wao ambao wana weledi mkubwa wa wanyama wamekoseshwa ajira lakini hilo haliwaumizi zaidi kinachowaumiza wao ni kuondolewa maeno wanayoishi kwa madai kupewa wawekezaji huku wamamasai wakisahauliwa kabisa.

‘Wametusahau kama sisi ni watanzaia kama walivowengine pia tunahitaji haki kama wanayopewa wawekezaji,angalia kundi hili la ngombe linakosa chakula sasa tumefukuzwa kilichobaki ni kutuletea mgogoro na wakulima kwa mashamba yao’’alieleza chif lamek.

Alishauri Serikali  kupitia wizara ya mali asili Tanzania kuangalia upya suala la wawekezaji vyenginevyo linaweza kuibuwa mgogoro mkubwa zaidi hapo badae lisipochukuliwa hatua suala hili.

Jicho la Serikali limekuwa likiangaza zaidi kuhusiana na suala la ujangiri kwa wanyama pori huku wakisahau uwepo wa hali hio unatokana na tatizo la wananchi wenyewe kutokufaidika na hifadhi zao na ndio maana wamekuwa na maamuzi yasiosahihi kwa taifa huku wakiamini ndio njia peke ya kujinufaisha kupitia mali zao.

Tanzania iwapo itatumia vyema rasilimali zake zilizonazo ni wazi kabisa tutafika mbali kimaendeleo ikiwa tutakubali rasilimali hizi ziwafaidishe watanzaia wenyewe na sio wageni au wachache huku tukiwasahau wananchi wanaoishi karibu na rasilimali zao.

Naamini suala la ujangiri na mabaya yote kwa rasilimali zetu yataondola iwapo watanzania watakuwa miongoni mwa wanaofaidia kinyume na hivi sasa ambapo watanzania wamekuwa njia ya kuwafaidisha wachache miongoni mwao.

Mhammed khamis
 University of Iringa (UoI)
 0652729061

No comments:

Post a Comment