Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Dkt.
Mohammed Gharib Bilal, akiwasha Mshumaa katika Kaburi ya Hayati Baba wa Taifa
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kama ishara ya Kumbukumbu wakati alipofika
katika Jumba la makumbusho Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015 baadda ya
kuadhimisha Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) iliyofanyika Butiama.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Dkt.
Mohammed Gharib Bilal, akiweka Shada la Maua katika Kaburi ya Hayati Baba wa
Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kama ishara ya Kumbukumbu wakati
alipofika katika Jumba la makumbusho Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015
baadda ya kuadhimisha Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) iliyofanyika Butiama. Kushoto
ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Kenya, Eugene Wamalwa.
Makamu wa Rais waJamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati wa sherehe za maadhimisho ya
Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika kwenye Uwanja wa Mwitongo, Butiama mkoani
Mara leo Sept 15, 2015
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mbogo Futakamba (kushoto)
akibadilishana mikataba na Waziri wa Maji na Umwagiliaji wa Kenya, Eugene
Wamalwa, mara baada ya kusainiana Mkataba huo wa Maridhiano ya Mto Mara, wakati
wa sherehe za Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika
Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015. Kulia
ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanznia, Dkt. Mohammed Gharib
Bilal, akishuhudia.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mbogo Futakamba
(kushoto) na Waziri wa Maji na
Umwagiliaji wa Kenya, Eugene Wamalwa (katikati) wakitiliana saini mkataba wa
Maridhiano ya Mto Mara wakati wa sherehe za Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya
Mara (Mara Day) zilizofanyika Butiama mkoani
Mara leo Sept 15, 2015. Kulia ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanznia, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akishuhudia.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Mohammed Gharib Bilal, akimkabidhi Tuzo ya kushiriki maadhimisho na kutunza
mazingira, Mwakilishi wa Serikali ya Jimbo la Narok nchini Kenya, Rebeccah
Seenoi, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day)
zilizofanyika kwenye Uwanja wa Mwitongo,
Butiama mkoani Mara leo Sept 15, 2015.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.
Mohammed Gharib Bilal, akipata maelezo kutoka kwa Eugene Muramira, wakati
alipotembelea katika Banda la maonesho la Afrika Mashariki, wakati wa Sherehe
za Maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Mara (Mara Day) zilizofanyika leo Sept 15,
2015 kwenye Uwanja wa Mwitongo Mkoani Mara. Picha na OMR
HOTUBA
YA MHESHIMIWA DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO
WA TANZANIA KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO
YA SIKU YA MARA (MARA DAY), BUTIAMA-MARA
TAREHE
15 SEPTEMBA 2015
Waheshimiwa Mawaziri kutoka Tanzania na Kenya;
Makatibu Wakuu wa Wizara;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Magavana wa Majimbo;
Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya;
Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Caunt kutoka Kenya;
Wawakilishi kutoka Jumuiya ya Afrika
Mashariki na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria;
Wataalam kutoka Wizara, Taasisi mbalimbali Kenya na Tanzania;
Wadau wa Maendeleo;
Wawakilishi wa Jumuiya za Watumiaji Maji;
Ndugu Wanahabari;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana
Kwanza kabisa nianze kwa
kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya njema na
kutuwezesha kukusanyika hapa siku ya leo kushuhudia tukio hili muhimu. Napenda
nitumie nafasi hii pia kuwashukuru waandaji wa shughuli hii, kunialika kuwa
Mgeni Rasmi katika siku hii ya pekee ambayo wadau wa Bonde
la Mto Mara, wanakutana katika Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mara (Mara
Day). Nimepokea mwaliko huu kwa mikono miwili, nasema; Asanteni Sana! Nitumie
fursa hii pia kuwakaribisha mkoani Mara, hususani hapa Butiama, wageni
mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania. Nasema Karibuni Sana Butima.
Jisikieni mpo nyumbani. Hili ni eneo lenye historia kubwa kwa Tanzania na Bara
la Afrika kwa ujumla kwani ndipo
alipozaliwa na alipolala, Baba wa Taifa letu na Mtetezi wa Wanyonge Barani
Afrika na Duniani kwa ujumla, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere(Mwenyezi Mungu
ailaze roho yake mahali pema peponi). Napenda pia nitumie nafasi hii
kuwashukuru waandaaji wa sherehe hizi na wadau mbalimbali waliochangia kwa
namna moja ama nyingine kufanikisha shughuli hii. Endeleni na moyo huo, fanyeni
kila linalowezekana kuzidi kuboresha jambo hili mwaka hadi mwaka.
Ndugu
Wageni Waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Tukio la leo linatoa fursa
kwa wadau kutoka nchi mbili, Tanzania na
Kenya zinazopitiwa na Bonde la Mto Mara, kukutana pamoja na kujadili masuala mbalimbali
ya uhifadhi na matumizi endelevu ya Mto Mara na kutafakari mustakabali wa Bonde hili kwa ujumla.
Hifadhi za Mto Mara zina
umuhimu mkubwa kiuchumi kwa nchi hizi mbili kutokana na mapato yatokanayo na
utalii. Wanyama waliopo katika hifadhi za Serengeti nchini Tanzania na Maasai
Mara kwa upande wa Kenya, hutegemea sana maji ya Mto Mara kwa maisha yao. Aidha siku hii inakwenda sanjari na msimu wa
uhamaji wa wanyamapori jamii ya nyumbu ambapo inakadiriwa kuwa jumla ya nyumbu Milioni mbili wanahama na kurudi
kutoka mbuga za Serengeti- Tanzania na
Maasai Mara nchini Kenya kwa kipindi cha
Julai na Oktoba kila mwaka.
Kaulimbiu ya Madhimisho ya mwaka huu ni “Mto Mara: Maisha yangu,
Maendeleo yangu”. Kaulimbiu hii ni nzuri kwani inalenga kusisitiza dhamira
ya dhati ya usimamizi shirikishi wa rasilimali za maji na nyinginezo katika
Bonde la Mto Mara. Fanyeni kila linalowezekana kuhakikisha mnabadilisha Bonde
hili na kuwa mfano katika shughuli za maendeleo ikiwa pamoja na kufungua
milango na fursa zaidi za uwekezaji. Ni wajibu wa wadau wote wa Bonde hili
kuhakikisha chini ya Ushirikiano mzuri wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, vitega uchumi mbalimbali vinawekezwa katika
Bonde hili ili kusaidia wananchi wa nchi
hizi mbili kuondokana na umasikini .
Wageni
Waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Mto Mara ni mto wa
kimataifa unaounganisha nchi mbili za Tanzania na Kenya. Wananchi na wadau
mbalimbali wa nchi hizi waishio katika
Bonde la Mto Mara wanatumia maji na rasilimali zingine kama ardhi na misitu
katika bonde hili kwa ajili ya kuendeleza maisha yao ya kijamii na kiuchumi kwa
nia ya kupunguza umasikini. Hata hivyo kadri ya miaka inavyokwenda, hali ya
rasilimali hizi imekuwa ikipungua kutokana na matumizi mbalimbali.
Hivi sasa tunashuhudia
matumizi ya rasilimali hizi yakiongezeka kutokana na ongezeko la mahitaji ikiwa
ni pamoja na ongezeko la fursa za kiuchumi. Kwa upande mwingine tunashuhudia
rasilimali hizi zikipungua na kuharibika hivyo kupunguza fursa ya nchi hizi na
jamii, kujikwamua kiuchumi na kupunguza umasikini. Wakazi wa Bonde hili sasa
wanashuhudia kupungua kwa maji na uchafuzi wa maji, kuzidi kupungua kwa misitu
kunakosababishwa na ukataji holela wa miti, uharibifu wa ardhi na uharibifu
mkubwa wa mazingira kwa ujumla unaosababishwa na shughuli za kibinadamu. Wito
wangu kwenu tunapoadhimisha Siku hii ya Mara, ni wajibu wa kila mmoja wetu
kutafakari juu ya changamoto za msingi zinazopaswa kuchukuliwa katika kuboresha
matumizi endelevu na usimamizi wa Bonde
hili. Sote tunafahamu kuwa Bonde la Mto
Mara lina umuhimu mkubwa kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa eneo hili, hivyo ni
wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha linatunzwa na kuendelezwa ili lisadie
wananchi wetu kupata maisha bora na kuondokana na umasikini.
Ni wajibu wetu sote
kuhakikisha tunatilia mkazo suala la utunzaji mazingira katika Bonde hili.
Uharibifu wa Mazingira ni moja ya tatizo
linalotishia kwa kiasi kikubwa uhai wa Bonde hili. Tusipotilia mkazo utunzaji
mazingira katika eneo hili tutaathiri kwa kiasi kikubwa rasilimali zilizomo
katika Bonde hili na kukwamisha juhudi za wakazi wa eneo hili kujikwamua na
umasikini. Tukiendelea kuharibu mazingira ya Bonde hili tutasababisha matatizo
mengi ikiwa ni pamoja na kupungua kwa kiasi kikubwa cha maji kwenye Mto Mara.
Jambo hili halitaathiri wanyama tu bali linaweza hata kusababisha migogoro ya wanaotumia maji hayo katika nchi hizi
mbili. Rai yangu kwa wadau wote wa Bonde la Mto Mara ni kwamba, Maadhimisho ya
Siku ya Mara kila mwaka yawe chombo cha
kuhakikisha kuwa hatufiki huko. Naamini kwamba Serikali za nchi zote mbili Tanzania
na Kenya zina sera, sheria na mikakati
mizuri inayolenga kuhifadhi na kuhakikisha usimamizi na matumizi endelevu ya
rasilimali mbalimbali za Mto Mara kwa ajili ya maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Lazima tuwe na chombo chenye malengo ya pamoja ya kusimamia Sera na Sheria
hizo.
Wageni
Waalikwa;
Mabibi
na Mabwana;
Kabla ya kuhitimisha hotuba
yangu kwa mara nyingine naomba niwashukuru wadau wote mliofanyikisha
Maadhimisho haya, bila kuwasahau ndugu zetu kutoka Jamhuri ya Watu Kenya kwa
namna mlivyojitoa kufanikisha shughuli hii. Asanteni Sana! tuzidi kushirikiana
na Karibuni tena na tena.
Baada ya kusema hayo, kwa
heshima kubwa na taadhima sasa natamka
rasmi kuwa; Sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Mara, zimefungwa rasmi.
Asanteni
sana kwa kunisikiliza.
CHIMBUKO
LA MAADHIMISHO YA SIKU YA MARA.
1. Utangulizi:
Maadhimisho
ya siku ya Mara hutoa taswira ya jinsi viongozi na wananchi wanchi mbili za
Kenya na Tanzania wanavyoshirikiana katika kusherehekea maadhimisho ya siku
hiyo. Hii ni mojawapo ya shughuli muhimu katika kuimarisha ushirikiano katika
Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kilele cha Maadhimisho hayo huwa ni tarehe 15
Septemba ya kila mwaka.
2. Bonde la Mto Mara:
Bonde
hili ni moja kati ya mabonde yenye mito inayoingiza maji katika Ziwa Victoria.
Bonde hili linahusisha nchi za pande mbili ambazo ni Kenya ambayo inamiliki
takribani asilimia 65 ya eneo bonde na Tanzania asilimia 35. Asili ya mto Mara
ni chemichemi ya Enapuyapui iliyoko kwenye misitu ya milima ya Mau katika nchi
ya Kenya na maji yake hutiririka kuelekea katika pori la akiba la hifadhi ya
Taifa ya Maasai-Mara kwa upande wa Kenya, na kwa upande wa Tanzania mto Mara
unapita katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti kabla ya kumwaga maji yake katika
Ziwa Victoria nchini Tanzania ambapo mto huo hupita katika Wilaya nne za
Serengeti, Tarime, Butiama na Rorya. Ikolojia ya Bonde la mto Mara ni moja kati
ya Ikolojia muhimu katika Bonde la Ziwa Victoria ambayo inachangia maendeleo
endelevu ya kiuchumi na kijamii pamoja na utumiaji na uhifadhi wa uoto wa
Asili.
3. Chimbuko la Maadhimisho ya Siku ya
Mara.
Maadhimisho
hayo ni kufuatia maamuzi yaliyofanywa na Baraza la Mawaziri wanaohusika na
masuala ya Bonde la Ziwa Victoria kwenye Mkutano wa kumi uliofanyika tarehe 04
Mei, 2012 huko Kigali Rwanda. Katika Mkutano huo iliamuriwa kuwa maadhimisho
hayo yafanyike kwa kupokezana baina ya nchi zote mbili za Kenya na Tanzania.
4. Faida ya maadhimisho haya:
Siku
ya Mara hutumika katika kuendelea kulitangaza na kulifuatilia tukio muhimu la
wanyamapori hasa nyumbu kuhama kutoka mbuga za hifadhi ya Taifa ya Serengeti
katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda katika pori la hifadhi ya Taifa
la Maasai-Mara katika Jamhuri ya Kenya na baadaye kurudi Tanzania na mara zote
mbili wanyama hao huvuka mto Mara.
Uamuzi
huo wa kuadhimisha Siku ya Mara, ulitokana na kutambua umuhimu wa Ikolojia ya
Bonde la mto Mara ambapo siku hiyo itatumika kuhamasisha jamii juu ya umuhimu
wa kulinda na kuhifadhi mto Mara. Aidha, maadhimisho ya siku ya Mara pia
hutumika katika kufanya yafuatayo:
i.
Kujengea
jamii uwezo juu ya uelewa wa masuala ya mazingira na changamoto za kijamii
zinazojitokeza katika Bonde la mto Mara.
ii.
Kuwawezesha
wadau kushiriki katika fursa zinazohusiana na Bonde la mto Mara
iii.
Kuitambulisha
sura ya Bonde la mto Mara kama eneo muhimu la uwekezaji
iv.
Kujadili
mwendelezo wa utekelezaji wa shughuli zilizoratibiwa katika Bonde la mto Mara.
5. Changamoto zinazolikabili Bonde la mto
Mara
Jamii
inayoishi katika Bonde la mto Mara pamoja na wadau mbalimbali wameendelea
kushuhudia upungufu mkubwa wa kiwango cha maji pamoja na uchafuzi wa vyanzo vya
maji kutokana na shughuli za kibinadamu, hali inayopelekea kuwa kikwazo kwa
jamii inayoishi katika Bonde la mto Mara katika juhudi zao za kujiongezea
kipato, kuwa na afya imara, kuwa na chakula cha uhakika pamoja na kukuza
uchumi.
Changamoto
hizi zinazotishia kutoweka kwa maliasili (Ikolojia) ya Bonde la mto Mara
zinatokana na shughuli za kila siku za kibinadamu ambazo ni pamoja na matumizi
ya ardhi yasiyo endelevu, ukataji miti holela kwa ajili ya kuchoma mkaa na
ujenzi, uchimbaji holela wa madini, uchafuzi wa vyanzo vya maji, kilimo kisicho
endelevu na ufugaji usio endelevu.
Shughuli
zingine ni sera na sheria za nchi mbili kutofautiana, ukosefu wa elimu ya
hifadhi ya mazingira kwa wakazi waishio katika Bonde la mto Mara, umaskini kwa
wakazi wengi wanaoishi katika Bonde, udhaifu wa kusimamia sheria pamoja na
ukosefu wa chombo shirikishi cha kusimamia rasilimali za bonde la mto Mara,
hizi zikiwa ni baadhi tu ya changamoto.
No comments:
Post a Comment