Na
Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Simu Tanzania (TTCL) sasa inayawezesha wateja wake ikiwa ni
pamoja na kampuni, taasisi na ofisi za Serikali kupata mawasiliano ya
intaneti sehemu ambazo ziko mbali na njia ya Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano kwa njia ya Satelaiti.
Akizungumza
katika Maonesho ya 39 ya Biashara ya Kimataifa, katika viwanja vya
Mwalimu Nyerere, Sabasaba, Ofisa Mtatuzi wa Masuala ya Kiufundi wa TTCL,
Fredrick Benard alisema teknolojia hiyo mpya ni muhimu sana kwa
makapuni na wateja wengine kwani ina ubora, uhakika kwa matumizi na ni
bei nafuu.
Alisema
mbali na mawasiliano ya intaneti wateja wanaweza pia kupata huduma ya
kuunganishwa kimawasiliano ya shughuli za kiofisi kwa ofisi zaidi ya
mbili ambazo zipo maeneo tofauti na kushirikiana kwa taarifa na mifumo
ya kikomyuta (Mpls Vpn).
Alisema TTCL iliamua kuleta huduma hiyo kutokana na mahitaji makubwa ya matumizi ya intaneti kwa shughuli za maendeleo.
“Kuna
maeneo ambayo awali yalihitaji huduma ya Mkongo(Fibre) lakini kutokana
na umbali pamoja na gharama imekuwa ngumu kuwapelekea huduma, suluhisho
la changamoto hiyo imeishapatikana, sasa taasisi hizo zinaweza pata
mawasiliano ya intaneti kwa njia ya Satelaiti, ubora wake ni ule ule
kama unaopatikana kwenye Mkongo (Fibre), alisema Benard.
Kwa
upande wake, Kaimu Mkuu wa Biashara Kanda ya Dar es salaam, Karim Bablia
akifafanua zaidi juu ya huduma hiyo alisema itawasaidia zaidi wamiliki
wa hoteli za kitalii, hospitali, vyuo na shule ambazo awali zilihitaji
huduma ya intaneti yenye kasi maeneo yasio na mkongo na kupata huduma
hiyo na kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo yao.
“…Kinachotakiwa
mteja anatakiwa kuleta maombi rasmi ya huduma anayoitaka kama ni
internet au Mpls Vpn baada ya hapo mteja atapelekewa tathmini ya gharama
ya kuunganishiwa juu ya huduma hiyo,” alisema.
Aidha
Bablia aliongeza kuwa teknolojia ya satelaiti itaweza kutoa huduma za
intaneti kwa wateja wake walio nje ya uwezo wa kufikiwa na huduma ya
intaneti kupitia waya (Mkongo).
Hivyo
basi, teknolojia hii itashughulikia haraka changamoto za TEHAMA nchini,
na kuchangia katika upatikanaji wa huduma na taarifa kwa haraka zaidi.
“Kupitia
Satelaiti wateja wanategema kupata huduma mbalimbali kama vile intaneti
yenye kasi, Mkutano kwa njia ya video (Video conference) na MPLS VPN,”
alifafanua.
Alibainisha kuwa kampuni ya Simu Tanzania(TTCL) sasa inaendelea na
mkakati wake kufanya mabadiliko katika kampuni na biashara kwa lengo la
kuhakikisha kuwa inatoa fursa kwa taasisi, makampuni ya umma na binafsi
ili waweze kuongeza ufanisi na uzalisha katika maeneo yao, kuongeza
pato na kukuza uchumi wa Taifa.
No comments:
Post a Comment