Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Mhandisi Philbert Rweyemamu akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Bi Josephine Matiro jengo la maabara la shule ya Sekondari ya Mazinge ambalo limejengwa kwa ufadhili wa kampuni yaKuchimbaDhahabu ya Acacia. Anayepiga makofi ni mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini Mh Steven Masele.
Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii Kanda ya Kaskazini aliyekuwa mkoani Shinyanga.
Kampuni ya Uchimbaji wa Madini ya Acacia kupitia mgodi wake wa Buzwagi imetumia zaidi ya shilingi Mil 400 kukamilisha miradi minne ya ujenzi wa vyumba vya maabara katika Shule za sekondari za Mazinge, Kizumbi, Ngokolo na Old Shinyanga zote za Manispaa ya Shinyanga.
Akizungumza wakati wa kukabidhi maabara hizo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Buzwagi Mhandisi Philbert Rweyemamu amesema, Acacia imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo yote ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya kampuni ya kufanya uchimbaji unaojali na hususani kwa kutekeleza miradi katika maeneo yanayozunguka migodi ya Acacia.
Kukamilika kwa miradi hii kunatajwa kuwa kutasaidia katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa wataalamu wa sayansi katika maeneo mbalimbali hapa nchini “Matumaini ya Kampuni ya Acacia ni kuona Tanzania inapata wataalamu wengi katika fani za Sayansi, ambao watasaidia katika maendeleo ya taaluma hii” Alisema Injinia Philbert Rweyemamu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mjini Bi Josephine Matiro ameupongeza Mgodi wa Buzwagi kwa namna ambavyo umekuwa ukishirikiana na wananchi wa Shinyanga katika kukamilisha miradi mbalimbali. “ Wananchi wetu wengi ni wa kipato cha chini, msaada huu mlioutoa ni mkombozi kwao lakini pia kwa watoto wetu maana mmetutengenezea mazingira mazuri ya watoto wetu kusoma na hapana shaka hawa watabadili hali ya maisha yetu na kuwa mazuri pindi watakapohitimu masomo yao” Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo hilo ambaye pia ni naibu Waziri ofisi ya makamu ya rais Mh. Steven Maselle amesema uwepo wa wawekezaji hapa nchini umekuwa ni chachu ya maendeleo, kutokana na ushiriki wao katika kutekeleza miradi mbalimbali ambayo imekuwa ya manufaa kwa jamii.
Mbali na utekelezwaji wa ujenzi wa maabara hizi za manispaa ya Shinyanga, katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita Acacia ilikabidhi pia maabara nyingine kwa Shule ya Sekondari Kinaga katika wilaya ya Kahama ambapo mradi huo uligharimu shilingi milioni mia moja na sitini pamoja na nyumba 3 kwa waathirika wa tukio la mvua za Mwakata zenye thamani ya zaidi ya shilingi za kitanzania milioni mia moja.
“Acacia kupitia Mgodi wake wa Buzwagi Pamoja na migodi mingine ya Bulyanhulu na North Mara itaendelea kushirikiana na jamii zinazotuzunguka katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa jamii na hasa katika maeneo ya afya, elimu, barabara, maji, pamoja na utoaji wa elimu ya ujasiliamali kwa vikundi mbalimbali.” Injinia Philbert Rweyemamu.
|
No comments:
Post a Comment