Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akisaini mkataba wa makubaliano ya kuwa na soko la pamoja kwa Nchi za
Wanachama wa Kanda ya tatu ya Nchi za Afrika Mashariki, Kusini mwa
Afrika na za Magharibi. Dkt.Bilal pamoja na Viongozi wa Nchi husika
wamesaini mkataba huo leo katika Mkutano mkuu wa tatu wa Wakuu wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la pamoja la Nchi za Kusini mwa
Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Sharm El Sheikh,
nchini Misri.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akizungumza jambo na Waziri wa Afrika Mashariki, Dkt. Harrison
Mwakyembe, akimpongeza baada ya kusaini mkataba huo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akipongezwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima,
baada ya kusaini mkataba huo.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal,
akiwa na baadhi ya Mawaziri wake katika mkutano mkuu wa tatu wa Wakuu
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Soko la pamoja la Nchi za Kusini
mwa Afrika (COMESA) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
uliofanyika leo Juni 10, 2015 kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa
Sharm El Sheikh, nchini Misri. Picha na OMR.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal
leo Jumatano Juni 10, 2015 amemuwakilisha Rais Jakaya Mrisho Kikwete
kwenye mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaolenga kuweka saini ya
makubaliano ya kuwa na soko la pamoja kwa nchi wanachama wa kanda tatu
za Afrika yaani Afrika Mashariki, Nchi za Kusini mwa Afrika na Nchi za
Afrika Magharibi, katika mji wa Sharm El Sheikh nchini Misri.
Makamu
wa Rais katika mkutano huu amemuwakilisha Rais Kikwete kwa nafasi yake
kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo alipata fursa ya
kuhutubia kwa niaba ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Wengine waliohudhuria katika mkutano huo ni pamoja na Rais Robert Mugabe
ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa SADC, Rais Abdel Fattah El-Sisi, Rais
wa Misri pamoja na watendaji wa SADC akiwemo Dkt. Stargomena Tax na
Balozi Richard Sezibera Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Pia
mkutano huo ulihudhuriwa na Katibu Mkuu wa COMESA, Rais wa Benki ya
Dunia pamoja na wawakilishi wa Mashirika mbalimbali ya Kimataifa
yanayohusika na Biashara na Viwanda.
Mkutano
huu unafanyika baada ya miaka takribani saba, ambapo wakuu wa nchi
katika kanda hizi walipendekeza kuwepo mkakati wa kuwa na soko huru kwa
nchi zote 26 na mkakati huu, sasa unasainiwa rasmi katika mkutano wa leo
hapa Sharm el Sheikh.
Katika
hotuba yake kwa niaba ya Afrika Mashariki, Mheshimiwa Makamu wa Rais
alisema, nchi zilizopo Afrika Mashariki zimepokea mkakati huu na kwamba
ziko tayari kupokea makubaliano kutokana na kubaini faida kubwa ya
kuleta uhuru kwa nchi nyingi za Afrika pamoja na kupunguza mipaka ya
kibiashara ambayo kwa miaka mingi imekuwa ikiathiri kukua kwa uchumi wa
Afrika.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais alifafanua kuwa, ili Afrika iendelee na ili iweze
kukabiliana na vikwazo vya kimaendeleo ni lazima kuwepo fursa za kutanua
uchumi na hasa kwa kuangalia rasilimali zilizopo Afrika ili ziweze
kukuza uchumi wa ndani katika Bara hili. “Hatuwezi kufanikiwa kama kila
mmoja atafanya mambo haya kivyake. Lazima kuwepo mtangamano kama huu kwa
maslahi mapana ya Afrika,” Mheshimiwa Makiamu wa Rais alisema.
Awali
akihutubia mkutano huo, Rais wa Misri Abdel Fattah El Sisi alisema,
Misri inajivunia kushiriki katika hatua hii mjuhimu ya kufungua mipaka
ya kibiashara katika Afrika na kwamba anatumia nafasi hiyo kuonesha
namna nchi yake ilivyo tayari kuhakikisha makubaliano ya Sharm el Sheikh
yanafanikiwa. “Nawakaribisha Misri na asanteni kwa kuja, sisi tuko
tayari kuhakikisha kuwa nia hii njema ya nchi za kanda hizi tatu
inafanikiwa,” alisema Rais Sisi.
Katika
mkutano huu, viongozi mbalimbali wamehudhuria na baadhi yao ni Mfalme
Mswati III wa Swaziland, Rais Omar al Bashir wa Sudan, Rais Arthur Peter
Mutharika wa Malawi, Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemanrian Desalegn na
Naibu Rais wa Kenya William Ruto. Viongozi hawa pamoja na wawakilishi
wao, wamedhamiria kufungua njia za kuwa na masoko huru ikiwa ni mkakati
kukabiliana na ukuzaji biashara na utanuaji wa teknolojia katika nchi za
Afrika hasa sasa ambapo nchi katika mabara mengine zimekwisha fikia
hatua hii, hali inayozineemesha huku Afrika ikibakia nyuma.
Hata
hivyo, wajumbe wengi wa Mkutano huu wanapokea jitihada ya Misri kurejea
kwa nguvu katika ukanda wa Afrika kuwa ni mpango maridhwa unaolenga
kuongeza nguvu kwa Afrika kwani nchi tajiri za Afrika zinaongezeka na
pia aina ya mahusiano inabadilika. Kubadilika huku kwa aina ya mahusiano
kunaonesha faraja kwa nchi ambazo hazijatanuka sana kiuchumi na
kiteknolojia na kwamba kutaongeza ushindani ndani ya Afrika pamoja na
bidhaa za Afrika kupata masoko makubwa ya ndani na nje.
Mheshimiwa
Makamu wa Rais yupo katika mkutano huu akiambatana na Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Kigoda. Mheshimiwa Makamu wa Rais
pamoja na msafara wake wanatarajia kurejea nyumbani kesho mara baada ya
mkutano huu kuisha jioni ya leo kwa sherehe rasmi ya kuweka saini
makubaliano ya utangamano wa utatu wa kanda hizi.
Imetolewa na: Ofisi ya Makamu wa Rais
Sharm el Sheikh, Misri
Jumatano Juni 10, 2015
No comments:
Post a Comment