Katibu
Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad, akiwahutubia wanachama na wapenzi
wa chama hicho kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kilombero jimbo la
Kitope.
Naibu
Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui akiwahutubia wanachama
na wapenzi wa chama hicho kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika
Kilombero jimbo la Kitope.
Baadhi
ya wanachama na wapenzi wa CUF waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika Kilombero jimbo la Kitope.(Picha na Salmin Said, OMKR)
Na: Hassan Hamad,OMKR
Katibu
Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad,
amewashukuru wanachama wa chama hicho katika Wilaya ya Kaskazini ‘B’ kwa
kujitokeza kwa wingi na kuwa wastahamilivu kwenye mkutano wa hadhara wa
CUF jimbo la Kitope, licha ya kuwepo kwa mvua kubwa.
Amesema kitendo hicho kinadhihirisha jinsi wanachama wa eneo hilo walivyokubali na kuamua kukiunga mkono chama hicho.
Akihutubia
mkutano wa hadhara wa CUF uliofanyika eneo la Kilombero jimbo la
Kitope, Maalim Seif amesema chama hicho kimekuwa kikipigania maslahi ya
Zanzibar, ili iweze kujikwamua kisiasa na kiuchumi.
Amefahamisha
kuwa katika jitihada za kuwakwamua wananchi kiuchumi chama hicho
kinakusudia kutekeleza kwa vitendo sera ya bandari huru, jambo ambalo
litaongeza ajira kwa vijana na hatimaye kunyanyua kipato cha wananchi.
Sambamba
na hilo, Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
amesema lengo la chama hicho ni kuhakikisha kuwa kinajenga mazingira na
miundombinu imara ili kuvutia wawekezaji katika sekta mbali mbali
zikiwemo utalii na uvuvi wa bahari kuu.
Katika
hatua nyengine Katibu Mkuu huyo wa CUF ameelezea kutoridhishwa na
kitendo cha jeshi la polisi nchini kuweka vikwazo vya kuwazuia wananchi
kutoka maeneo mengine kushiriki kwenye mikutano ya hadhara ya chama
hicho.
Amesema
CUF hakikushiriki katika kikao baina ya jeshi la polisi na vyama vya
siasa kilichofikia maamuzi hayo kutokana na kuweko kwenye mkutano muhimu
wa ndani wa chama hicho, na kwamba tamko hilo la jeshi la polisi
linakwenda kinyume na Katiba ya nchi.
Amelitaka
jeshi la polisi kutoa ufafanuzi juu ya sheria waliyotumia hadi kufikia
kutoa tamko hilo ambalo amesema linazuia uhuru wa watu kushiriki
shughuli za kisiasa.
Aidha
amelishauri jeshi hilo kuzingatia hali ya uchumi na mazingira ya
Zanzibar, kwani kitendo cha kuweka vizuizi barabarani kinaleta taswira
mbana kwa wageni na kinaweza kuathiri hali ya uchumi, ikizingatiwa kuwa
Zanzibar inategemea zaidi sekta ya utalii.
Naye
Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui amesema chama
hicho kinapinga kunyimwa uhuru wao wa kikatiba wa kuwazuia wananchi
kushiriki katika mikutano ya hadhara kutoka Wilaya moja kwenda nyengine.
Katika
risala ya wanachama wa CUF jimbo la Kitope iliyosomwa na bi. Fatma Seif
Said, wamesema wameamua kukiunga mkono chama hicho kutokana na mwelekeo
wake wa kutaka kuleta ukombozi wa kweli kwa wazanzibari.
Aidha
wameomba kujengewa tawi la kisasa katika eneo la Kilombero, ili iwe
kielelezo cha kukubalika kwa chama hicho katika eneo hilo.
Katika mkutano huo, jumla ya wanachama wapya 285 wamejiunga na chama hicho kutoka jimbo la Kitope.
No comments:
Post a Comment