Maisha :Ujumbe wa Vicky Ntetema kwa Rais Kikwete - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Thursday, 12 March 2015

Maisha :Ujumbe wa Vicky Ntetema kwa Rais Kikwete

10996517_845823052143916_6053821272163062755_o
Kilio kwa mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!
Mheshimiwa Rais Dakta Jakaya Kikwete,
Mheshimiwa Rais nakuja kwako kama mwanamke na mama mwenye watoto wenye albinism wanaowindwa kama wanyama na wakatili ili wachukue viungo vyao na kuwapelekea waganga wa kienyeji ambao wanavitumia kwa shughuli za kishirikina.
Leo umetuusia mengi mazuri kwenye maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika kitaifa huko Morogoro. Umeyaweka masuala yote vizuri sana katika jitihada zako za kututetea sisi wanawake wa taifa hili unaloliongoza! Nasema ahsante sana!
Mheshimiwa Rais, nasikitika kukufahamisha kwamba furaha ya leo imeingia shubiri na uchungu usio kipimo na wala hauelezeki. Wamemkata mkono mtoto wetu mwingine mwenye albinism mwenye umri wa miaka sita huko Rukwa. Mtoto wetu wa kiume anayeitwa Baraka Cosmas Rusambo ameachiwa maumivu makali na ulemavu wa kudumu wa viungo. Huyu kesho yake itakuwaje, Mheshimiwa Rais?
Mwanamke mwenzangu – mama mzazi wa Baraka, Prisca Shaaban amekatwakatwa mapanga akijaribu kumlinda mtoto wake asichukuliwe na kudhuriwa na majambazi.
Tunanyanyaswa, tunabaguliwa na tunanyanyapaliwa kwa kuzaa watoto wenye albinism. Kana kwamba hiyo haitoshi, bado tunaachwa na waume zetu kwa kuwa ati tumewaletea laana katika familia. Licha ya vitendo hivi vya kudhalilishwa bado tunashambuliwa na kujeruhiwa vibaya wakati tukiwalinda watoto wetu dhidi ya wauaji na majambazi hawa.
Mheshimiwa Rais wetu nakuomba uwawajibishe akina baba na waume zetu wanaowatelekeza watoto wao wenye albinism au wanaotuacha tupambane na majambazi na wao kukimbia badala ya kutulinda. Wachukulie hatua kali sana wale wanaume wetu wanaotuacha nyumbani peke yetu tukiwa na watoto wenye albinism huku wakijua dhahiri kwamba wakatili wanaweza kutuvamia na kutushambulia ili wawakate watoto wetu viungo.
RAI YA MTOTO KWA BABA YAKE
Nakuja kwako Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete kama mtoto wako wa taifa hili unaloliongoza. “Baaba nawachongea watu waovu waliomkata mkono ndugu yetu, Baraka Jumamosi usiku!
“Baaba! Machi 5, 2015 uliwakemea waovu hawa! Uliwaambia waache kabisa kuwafanyia ukatili watoto wako wenye albinism! Baaba! Majambazi hayo hayakusikilizi! Bado yanawasaka ndugu zetu na kuwakata viungo! Ati siku mbili tu baada yaw ewe kutamka kwamba unapanga mikakati ya kuwabaini wahalifu, waganga wa kienyeji na watumiaji wa viungo wao wakaenda Rukwa kumkata mkono Baraka. Baaaba, wahalifu hawa wamejiondoa ufahamu na wala hawana ubinadamu! Wajeuri, wakatili, wana kiburi!
“Baaba naomba uongeze nguvu ili majambazi hayo yapatikane na yafikishwe mahakamani. Yanatumalizia ndugu zetu na kutuharibia jina la taifa letu! Baaba! Ile adhabu iliyotolewa mahakani kwa wale wakatili waliokutwa na hatia hivi ulisema itatekelezwa lini, tena? Baaba! Pengine watu hawa wanaendelea na uovu huu kwa kuwa wenzao walohukumiwa bado wanajidai rumande. Pengine wanasema, “Mtatufanya nini, makamu kama haya?” Baaba! Pengine ndiyo maana haya mauaji na ukatili huu wa kuwateka nyara na kuwakata viungo ndugu zetu unaendelea!” Chanzo: MO BLOG

No comments:

Post a Comment