Dodoma. Serikali imeuchomoa muswada wa kuanzisha Mahakama ya Kadhi uliokuwa uwasilishwe bungeni ili yafanyike maridhiano kwanza.
Wakati Serikali ikichukua hatua hiyo, taasisi 11
za Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania zimeazimia kuwahamasisha wana
jumuiya wake kususia Kura ya Maoni ya Katiba Mpya hadi watakapopata
uhakika wa kuwa na Mahakama ya Kadhi yenye meno.
Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala iliyokutana
jana mjini Dodoma ilielezwa kuwa Serikali imeomba muda wa kufanya
maridhiano kabla ya kuwasilishwa muswada huo katika mkutano huu wa Bunge
unaomalizika kesho. Ilielezwa kuwa muswada huo utawasilishwa katika
mkutano ujao wa Bunge.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kamati hiyo
zinasema kuwa Bunge liliamua kuondoa muswada huo kujadiliwa pamoja na
sheria mbalimbali na badala yake ujadiliwe peke yake.
Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa
Muhambwe, Felix Mkosamali alisema katika kikao chao Mwenyekiti wa Kamati
hiyo, Jasson Rweikiza aliwaeleza kuwa Serikali imeomba hivyo ili
kufanya maridhiano na kuahidi kuwa itauwasilisha katika mkutano wa Bunge
ujao.
Taasisi zapinga
Kauli ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu zipatazo
11 iliyotolewa Dar es Salaam jana na kusomwa na Naibu Katibu wa Jumuiya
ya Shura ya Maimamu, Sheikh Rajabu Katimba ilisema itasusia mchakato wa
Kura ya Maoni kwa madai kuwa kinachoendelea katika mchakato wa
kupatikana kwa Mahakama hiyo ni hadaa za Serikali zinazofanyika miaka
yote hasa kinapofika kipindi cha kupiga kura kwa lengo la kuungwa mkono
na waumini hao.
Akizungumza kwa niaba ya jumuiya hizo zikiwamo,
Baraza Kuu, Tampro, Basuta, Jasuta, IPC, Haiyat Ulamaa na Shura ya
Maimamu Tanzania, Sheikh Katimba alisema watawahamasisha Waislamu
wanaounda Jumuiya hizo kutopiga kura ya maoni wala kushiriki kwa namna
yoyote ile katika mchakato wa kupatikana Katiba Mpya kwa sababu
haiitambui Mahakama hiyo.
Alisema mchakato wa kutoa maoni juu ya muswada
unaohusu Mahakama ya Kadhi umepotoshwa kwa kuituhumu kuwa italeta vurugu
ikiwamo kuhukumu kwa kukata watu mikono, kuhukumu wasiokuwa Waislamu na
kuwabagua wasiokuwa Waislamu na kwamba ni upotoshaji wa makusudi ukiwa
na lengo la hadaa.
“Wamefanya hivyo makusudi ili wananchi na Serikali
wasitilie maanani maoni yaliyotolewa na taasisi 11, ambayo kama
yatafanyiwa kazi na Serikali yatawezesha kupatikana kwa Mahakama ya
Kadhi inayokidhi matakwa ya Sheria za Kiislamu na wajibu wake kama
mamlaka ya kutoa na kutenda haki,” alisema Sheikh Katimba.
Hata hivyo, Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Issa
Shaaban Simba alisema Kamati ya kudumu ya Bunge ya Katiba Sheria na
Utawala ilipata maoni ya taasisi zote za Kiislamu na kila moja ilitoa
maoni ya nini kifanyike ili kuboresha muswada wa Mahakama ya Kadhi.
Alisema Bakwata iliungana na Serikali na
kukubaliana nini kitoke, kibaki, kiboreshwe na kusema taasisi hizo nazo
zilipaswa kutumia wakati huo kukubali, kukataa, kutoa mapendekezo,
kujadili.
Muswada huo ulitarajiwa kuzua mjadala mkali hasa baada ya Jukwaa
la Wakristo Tanzania kuitaka Serikali kuachana nao ili kuepusha kuvunja
misingi ya Taifa inayopinga ubaguzi na kutofungamana na dini yoyote.
Suala hilo lilikuwamo katika Muswada wa
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali uliotarajiwa kuwasilishwa bungeni wiki
hii na ulilenga kufanya mabadiliko katika Sheria ya Tamko ya Sheria za
Kiislamu Sura ya 375 ili suala hilo litambuliwe kisheria.
Endapo muswada huo ambao tayari umechambuliwa na
wadau ungepitishwa, kungefanyika marekebisho kwenye kifungu cha tatu
baada ya maneno ‘all courts’ (Mahakama zote) na kuongezwa maneno
‘including Kadhi Courts’ (Ikijumuishwa na Mahakama ya Kadhi).
Hata hivyo, Jukwaa la Wakristo linaloundwa na
Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC) na Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste nchini (CPCT), lilisema
mapendekezo hayo “yanaibua mambo mazito ya kikatiba ambayo hayawezi
kuamuliwa na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali na
sheria hiyo itawaathiri hata wenye imani tofauti.”
Imeandikwa na Kalunde Jamal, John Daudi na Boniface Meena. Mwananchi
No comments:
Post a Comment