Kaimu
Meneja Utawala Bw. Atanas William wa Kiwanda Cha Mafuta (Jielong
Holdings) akitoa maelezo kwa timu ya ukaguzi jinsi mafuta
yanavyofungashwa katika ndoo tayari kwa kwenda sokoni. Kiwanda hiki kina
uwezo wa kuzalisha lita za mafuta milioni 2.4 kwa mwezi.
Wakaguzi
wa Miradi kutoka Ofisi ya Raisi, Tume ya Mipango wakiwa na Kaimu Meneja
Utawala Bw. Atanas William wa Kiwanda Cha Mafuta (Jielong Holdings)
wakiangalia jinsi mitambo inavyomimina mafuta katika ndoo tayari kwa
kwenda sokoni.
Kaimu
Meneja Utawala Bw. Atanas William wa Kiwanda Cha Mafuta (Jielong
Holdings) akimwonyesha Bw. Paul Sangawe, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume
ya Mipango, shehena ya mbegu za pamba zinazotumika na kiwanda katika
usindikaji wa mafuta.
Afisa
fedha wa Kiwanda cha nguo Dahong Bw. Luke Li akiwaonyesha Bw. Erasmus
Masumbuko na Bi. Angela Shayo (wachumi kutoka Tume ya Mipango) ubora wa
nyuzi za pamba zinazotengenezwa na kiwanda chake.
Na Oyuke Phostine - Shinyanga
Serikali
imetoa wito kwa Ofisi za wakuu wa mikoa kuhamasisha uwekezaji katika
sekta ya viwanda kwenye mikoa yao ili kuweza kukuza uchumi wa mikoa
husika na taifa kwa ujumla.
Wito
huo umetolewa na Bw. Paul Sangawe, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya
Mipango, anayeshughulikia Biashara za Kimataifa wakati akiongoza timu ya
wataalam kutoka ofisi hiyo iliyokuwa ikifanya ukaguzi wa miradi ya
maendeleo inayotekelezwa na Serikali na sekta binafsi katika mikoa ya
Shinyanga, Mara, Simiyu, na Mwanza.
Bw.
Sangawe, alisema kuwa Wajibu wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi
kwa sekta binafsi kuwekeza. Alifafanua kuwa, moja ya vipaumbele katika
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao utekelezaji wake unaishia
2015/16, ni miundombinu ili kufungulia fursa za ukuaji wa uchumi.
Aidha,
Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano unaofuata kuanzia 2016/17 utalenga
katika kuendeleza viwanda. Hivyo, alitoa rai kwa viongozi katika ngazi
za mikoa kuratibu masuala ya uwekezaji hususan katika viwanda ikiwa ni
pamoja na kuhakikisha kuwa uwekezaji huo unawanufaisha wananchi wa
maeneo husika kwa kuongeza fursa za ajira na masoko ya bidhaa za kilimo.
“Uwepo
wa viwanda hivi unaonyesha mwenendo na mwelekeo mzuri wa taifa katika
kufungua fursa za maendeleo na kiuchumi kupitia sekta ya viwanda, hivyo
basi iwapo jitihada za kuhamasisha uwekezaji wa viwanda katika kila mkoa
zitatiliwa maanani ni dhahiri kuwa fursa za ajira zitaongezeka na kasi
ya ukuaji uchumi itaongezeka” alisema Bw. Sangawe.
Akizungumza
na timu hiyo ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo ilipotembelea na kukagua
kiwanda cha kusindika mafuta kwa kutumia alizeti na mbegu za pamba cha
Jielong Holdings Mkoani Shinyanga, Kaimu Meneja Utawala Bw. Atanas
William alisema kuwa mpaka sasa kiwanda hicho kinaweza kusindika na
kuhifadhi lita milioni 2.4 kwa mwezi.
“Kwa
sasa upatikanaji wa mali ghafi ni wakuridhisha kwa sababu bado
tunanunua alizeti kutoka kwa wakulima, na mbegu za pamba katika vinu vya
kuchambua pamba (Ginneries). Tuna mpango wa kuhamasisha na kuwafundisha
wakulima njia bora za kilimo na utunzaji wa mazao ili kujihakikishia
upatikanaji wa mali ghafi yenye ubora zaidi” alisema Bw. Atanas.
Viwanda
vingine vilivyotembelewa ni kiwanda cha Dahong kinachotengeneza nyuzi
za pamba na kiwanda cha Xinghua cha kusindika ngozi mkoani Shinyanga na
kiwanda cha nguo cha Mwatex Mkoani Mwanza. Kiwanda cha Dahong kina uwezo
wa kununua tani 12,000 za pamba kwa mwaka na kuzalisha tani 7 za nyuzi
za pamba kwa siku. Kiwanda hiki kimeanza uzalishaji mwezi Septemba 2014,
na nyuzi zote zinazozalishwa zitauzwa nchini China.
Kwa
mujibu wa bwana Luke Li, ambaye ni afisa fedha wa kiwanda hicho,
mipango ya baadae ya kiwanda hicho ni kutengeneza nguo. Bwana Li pia
alisema kuwa kuna mpango wa kujenga kinu cha kuchambua pamba na kutoa
mafunzo kwa wakulima ili kuwezesha upatikanaji wa pamba yenye ubora
unaotakiwa.
Kwa
upande wake, Meneja wa kiwanda cha Xinghua, Bw. Wang, alisema kuwa
usindikaji wa ngozi unasuasua kutokana na upatikanaji hafifu wa
malighafi. Wafugaji wanapowekea alama mifugo na kutoboa ngozi wakati wa
kuchinja, wanaathiri sana ubora wa ngozi alisema meneja huyo. Katika
kukabiliana na changamoto hii, mwekezaji huyo ana mpango wa kujenga
machinjio ya kisasa ambayo pia itahusisha usindikaji wa nyama.
Aidha
Bw. Sangawe alitoa rai kwa viongozi wa mikoa inayotoa ngozi kwa wingi
kuongeza jitihada za kutoa elimu kwa wafugaji kuhusu umuhimu wa ubora wa
ngozi ili kuhakikisha ngozi inayopatikana Tanzania inakuwa na thamani
ya hali ya juu.
No comments:
Post a Comment