.jpg)
Mkurugenzi
wa Serikali za Mitaa bwana Kharist Michael Luanda akitangaza idadi ya
watanzania waliojiandikisha kushiriki uchaguzi wa serikali za Mitaa
utakaofanyika jumapili ijayo.
Jumla
ya Watanzania 11,491,661 sawa na asilimia 62% ya watanzania 18,587,742
ambao walitarajiwa kujiandikisha kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa
utakaofanyika jumapili ijayo wamejiandikisha kushiriki uchaguzi huo.
Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za
Mikoa na Serikali Mitaa Bwana Kharist Michael Luanda aliwaambia
waandishi wa habari mjini Dodoma kuwa mikoa ambayo imeandikisha idadi
kubwa ya wapiga kura ni Katavi 79% na Kagera (78%) na mikoa ambayo
iliandikisha idadi ndogo ya wapiga kura ni Dar es salaam 43% na
Kilimanjaro 50% .
Aidha
alizitaja Halmashauri ambazo zimeandikisha idadi kubwa ya wapigakura
kuwa ni Halmashauri ya mji wa Mpanda 107% na Halmashauri mji wa Babati
101%. Halmashauri ambazo hazikufikia hata nusu ni Halmashauri ya Wilaya
ya Kilindi 21% na Halmashauri ya Wilaya ya Same 22%.
Alisema
kila Halmashauri imeandaa karatasi za kupigia kura ambazo zitakuwa na
Jina la mgombea, Jina la Chama, Nembo ya chama na nembo ya
Halmashauri,hivyo kila mpiga kura atatakiwa kuweka alama ya vyema katika
kisanduku kilicho chini ya Nembo ya chama kuonyesha kuwa amempigia kura
mgombea aliyetaka kumchagua.
Bwana
Luanda alisema kuwa vituo vya kupiga kura vitakuwa katika majengo ya
Umma isipo kuwa katika vituo vya Polisi, kanisani au msikitini na katika
vituo vya Afya. Aliongeza kuwa pale ambapo hakuna majengo ya Umma
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atashauriana na Vyama vya Siasa kuandaa
sehemu maalum ya kupigia kura.
Bwana
Luanda alisema vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi mpaka saa
10:00 jioni, wapiga kura watakaokuwepo kituoni saa 10:00 jioni
wataruhusiwa kupiga kura hadi watakapokuwa wamemaliza kupiga kura.
Mkurugenzi
huyo aliongeza kuwa wakati wa kupiga kura kabla Msimamizi Msaidizi wa
uchaguzi hajampa karatasi za kupiga kura atajiridhisha kama jina la
mpiga kura limeorodheshwa katika Orodha ya wapiga kura na baada ya
kuridhika atamtaka ajitambulishe kwa kutumia kitambulisho kimoja kati ya
Kitambulisho cha Mpiga kura cha Uchaguzi Mkuu, kazi, Hati ya kusafiria,
Kadi ya Benki, Kadi ya Bima ya Afya, Shule au Chuo, Leseni ya Udereva
na kitambulisho cha Uraia.
“Ikiwa
Mpiga Kura atakuwa hana kitambulisho cha aina yoyote kichotajwa katika
kanuni za Uchaguzi lakini jina lake limo kwenye orodha ya Wapiga Kura,
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi atamruhusu mtu huyo kupiga kura baada ya
kutambuliwa na wakazi wa eneo husika” alisema.
Bwana
Luanda ametoa rai kwa watanzania wote waliojiandikisha kupiga kura
wajitokeze kwa wingi siku ya juma pili kwenda kupiga kura. Pia ameviomba
Vyama vya Siasa na viongozi wa Asasi zisizo za Kiserikali kuhamasisha
wapiga kura kujitokeza kwa wingi kuchagua Viongozi wao.
Aidha
Mkurugenzi huyo wa TAMISEMI aliwaonya wananchi kutopiga kura zaidi ya
mara moja au kutaka kupiga kura endapo hawakujiandikisha kushiriki
uchaguzi huo kwani ni kosa la jinai na hatua kali za kisheria
zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakaye jaribu kukiuka Sheria, Kanuni na
Taratibu za Uchaguzi.
No comments:
Post a Comment