Na Saidi Mkabakuli, Sumbawanga
Serikali
imeazimia kuanza kuiboresha bandari ya kimkakati ya Kasanga
inayohudumia nchi za Burundi, Rwanda na Kongo iliyopo katika Ziwa
Tanganyika, mkoani Rukwa.
Ahadi
hiyo imetolewa na Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo
kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri wakati
walipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya miundombinu katika Bandari ya
Kasanga.
Bibi
Mwanri alisema kuwa serikali kupitia Mamlaka ya Bandari Tanzania
imepanga kuboresha bandari zote ili kuwa malango kuu la biashara kwa
soko la ndani na kwa nchi jirani ili kuongeza uwezo wa kuhudumia shehena
kwa ufanisi.
“Tumedhamiria
kuendelea kuboresha miundombinu ya bandari hususan miradi iliyoibuliwa
katika Programu ya Matokeo Makubwa Sasa ikiwemo Bandari ya Kasanga ili
kuweza kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma katika eneo hili,” alisema.
Bibi
Mwanri aliongeza kuwa serikali pia imejipanga kuendelea kuboresha
miundombinu na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya kuhudumia shehena katika
bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Kasanga na Kigoma na
kukamilisha maandalizi ya ujenzi wa bandari mpya za Mwambani (Tanga),
Mbegani (Bagamoyo) na Bandari Kavu ya Kisarawe.
Akizungumza
na ugeni huo, Msimamizi Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli
Thompson Mwamafupa alisema kuwa Bandari hiyo ina fursa nyingi katika
kuhudumia shehena na abiria wanaopitia bandarini hapo.
“Bandari
yetu ina fursa kubwa za kibiashara kwani tuna wateja wengi kutoka ndani
na nje ya nchi wanaotumia bandari yetu kupitishia bidhaa zao, pamoja na
abiria wanaosafiri kwenda nje na ndani ya Tanzania,” alisema.
Kwa
mujibu wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka ujao wa fedha Serikali
imedhamiria kuboresha mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kuwekeza
katika kujenga miuondombinu na kuboresha usafirishaji wa mizigo katika
bandari zote nchini.
Pia, Mpango huo unaweka bayana kuendeleza na ukarabati na ununuzi wa vyombo vya usafiri na usafirishaji katika maziwa.
Kiongozi
wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya
Mipango, Bibi Florence Mwanri (Watatu kushoto) akimsikiliza kwa makini
Mkuu wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kulia) mara
walipowasili katika bandari hiyo kujionea shughuli mbalimbali za
maendeleo bandari hapo.
Mkuu
wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto)
akiwaongoza wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume
ya Mipango kujionea moja ya meli za kigeni zinazotia nanga katika
bandari hiyo. Meli hiyo ni MV Rwegura kutoka nchini Burundi.
Mkuu
wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto)
akiongea na wakaguzi wa miradi ya maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume
ya Mipango kuhusu namna ya kuhudumia meli kutoka nje ya nchi.
Mkuu
wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kulia) akitoa
ufafanuzi juu ya namna bandari yake inavyohudumia meli kutoka nchi
jirani. Wanaomsikiliza ni Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka
Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango ikiongozwa na Bibi Florence Mwanri
(Kushoto aliyevaa fulana nyeusi).
Mkuu
wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kulia)
akiwaonesha maghala ya kuhifadhia mizigo katika Bandari ya Kasanga.
Maghala hayo yalifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed
Gharib Bilali tarehe 22 Februari 2012.
Timu
ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
ikiwa katika picha ya pamoja katika Ofisi za Mamlaka ya Mapato nchini
(TRA) zilizopo kwenye Bandari ya Kasanga.
Timu
ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango
ikiwa katika picha ya pamoja katika jiwe la msingi la uzinduzi wa
maghala ya kuhifadhia mizigo katika Bandari ya Kasanga. Maghala hayo
yalifunguliwa rasmi na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilali
tarehe 22 Februari 2012.
Mkuu
wa Bandari ya Kasanga, Bw. Mponjoli Thompson Mwamafupa (Kushoto)
akimfafanualia jambo Kiongozi wa Timu ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo
kutoka Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango, Bibi Florence Mwanri (Kulia)
wakati akimkabidhi taarifa ya maendeleo ya bandari hiyo.
No comments:
Post a Comment