Naibu
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo kikuu
cha Kiislamu Morogoro Nd.Kassimu N’gwali akitoa neno la shukrani kwa
waalikwa wa hafla yao ya kuagana kwa wanajumiya wanaomaliza masomo yao
mwezi Septemba mwaka huu wa 2014. Kushoto ni Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae ndie mgeni rasmi wa hafla hiyo Mama Asha Suleiman Iddi.
Baadhi
ya wana jumuiya ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha
Kiislamu Morogoro wakifuatilia hafla ya maagano kwa wanajumiya
wanaotarajiwa kumaliza mafunzo yao mwezi Septemba mwaka huu.
Mwanajumiya
ya ZAMUMSA Saleh Haji alitaja baadhi ya changa moto wanazopakabiliana
nazo wakati akisoma Risala ya jumiya hiyo katika hafla iliyofanyika
kwenye ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi Kikwajuni Mjini
Zanzibar.
Mwenyekiti
wa ZAMUMSA Bibi Saada akimkabidhi zawadi Mke wa Makamu wa Pili wa Rais
wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi kwenye hafla ya kuagana wanajumiiya
hiyo wanaomaliza masomo yao mwezi Septemba mwaka huu.
Mama
Asha Suleiman Iddi akizungumza na Wana Jumuiya ya ZAMUMSA kwenye ukumbi
wa zamani wa Baraza la Wawakilishi uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Mama
Asha akimkabidhi Cheti Maalum Mwenyekiti mstaafu wa ZAMUMSA Nd. Rashid
Mjaka kwa niaba ya viongozi wenzake baada ya kumaliza muda wao wa
utumishi wa jumuiya hiyo. Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
**********************************
Mke
wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema
kwamba utitiri wa vyuo vikuu bila ya ubora wa elimu inayotolewa ni jambo
linalopelekea vyuo hivyo kutoa vijana wasiouzika kiajira katika taasisi
mbali mbali za umma na hata zile za binafsi.
Alisema
athari hiyo ambayo pia ni hatari kwa hatma yao ya kimaisha hapo baadaye
pia inaweza kuwanyima fursa pana nay a uhakika ya kujiunga na vyuo
vyengine vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi.
Mama
Asha Suleiman Iddi alisema hayo wakati wa hafla maalum ya kuagana kwa
wana jumuiya ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu
Morogoro wa ZAMUMSA ambao wanatarajiwa kumaliza mafunzo yao mwezi
Novemba mwaka huu.
Hafla
hiyo ya aina yake iliyoshirikisha pia baadhi ya wahitimu wengine wa
vyuo vikuu mbali mbali Nchini Tanzania ilifanyika katika ukumbi wa
Zamani wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliopo Kikwajuni Mjini
Zanzibar.
Mama
Asha alisema vyuo vikuu viliopo hapa nchini hivi sasa vinatosha,
lakini kinachohitajika zaidi ni kuimarishwa kwa ubora wa elimu
inayotolewa kwenye vyuo hivyo.
Aliwataka
wasomi wa vyuo vikuu wanaomaliza masomo yao kuweka malengo maalum ya
kujiendeleza kimaisha ili kuwa tayari kukabiliana na changamoto
watakazokuja pambana nazo katika maisha yao ya baadaye.
Alisema
Zanzibar ni ndogo kulingana na wimbi la vijana wanaomaliza elimu ya
vyuo vikuu. Hivyo akasema ni vyema wakajiandalia mazingira ya kujiunga
katika vikundi vya uzalishaji ndani na nje ya vyuo ili kuwa tayari
katika kukabiliana na matatizo ya kimaisha wamalizapo masomo yao.
Mama
Asha alifahamisha kwamba jumuiya ya ZAMUMSA inafaa kufanya miradi ya
kisomi kwa kutengeneza vitini na kuwauzia wanafunzi wa sekondari na pale
inapowezekana hata kutunga vitabu vya sekondari katika masomo mbali
mbali.
Katika
kuunga mkono jumuiya hiyo ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo kikuu
cha Kiislamu Mkoani Morogoro Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar Mama Asha aliahidi kuipatia mchango wa Kompyuta, Printa na
Mashine ya Fotokopi Jumuiya hiyo ili ipate nguvu zaidi za kiutendaji.
Hata
hivyo Mama Asha aliwaasa na kuwatahadharisha wanafunzi hao wa elimu ya
juu kujiepusha na ushawishi wa wanasiasa kwa kuwatumia kujiingiza katika
matendo maovu ya uvunjifu wa amani ya Nchi.
Alisema
wasomi mara nyingi ndio wanaotumiwa katika kufanya fujo na kuvuruga
amani katika maeneo mbali mbali duniani kupitia mkono wa Viongozi wa
kisiasa.
Akigusia
suala la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu kulazimishwa kusomea fani
wasiyoitaka, mama Asha alisema suala hilo bado linazungumzika bila ya
kuleta utata au hofu yoyote ile.
Alitoa
wazo kwa wana jumuiya hiyo pamoja na wasomi wengine kukutana na
Uongozi wa juu wa Wizara inayoshughulikia Taaluma katika kutafuta njia
muwafaka ya kulitatua tatizo hilo kwa njia sahihi isiyo na shaka.
Akisoma
risala ya wanajumuiya hiyo ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma Chuo
Kikuu cha Kiislamu Mkoani Morogoro { ZAMUMSA } Mwanajumuiya Saleh Haji
alisema lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo mwaka 2006 ni kuwaunganisha
pamoja wanafunzi wote ili kuwa rahisi kukabiliana na changamoto
wanazopambana nazo.
Saleh
Haji kwa niaba ya wanajumiya wenzake wameiomba Serikali Kuu kuongeza
nguvu za ziada katika uimarishaji wa maabara na Maktaba kwa skuli za
Sekondari ili kuzalisha wanafunzi wa sayansi ambao hivi sasa bado idadi
yao hailingani na mahitaji halisi ya upatikanaji wa wataalamu wa fani
hiyo.
Aidha
wanafunzi hao wa ZAMUMSA wameiomba Serikali kufanya juhudi ya
kuwadhibiti wasomi wanaomaliza elimu ya juu kwa kuwajengea mazingira
mazuri yatakayowapa hamu ya kuitumikia elimu yao hapa nyumbani.
Mapema
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha
Kiislamu Morogoro Hamad Ali alisema wanajumiya hao wameamua kujitolea
kuitumikia nchi yao licha ya changamoto wanazopambana nazo.
Hamad Ali alisema wanafunzi hao wanahitaji kuitumia taaluma waliyojifunza kwa kuisaidia jamii iliyowazunguuka katika maeneo yao.
Wanafunzi
wasiopungua mia 800 kutoka Zanzibar wamejiunga na chuo kikuu cha
Kiislamu Morogoro katika fani mbali mbali ikiwa ni zaidi ya asilimia 47%
ya wanafunzi wote chuoni hapo.
Idadi
hiyo ni kubwa ikilinganishwa na vyuo vyengine vikuu hapa Tanzania
inayotokana na mazingira halizi ya chuo hicho yanayolingana na utamaduni
na silka za wanafunzi hao.
No comments:
Post a Comment