CLOUDS FM RADIO YATOZWA FAINI : TCRA YAITOZA FAINI MILIONI 4 CLOUDS ENTERTAINMENT FM RADIO KWA KUKIUKA KANUNI ZA UTANGAZAJI - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633

Saturday, 23 August 2014

CLOUDS FM RADIO YATOZWA FAINI : TCRA YAITOZA FAINI MILIONI 4 CLOUDS ENTERTAINMENT FM RADIO KWA KUKIUKA KANUNI ZA UTANGAZAJI

Mtangazaji wa Kipindi cha Redio cha Njia Panda kinachorushwa na Clouds FM Dkt. Isack Maro. Kipindi cha NJIA PANDA ndicho kilichokiuka kanuni za utangazaji na kupelekea TCRA kuwatoza faini ya shilingi milioni 4 ya Kitanzania.Picha na Michuzi Blog


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
KATIKA KAMATI YA MAUDHUI YA MAMLAKA YA MAWASILIANO TANZANIA
DAR ES SALAAM

SHAURI LA UKIUKAJI WA KANUNI ZA UTANGAZAJI
NAMBA 4/2014

DHIDI YA
CLOUDS ENTERTAINMENT FM RADIO
UAMUZI
UAMUZI WA KAMATI YA MAUDHUI KUHUSU LALAMIKO LA UKIUKAJI WA KANUNI ZA UTANGAZAJI, MWAKA 2005
1.0 Utangulizi:
Tarehe 15/06/2014, kituo cha Clouds Entertainment FM Radio cha Dar es Salaam kilikiuka Kanuni za Utangazaji (Maudhui) za mwaka 2005, kupitia kipindi chake cha Njia Panda kilichorushwa hewani kati ya saa 8.00 mchana na saa 10.00 jioni. Kipindi hiki kilikuwa na mada iliyohusu Safari ya Kuzimu. Maudhui ya kipindi hiki yalijaa simulizi za kufikirika, za kishirikina na kichawi.
2.0 Maelezo ya kosa
2.1 Kurusha kipindi chenye simulizi za kishirikina na kichawi
Kituo cha Clouds Entertainment FM kilitangaza kipindi ambacho kimejaa simulizi za kufikirika, kishirikina na kichawi ambazo zinaweza kujenga Imani potofu za kichawi kwa wananchi na jamii iliyokuwa inasikiliza kipindi hiki.
2.2 Kutokuwasilisha ratiba za vipindi kwa mujibu wa Sheria
Kituo cha Clouds Entertainment FM hakikufuata Kanuni za Utangazaji (Maudhui) za mwaka 2005 zinazowataka kuwasilisha ratiba ya vipindi vyao kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ili viidhinishwe na vilevile kuvichapisha katika gazeti kabla ya kurushwa hewani. Kipindi cha Njia Panda hakikuwasilishwa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa ajili ya kuidhinishwa. Hii ni kinyume na Kanuni Na. 22(1),(3),(a),(b).
3.0 Kanuni zilizokiukwa
3.1 Kosa la Kwanza
Kituo cha Clouds Entertainment FM Radio kimekiuka Kanuni zifuatazo za Huduma ya Utangazaji (Maudhui) 2005: Na. 5(a), (b), (c), (d), (f), (g), (h), 14(1) na 15(b)
5. Every licensee shall ensure that the programme and its presentation:-
(a) upholds national sovereignty, national unity, national interest, national security and Tanzanian’s economic interests;
(b) projects Tanzanian national values and national points of view;
(c) observes good taste and decency;
(d) upholds public morality;
(f) does not injure the reputation of individuals;
(g) protects children from negative influences;
(h) does not incite or perpetuate harted against or vilify, any group or persons .............
Tafsiri ya Kanuni hizi kwa mujibu wa Kamati katika shauri hili ni kama ifuatavyo:-
5. Kila mwenye leseni ya utoaji huduma za utangazaji lazima ahakikishe kuwa vipindi vyake vinazingatia:-
(a) mshikamano wa kitaifa, umoja na maslahi ya Taifa, usalama wa Taifa, na kulinda manufaa ya uchumi wa Tanzania;
(b) kulinda maadili ya Mtanzania na Taifa;
(c ) ubora wa kipindi pamoja na staha;
(d) kuzingatia maadili ya umma;
(f) kutoharibu /kuchafua sifa za watu;
(g) kuwalinda na kuwaepusha watoto kuiga tabia hasi;
(h) havileti uchochezi wala kujenga chuki kwa mtu au kundi la watu …………………
14(1) Every licensee shall have particular regard to the need to protect children from unsuitable programme material;
15(b) Every free-to air licensee shall refrain from using language meant to mislead or unnecessarily cause alarm and despondency;
Tafsiri ya Kanuni hizi kwa mujibu wa Kamati katika shauri hili ni kama ifuatavyo:-
14(1) Kila mwenye leseni anatakiwa azingatie umuhimu wa kuwalinda watoto na vipindi visivyofaa;
15(b) Kila mwenye leseni ya utangazaji wa vipindi vya Radio na Televisheni vinavyosikilizwa au kutazamwa bila malipo anatakiwa kutotumia lugha ya upotoshaji au inayoweza kusababisha hofu na kukatisha tamaa.
3.2 Kosa la Pili
Kituo cha Clouds Entertainment FM Radio kimekiuka Kanuni zifuatazo za Huduma ya Utangazaji (Maudhui) 2005: Na. 22(1),(3),(a),(b):-
22(1) A licensee shall publish programme schedule in a daily newspaper circulating widely in Tanzania at least one month in advance.
(3) a licensee shall submit to the Authority: –
(a) advance quarterly programme schedule fourteen days before each quarter;
(b) transmission reports detailing programmes actually broadcast within seven days after the end of each calendar month.
Tafsiri ya Kanuni hizi kwa mujibu wa Kamati katika shauri hili ni kama ifuatavyo:-
22(1) Mwenye leseni anapaswa kuchapisha ratiba ya vipindi vyake katika gazeti linalochapishwa kila siku na kusomwa na sehemu kubwa ya nchi ya Tanzania angalau mwezi mmoja kabla ya vipindi kusikika hewani.
(3) Mwenye leseni anapaswa kuwasilisha kwa Mamlaka :-
(a) ratiba ya vipindi vyake vya robo mwaka siku kumi na nne kabla ya robo mwaka inayotarajia kuanza;
(b) kutoa taarifa za kina za vipindi halisi vinavyotangazwa ndani ya siku saba kabla ya mwisho wa kalenda kila mwezi.
4.0 Ushahidi wa Makosa
4.1 Kusikiliza CD ya kipindi cha “Njia Panda”
Ili kujiridhisha kama maudhui ya kipindi cha Njia Panda na uwasilishaji wake ulikiuka Kanuni za Utangazaji, Kamati na uongozi wa Clouds Entertainment FM Radio walisikiliza sehemu ya kipindi hicho. Maudhui ya kipindi hicho yalionyesha wazi ukiukwaji wa Kanuni za Utangazaji.
5.0 Maelezo ya utetezi
5.1 Maelezo ya Dkt. Isaac Maro
Mtangazaji wa kipindi cha Njia Panda DKt. Isaac Maro, alianza kutoa utetezi wake kwamba kipindi cha Njia Panda kina miaka kumi na tatu tokea kuanzishwa na hapo mwanzo kilikuwa kinajulikana kama APEX na kilianzishwa kwa lengo la kuangalia mambo yanayohusiana na HIV. Kilipoanzishwa, kilikuwa kinazungumzia mambo matatu ya kufanya ili kujikinga na HIV ambayo ni Kuacha, Kuwa mwaminifu na Kutumia Kondomu.
Dkt. Isaac Maro aliendelea kutoa utetezi wake kwamba baadae tafiti zilionesha kuwa ukizungumzia Ukimwi kwa kuangalia hayo mambo matatu tu ni sawa na kuangalia tatizo kutoka kwenye matawi na hivyo badala ya kuangalia kiini cha tatizo na kikaanzishwa kipengele kinachoitwa Nini Chanzo yaani “Root Causes”.
Kipindi kilipanuka na kuanza kuangalia changamoto ambazo kijana anapitia na kuzungumzia umasikini, elimu, imani potofu, dini na maisha ya kawaida ya Mtanzania. Kwa bahati mbaya sana waandaaji wa kipindi ni madaktari na jinsi walivyokuwa wanaenda kwenye chanzo walikuwa wanakutana na watu ambao walikuwa wanasema walipata ukimwi kwa sababu ya kulogwa na moja ya maeneo yenye changamoto ni imani potofu. Hivyo walianza kutumia watu kuelezea imani potofu, na jinsi gani zinasaidia kuchochea maambukizi.
Dkt. Maro alisistiza kwamba haya ni matukio ambayo yalitokea miaka mingi iliyopita na waliangalia kutafuta stori ambayo itapelekea watu kuamini kwamba mambo yale yaliyotokea ambayo watu walikuwa wakiyaamini yalikuwa siyo ya kweli na hayapo. Mila hizi potofu mwisho wa siku zitasababisha mgonjwa asiende hospitali.
5.2 Maelezo ya Bwana Ruge Mutahaba
Mkurugenzi wa vipindi wa Clouds Entertainment FM Bwana Ruge Mutahaba alitoa utetezi wake kwa kusema changamoto kubwa inayokikabili kituo chake ni kutafuta ubunifu wa kuwafikia walengwa ambao ni vijana. Bwana Ruge alisema maneno yafuatayo:-
“…..ukisikiliza kipindi cha Njia Panda siku zote kimekuwa kinazungumza kuhusu…. an individual person…. na story yake na namna alivyokutana na jambo lililogeuza maisha yake na jambo hilo mwisho wa siku lilivyo muathiri kuelekea kupata maambukizi….”
Bwana Ruge aliendelea kusema kwamba kituo chake kilianzisha kampeni ya Vunja Ukimya ambayo ilikuwa na lengo la kuzungumzia HIV kwa uwazi na kuleta vijana wengi ambao walijitangaza kuathirika na ugonjwa wa Ukimwi ilikuisaidia jamii. Alisema kipindi kilicholalamikiwa kilihitimishwa kwa kuelezea mambo yanayohusu uchawi na ushirikina hayana msaada wowote.
Bwana Ruge alisisitiza kwamba kipindi kiliruka kwa wiki tatu. Mhusika alianza kuzungumzia maisha yake ya kawaida, akaenda kwenye sehemu ya pili ya kuingia kwenye misukule na akaenda kwenye sehemu ya tatu akazungumza kwamba hata ile ajali na matukio yaliyotokea ilikuwa ni ajali ya kawaida kama nyingine zinavyotokea na kwamba yeye hana nguvu hiyo na hayo mambo siyo ya kweli.
Bwana Ruge alisema huyu aliyekuwa anasimulia ni mtu mpumbavu yaani “ Stupid” na aliyoyasema yalikuwa siyo ya kweli. Alisema maneno yafuatayo:
“ ……hakuna aliyesema wale walikufa kwa kulogwa….tunachozungumza ni kwamba there is a stupid guy alikuja kusema amehusika na hii kitu….this guy is a stupid guy lakini mwisho wa siku inakuja kujulikana ni uongo……”
Bwana Ruge alisema waliamua kuweka masimulizi hayo kwa sababu watu wanaamini vitu ambavyo havipo kwenye jamii.
6.0 Kukiri Kosa
Mkurugenzi wa Clouds Entertainment FM Bwana Ruge Mutahaba alisema kwamba hawakufanya kosa lolote na hitimisho la kipindi katika wiki ya tatu lilieleza kwamba mambo yaliyosemwa ni ya uongo na hakuna kitu kama hicho.
7.0 Tathmini ya Kamati
Kamati iliridhika na kusisitiza kwamba, kituo cha Clouds Entertainment FM Radio katika kipindi cha Njia Panda kilikiuka Kanuni za Utangazaji kwa kutangaza maudhui yenye simulizi za kishirikina na kichawi jambo ambalo ni kinyume na taratibu na Sheria za nchi.
Habari na simulizi za Safari ya Kuzimu zinaweza kupelekea kuipotosha jamii na ni kinyume na utamaduni wa Taifa. Jambo hili linaweza kumomonyoa utaifa wa Watanzania, vilevile linaweza kuumiza hisia za wananchi wa Tanzania na kusababisha mvurugano miongoni mwa wananchi, pamoja na kuhatarisha usalama wa taifa. Kitendo hiki ni kinyume na Kanuni za Utangazaji (Maudhui).
Vilevile, lugha iliyotumika kuendesha kipindi hicho ilikuwa ni ya moja kwa moja isiyopunguza ukali wa maneno badala ya kutumia “tafsida”. Lugha iliyotumika ni lugha inayoweza kuwajengea hofu wasikilizaji, na inaweza kuwajengea watoto tabia mbaya na kuwapotosha kutokana na kusikia mambo yasiyofaa. Jambo hili ni kinyume na Kanuni za Utangazaji (Maudhui),2005,
8.0 Uamuzi wa Kamati
Kamati iliridhika kuwa kipindi cha “Njia Panda” kilichorushwa hewani na kituo cha Clouds Entertainment FM Radio tarehe 15/06/2014 kilikiuka Kanuni za Utangazaji, 2005 Na. Na. 5(a), (b), (c), (d), (f), (g), (h), 14(1), 15(b) na 22(1),(3),(a),(b):- kama ilivyonukuliwa hapo juu.
Baada ya kusikiliza na kutafakari kwa kina maelezo ya utetezi kutoka kwa Mkurugenzi wa Vipindi wa Clouds Entertainment FM Radio na Mtangazaji wa kipindi cha “Njia Panda”, Kamati ya Maudhui inaamua yafuatayo:-
1.1 Clouds Entertainment FM Radio inapewa onyo kali; na,
1.2 Clouds Entertainment FM Radio inatozwa faini ya shilingi milioni nne za Kitanzania ambazo inapaswa kuzilipa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ndani ya mwezi mmoja toka siku ya uamuzi huu.
Endapo Clouds Entertainment FM Radio itakiuka tena Kanuni za Utangazaji, hatua kali zaidi za Kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Uamuzi huu umetolewa na kusomwa Dar es Salaam siku hii ya ……., Mwezi wa Agosti Mwaka 2014.
Haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huu iko wazi ndani ya siku 30 tangu uamuzi unapotolewa
Uamuzi Umesainiwa na:
Eng. Margaret T. Munyagi
………………………………......
(Sahihi)
Mwenyekiti
WAJUMBE WA KAMATI YA MAUDHUI
1. Bwana Walter Bgoya (Sahihi).......................................
2. Bwana Joseph Mapunda (Sahihi).................................
3. Bwana Abdul Ramadhani Ngarawa (Sahihi)…………………

No comments:

Post a Comment