SHIRIKA
la Maendeleo la Taifa (NDC) limeanza mchakato wa kupata wazabuni kwa
ajili ya ujenzi wa viwanda vya uzalishaji magadi soda kwenye Ziwa Natron
na Bonde la Engaruka.
Viwanda hivyo vitajengwa umbali wa zaidi ya kilometa 10 kutoka kwenye
ziwa yatakapochimbwa magadi ambapo wanatarajia kuzalisha tani za ujazo
milioni 1.5 kwa mwaka, huku thamani yake kwa bei ya soko ikiwa zaidi ya
sh bilioni 720.
Kiwanda kitakachojengwa Ziwa Natron, ndicho kitaanza kutekelezwa
ambapo kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwanzoni mwa 2015 na utafiti
pekee umegharimu sh bilioni 2.5.
Akizungumza juzi jijini hapa, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NDC, Mlingi
Mkucha, alisema kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kukamilika kwa
utafiti wa kina wa mazingira ambao pamoja na mambo mengine umethibitisha
kuwa hakuna madhara yoyote kwa mazalia ya korongo wadogo (Lesser
Flamingo) wanaoishi kwenye maeneo hayo kama ilivyokuwa ikihofiwa na
wanamazingira.
Mkucha alisema kuwa watafiti hao walijikita katika kuangalia namna
uzalishaji wa magadi soda utakavyoweza kufanyika bila kuathiri mazingira
kwenye maji, hasa mchanganyiko wa maji na kemikali usiharibike, ubaki
kama ulivyo sasa.
Kwamba korongo wadogo wanaozaliana na kuishi kwenye Ziwa Natron
waliwachunguza maisha yao hatua kwa hatua kwa kipindi cha mwaka na kuona
hakuna madhara yoyote yatakayowapata.
Alisema kuwa kulingana na ujazo wa magadi soda yaliyopo kwenye maeneo
ya Ziwa Natron na bonde la Engaruka, yanaweza kuvunwa kwa miaka 540
bila kuisha, huku akisema kuwa muda huo utaongezeka kwani kila mwaka
magadi hayo huongezeka mita za ujazo bilioni 1.9.
Mkucha aliongeza kuwa tayari mchakato wa kuandaa mpango bora wa ardhi
kwenye maeneo hayo umeanza ili kuainisha maeneo kwa ajili ya ujenzi wa
makazi ya watu, viwanda, biashara na huku wakala wa barabara nchini
(Tanroads) akitakiwa kuangalia barabara zinazoelekea maeneo ya mradi
pamoja na njia za reli.
“Tumekuja kushauriana na viongozi wa wilaya za Monduli na Longido
pamoja na mkoa ili miradi hii ifanyike kwa muda tuliojiwekea, baada ya
muda mfupi mtaanza kuona mabadiliko makubwa, kutakuwa na ajira za moja
kwa moja si chini ya 1,000.
“Viwanda hivi vya magadi vitavuta viwanda vingine kujengwa kwenye
maeneo haya kwa ajili ya kutumia magadi kama malighafi, ndiyo sababu
katika utengaji wa maeneo kutatengwa maeneo ya viwanda, watu wa mabenki
nao watakuja, migahawa, wote hawa watatoa ajira,” alisema Mkucha.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli lilipo Ziwa Natron, Jowika Kasunga, alisema
kuwa wananchi wameshirikishwa kiasi cha kutosha, na kwamba baada ya
matokeo ya utafiti watawaeleza watu namna watakavyonufaika na mradi huo.
Mkuu wa Wilaya ya Longido lilipo bonde la Engaruka, James ole Millya,
alisema kuwa hana taarifa za wananchi kuupinga mradi huo, huku
akisisitiza kwamba wananchi wa Kitongoji cha Oasis wanaoishi kandokando
ya bonde hilo wako tayari mradi huo uanze mara moja.
Chanzo:Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment