Na Anna Nkinda – Maelezo
Taasisi
ya Fursa ya Elimu (Opportunity Education Foundation) ya nchini
Marekani imetoa mchango wa dola za kimarekani laki moja kwa ajili ya
udhamini wa wanafunzi wa kike ambao ni yatima na wanaotoka katika
mazingira hatarishi katika shule ya Sekondari ya WAMA-Nakayama iliyopo
wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Fedha
hizo ambazo ni zaidi ya shilingi milioni mia moja na sitini na mbili
zitaweza kuwasomesha wanafunzi 75 kwa kipindi cha mwaka mzima kwa
kuwapatia malazi, chakula, sare za shule, viatu, shajara, vitabu na
mahitaji mengine ya kila siku ya mwanafunzi.
Hayo
yamesemwa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete ambaye ni Mwenyekiti
wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ambao ndiyo wamiliki wa shule
hiyo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mradi wa laptop ndogo (tablets
computer) uliofanyika shuleni hapo jana.
Mama
Kikwete pia alimpongeza Joe Ricketts ambaye ni mwanzilishi na mtendaji
mkuu wa Fursa ya Elimu kwa moyo wa upendo alionao na dhamira ya
kuisaidia jamii ya watanzania kwa kutambua kwamba kupata elimu bora kwa
wanafunzi wote ni ufunguo wa kuwa na afya bora, uchumi imara,
miundombinu bora na ya kutosha, jamii yenye uelewa jambo ambalo
litasababisha ustadi wa taifa kunasonga mbele.
Mwenyekiti
huyo wa WAMA alisema , “Kwa mantiki hiyo ningependa kusema kwamba
kukosekana kwa fursa ya kumpatia mtoto wa kike elimu bora ni kulikosesha
taifa fursa ya maendeleo kwani kadri mtoto wa kike anavyopata elimu
ndivyo anavyoweza kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi na ataweza
kuboresha uzazi wa mpango, afya ya mtoto na kujiongezea kipato”.
Akizungumzia
kuhusu mradi wa laptop ndogo (tablets) ambapo shule hiyo ilipata
61 Mama Kikwete aliiomba Taasisi hiyo na wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi kuangalia uwezekano wa kuongeza mitaala ya mafunzo ya kitanzania
ili iwasaidie wanafunzi kumudu masomo wanayofundishwa darasani
halikadhalika kuandaa mkakati wa kuzifikia shule zilizopo pembezoni
ambazo zinakuwa na uhaba wa walimu.
“Ninawaasa
walimu na wanafunzi wa shule hii na kupitia wanafunzi wa shule
zitakazofaidika na mpango huu kutumia vifaa hivi kwa mahitaji ya masomo
kama ilivyokusudiwa na siyo kupoteza muda kwa michezo isiyo na manufaa.
Napenda mjione kama watu wenye bahati ambao mmepata fursa ya kipekee
ambayo wanafunzi wengi nchini hawana, mvitunze vifaa hivi ili viwafae
wanafunzi wengine watakaokuja baada yenu”, alisisistiza Mama Kikwete.
Kwa
upande wake Ricketts alisema kwa mara ya kwanza alikuja nchini mwaka
2006 wakati anaelekea Serengeti alikuta mwalimu mmoja anafundisha
wanafunzi zaidi ya miamoja aliamua kuanzisha mahusiano na shule hiyo
ambayo aliwapelekea vifaa mbalimbali vya kufundishia.
Alisema
lengo la kuanzishwa kwa Taasisi yake ni kutoa msaada wa kielimu ikiwa
na nia ya kufanya upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi kutoka nchi
zinazoendelea ili wale wanaotoka katika familia maskini waweze kusoma na
kupata ajira pale watakapokuwa wamemaliza masomo yao na hivyo
kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
“Vijana
wadogo wanategemea kupata elimu bora kwa kuwa elimu kwa wanafunzi
imegawanyika katika sehemu mbili ambazo ni technolojia na mwanafunzi
mwenyewe kukuwa na kukomaa kiakili ili aweze kufanya vizuri katika
masomo yake.
Kama
mradi huu utafanikiwa walimu watakuwa na mwamko mkubwa wa kufundisha na
nitahakikisha kuwa zinapatikana laptop ndogo (tablets) za kutosha kwa
ajili ya kusomea nchini kwani matokeo ya maisha ya watoto wetu
yanategemea elimu wanayoipata” , alisema Ricketts.
Taasisi
ya Fursa ya Elimu ilianzishwa mwaka 2005 na kusajiliwa nchini mwaka
2006 walianza kufanya kazi na shule moja ya msingi na hadi kufikia
sasa shule 434 zikiwemo za Sekondari 33 zimenufaika kwa kupata vitabu,
DVD na zana za kufundishia.
Kwa
shule za sekondari wanatoa mwongozo wa mwalimu ambao unamuongoza
kirahisi jinsi ya kuwafundisha wanafunzi , laptop ambazo zinamasomo
yaliyorekodiwa ambayo ni ya sayansi, hesabu, kiingereza na maarifa ya
jamii ,projecta na Televisheni ambazo zinasaidia kuonyesha masomo na
vitabu na video inawasaidia wanafunzi kujifunza somo la kiingereza kwa
njia ya kusikiliza na kusoma.
Wanafunzi
watakaonufaika na program hiyo ni wa kidato cha pili kutoka shule za
Sekondari Ilboru,(Arusha) Mzumbe (Morogoro), Msalato,
(Dodoma),FidelCastro (Pemba), WAMA - Nakayama (Pwani), shule ya
Sekondari ya wavulana Bwiru (Mwanza), J Ossian (Bukoba), Laureatte
(Zanzibar), Notredame (Arusha) na Tusiime (Dar es Salaam).
No comments:
Post a Comment