Dar es Salaam. Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Edward Lowassa amesema juhudi anazofanya Rais
Jakaya Kikwete katika kuinua sekta ya michezo nchini bado mafanikio yake
hayaridhishi.
Kutokana na hali hiyo, Lowassa ameitaka Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuchukua hatua za makusudi ili
kuhakikisha tija inapatikana kwenye sekta hiyo ya michezo na
kuwanufaisha vijana.
Lowassa alisema hayo katika hafla fupi ya kumuaga Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia.
Hafla hiyo iliandaliwa na kamati hiyo ya mambo ya
nje na ilifanyika kwenye Ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam,
ambapo Nkamia alikuwa ni miongoni mwa wajumbe wa kamati hiyo kabla ya
kuchaguliwa kuwa Naibu Waziri.
“Rais Kikwete atakumbukwa kwa jitihada zake
alizofanya katika kuwekeza kwenye michezo, lakini bado hakuna mafanikio
yaliyotarajiwa, Jamali Malinzi alikuja kwangu nina imani ana nia ya
kuendeleza soka,” alisema Lowassa.
Aliongeza,“ Ingawa watu wengine walihoji ujio wake
kwangu, lakini mimi naona mwelekeo wa maendeleo chini ya uongozi wake,
naomba wizara yako iwe karibu na vyombo vinavyosimamia michezo,”
alisisitiza Lowassa.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo, Suzan Lyimo alisema
suala la michezo bado liko nyuma sana hususan upande wa wanawake hivyo
akamwomba Nkamia kuhakikisha anatafuta mbinu mbadala za kuzisaidia timu
za taifa.
Kwa upande wake, Nkamia alisema amekutana na
viongozi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) kwa lengo la kuzungumza ni
jinsi gani timu za taifa zitaweza kusaidiwa kwa njia zozote zile.
“Tukitegemea wadhamini hatuwezi kufika, kwani nao
wadhamini wanaangalia maeneo ambayo yatawalipa hivyo sisi wenyewe lazima
tuangalie ni njia zipi zinaweza kusaidia timu zetu zote za taifa,”
alisema Nkamia. Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment