Biashara : Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni aipongeza Puma Energy kurahisisha upatikanaji huduma za nishati kwa wananchi - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Wednesday 9 October 2024

Biashara : Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni aipongeza Puma Energy kurahisisha upatikanaji huduma za nishati kwa wananchi


• Mkuu wa Wilaya ashiriki uzinduzi wa kituo kipya cha mafuta pamoja na huduma za ziada kama vile duka la manunuzi ya mahitaji ya nyumbani, huduma za kuosha na matengenezo ya magari.

• Pia, apokea msaada wa mitungi ya gesi safi ya kupikia ya Puma Gas inayosambazwa na kampuni hiyo ili kuwanufaisha akina mama wanaojishughulisha na biashara ndogondogo za uuzaji wa chakula.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mheshimiwa Halima Bulembo ameipongeza Puma Energy Tanzania kwa jitihada zake za kuendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma na bidhaa za nishati kwa Watanzania kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Aliyasema hayo wakati aliposhiriki katika uzinduzi rasmi wa kituo kipya cha mafuta na huduma za ziada cha kampuni hiyo katika eneo la Dege Mtaa, Kata ya Somangila, Halmashauri ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

“Tanzania inashuhudia mapinduzi makubwa ya ukuaji wa uchumi wake na ili kuwawezesha wananchi wote kunufaika, ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi ni muhimu. Miongoni mwa sekta inayochochea ukuaji huu ni ya nishati, ambayo ni msingi katika uendeshaji wa shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Hivyo, kadri wananchi wanavyosogezewa huduma za nishati karibu hurahisisha upatikanaji wake na kuokoa gharama za kusafiri umbali mrefu,” alisema Mheshimiwa Bulembo.

Kituo kipya cha mafuta ambacho kinapatikana Dege Mtaa kitakuwa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo ya jirani katika urahisishaji wa huduma za mafuta na bidhaa za vilainishi. Lakini pia kutakuwepo na huduma za ziada ambazo zitawarahisishia Watanzania wengi kufanya manunuzi ya mahitaji yao yote katika eneo moja kama vile duka la mahitaji mbalimbali ya nyumbani pamoja na kuwezeshwa kupata huduma za kununua na kujaza mitungi ya gesi ya kupikia kwa gharama nafuu.

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni ameipongeza Puma Energy Tanzania kwa dhamira yake ya kuendelea kusambaza huduma zake ili kuwafikia wananchi popote walipo, “jukumu la serikali ni kujenga miundombinu na kushirikiana na wadau kutoka sekta tofauti ili kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na maisha bora. 

Nawapongeza Puma Energy Tanzania kwa kuwa mshirika wa karibu wa serikali katika maendeleo ya sekta ya nishati nchini,” aliongezea na kuhitimisha, “Ushirika huu unaendelea kuwanufaisha Watanzania kutokana kuwahakikishia upatikanaji wa huduma na bidhaa za nishati wa uhakika na gharama nafuu. Kama serikali, tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa kuwahikikishia mazingira mazuri ya biashara ili muendelee kusambaza huduma zenu maeneo ya vijijini ambapo bado hawajafikiwa. 

Kwa niaba ya wakazi wa Kigamboni, tunawashukuru pia kwa msaada wa mitungi ya gesi ambayo itawanufaisha akina mama wanaojishughulisha na biashara ndogondogo ya uuzaji wa chakula ikiwa ni sehemu ya mkakati wenu mliojiwekea kuzisaidia jamii za Kitanzania ili kuchochea shughuli za maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini kote.”

Naye kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Abdallah ameelezea kuwa uzinduzi wa kituo hiki sehemu ya mkakati wa kampuni kuendelea kuiwezesha jamii ya Watanzania na kuwahudumia wateja wake kwa ubunifu na weledi wa hali ya juu katika maeneo mbalimbali nchini.

“Dhamira yetu kuu ni kuendelea kuiwezesha jamii ya Watanzania pamoja na kuwahakikishia wateja wanapata huduma na bidhaa bora za nishati kwa gharama nafuu na kwa viwango vya hali ya juu. Hivyo, kama sehemu ya shamrashamra za Wiki ya Huduma kwa wateja sisi tumeona ni vema kufanya kwa vitendo kwa kuwasogezea huduma karibu zaidi. 

Uzinduzi wa kituo hiki kipya cha mafuta hautakuwa unatoa huduma za ujazaji wa mafuta pekee bali kutakuwa na huduma za ziada kama vile uoshaji wa magari, ufundi, mitungi ya gesi safi ya kupikia, vilainishi, pamoja na duka lenye mahitaji mbalimbali kwa matumizi ya nyumbani,” alifafanua Bi. Abdallah.

Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania alimalizia kwa kuwasihi wakazi wa DegeMtaa kukitumia vema kituo hiko kipya ili kurahisisha shughuli za maisha yao ya kila siku,

“nawasihi wananchi wa Kigamboni kutumia fursa zitokanazo na uwepo wa kituo hiki kipya karibu na makazi yenu. Tunaishukuru serikali kwa ushirikiano endelevu na kututengenezea mazingira mazuri ya biashara ambayo yanatuwezesha kuendelea kusambaza na kuboresha huduma zetu. Kituo hiki kitakuwa kinatoa huduma masaa 24 kila siku kwa siku zote za wiki ili kuhakikisha watu hawakwami katika shughuli zao za kijamii na kiuchumi.”

Mbali na kuzindua kituo kipya cha mafuta na huduma za ziada, Puma Energy Tanzania

ilikabidhi msaada wa mitungi 200 ya Puma Gas. Msaada huo uliokabidhiwa kwa Mkuu wa Wilaya unalenga kuwanufaisha wanawake wanaojihusisha na biashara ndogondogo za uuzaji wa chakula ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kampuni kuiwezesha jamii ya Watanzania nchini kote.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mheshimiwa Halima Bulembo (katikati) akikata utepe kuashiria ufunguzi wa kituo cha mafuta cha Puma Energy Tanzania na huduma za ziada katika eneo la Dege Mtaa, Kata ya Somangila, jijini Dar es Salaam. Akishirika pamoja naye kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bi. Fatma Abdallah pamoja na Meneja Mauzo ya Rejareja (kulia), Bw. Sulpis Mmasi.


Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mheshimiwa Halima Bulembo akipokea msaada wa mitungi 200 ya gesi safi ya kupikia ya Puma Gas kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Abdallah ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini kote. Tukio hili lilifanyika wakati wa uzinduzi wa kituo cha mafuta cha Puma Energy Tanzania na huduma za ziada katika eneo la Dege Mtaa, Kata ya Somangila, jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Mheshimiwa Halima Bulembo (katikati) akijaza mafuta gari kuashiria ufunguzi wa kituo cha mafuta cha Puma Energy Tanzania na huduma za ziada katika eneo la Dege Mtaa, Kata ya Somangila, jijini Dar es Salaam. Akishirika pamoja naye kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bi. Fatma Abdallah pamoja na Meneja Mauzo ya Rejareja (kulia), Bw. Sulpis Mmasi.

No comments:

Post a Comment