Teknolojia : Shule Soft na Selcom Wazindua Mfumo wa Kulipa Ada kwa Namba Maalum - Wazalendo 25 Blog

Glory to Story.

Habari Mpya

PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0784 643 633


PRINTING / GRAPHICS / DESIGN : 0676 643 633

Tuesday 8 October 2024

Teknolojia : Shule Soft na Selcom Wazindua Mfumo wa Kulipa Ada kwa Namba Maalum

KAMPUNI ya Shule Soft, kwa kushirikiana na Selcom Tanzania, imezindua mfumo mpya wa ulipaji ada ambao unatumia namba maalum ili kuwatambua wanafunzi waliolipiwa ada.


Mfumo huu unalenga kutatua changamoto zinazotokana na ukosefu wa risiti na taarifa za malipo, ambazo mara nyingi zinapelekea wanafunzi kurudishwa nyumbani na kushindwa kufanya mitihani.

Akizungumza katika hafla hiyo leo Oktoba 8,2024 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Shule Soft, Ephraim Swilla, amesema mfumo huo, unatoa nafasi kwa wazazi au walezi kulipa ada kwa kutumia benki au mtandao wowote wa simu, kulingana na mazingira yake na fedha hiyo itaingia moja kwa moja kwenye mfumo wa shule.

“Mfumo huu ni maalum kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya fedha kutoonekana kwenye mifumo na matokeo yake wazazi kuendelea kudaiwa, tumekuja na suluhisho hili, ambalo litasaidia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji ada na kuondoa malalamiko kwani itamtambua ni mwanafunzi yupi amelipa,” amesema Swilla.

Aidha amesema kuwa mfumo huo mpya hauna makato yeyote na utazinufaisha shule zaidi ya 450 zilizoko mikoa mbalimbali nchini, ambazo ni za msingi, sekondari na vyuo vya kati.

Amesema mfumo huo umeunganishwa kati ya mtoa huduma na mteja, kwa shule watapata ujumbe mfumo wa maneno( sms) pamoja na barua pepe, aliongeza kuwa kampuni inahudumia zaidi shule binafsi huku za serikali zikiwa ni saba tu.

Nae Mkuu wa biashara kutoka Kampuni ya Shule Shule Soft, Elisha Tengeni, amesema ulipaji wa kidigitali unasaidia kubaini waliolipa ada katika muda uliopangwa, aliomba shule kujiunga na mfumo huo ili kuepuka malalamiko na upotevu wa fedha kwenye baadhi ya mifumo.

Kwa upande wake Mkuu wa Masoko wa Selcom, Shumbana Walwa, amesema mifumo mingi ya ulipaji ada ina matatizo, ikiwemo fedha kutoonekana kwenye mfumo.

Amesema mfumo huo utasaidia kuhakikisha malipo yanapatikana kwa urahisi, hivyo kuwapa wanafunzi fursa ya kusoma kwa utulivu.

"Wazazi wanaweza kulipa ada kupitia benki au mitandao ya simu, na fedha zitakuwa na ufuatiliaji mzuri kwenye mfumo wa shule". Amesema






No comments:

Post a Comment