Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni,Sanaa na Michezo. Mhe Mohamed Mchengerwa amewataka viongozi wa vyama na mashirikisho ya michezo nchini kutotumia taasisi wanazoziongoza kujinufaisha kwa vipato tu na badala yake wawe wabunifu na wazalendo ili kuleta mapinduzi kwenye michezo na kuendana na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan ya kutumia michezo kuleta uchumi kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Mei 27, 2022 wakati akifunga kikao kazi cha viongozi wa vyama na mashirikisho ya michezo nchini kilichoratibiwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kufuatia maelekezo yake aliyoyatoa wakati akiisimika Bodi ya BMT hivi karibuni ya kutaka kuwa na utawala bora kwenye vyama na mashirikisho ya michezo ili kuendeleza michezo.
Mhe. Mchengerwa amefafanua kuwa yapo mataifa mbalimbali duniani ambayo hayana miundombinu ya michezo na yana idadi ndogo ya watu ukilinganisha na Tanzania lakini yamekuwa yakifanya vizuri kwenye michezo hivyo amewataka kubadili fikra potofu ili wanaowaongoza waige mifano kutoka kwao hatimaye kuleta mapinduzi makubwa kwenye michezo.
“Hatutaweza kupiga hatua kwenye michezo kama sisi viongozi hatutaweza kubadilika na kuendelea kuwa na fikra potofu ya kudhani vyama na mashirikisho ni mahali pa kujipatia vipato tu. Nawaomba tubadilike mimi katika kipindi changu sitaweza kuruhusu kutokea hayo. Mpango wa matumauni ya kesho lazima tuanze kujenga leo”. ameongeza Mhe. Mchengerwa.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imeelekeza nguvu kubwa kuendeleza sekta za utamaduni, Sanaa na Michezo ndiyo maana iliunda upya Wizara hii ili iweze kujitegemea, kuongeza bajeti, kutoa punguzo kwenye nyasi bandia ili kuimarisha viwanja vya soka pamoja na kuanzisha mfuko wa maendeleo ya michezo.
Ameongeza kuwa mfuko huo umepewa chanzo madhubuti ambacho ni fedha za asilimia tano ya mapato yatokanayo na michezo ya kubashiri matokeo ya michezo.
Kikao hicho pamoja na mambo mengine kimejadili kwa kina vigezo vya muongozo wa kusaidia timu za taifa kwa kutumia fedha za mfuko wa maendeleo ya michezo na kuja na mawazo ambayo yatafanyiwa kazi na serikali ili kuwa na uwazi katika usaidiaji wa timu hizo katika michezo mbalimbali.
Aidha, amewasihi viongozi hao kufuata miongozo na taratibu za nchi sambamba na kuziheshimu mamlaka na taasisi zinazosimamia michezo nchini, kuimarisha utawala bora na weledi katika kazi.
Mambo mengine ni pamoja na kuimarisha eneo la utaalamu na taswira za taasisi zao kwa kuwa na mikakati yenye dira.
Ameeleza kuwa Serikali itaendelea kujenga miundombinu mipya na ya kisasa ya michezo ambapo kwa upande wake Naibu Waziri, Mhe, Pauline Gekul amewataka wadau washirikiane na kupendana ili kuongoza kwa mafanikio.
Naye Katibu Mkuu. Dkt, Hassan Abbasi amewataka viongozi hao kuwa wabunifu wa kutafuta vyanzo mbalimbali vya mapato badala ya kutegemea Serikali pekee.
No comments:
Post a Comment