Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina(mwenye miwani) akikagua moja kati ya pikipiki kumi kabla ya kuzikabidhi ili zitumike kwenye minada ya mipakani na upili.Picha na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (mwenye miwani) akikata utepe kwenye moja kati ya pikipiki kumi kabla ya kuzikabidhi ili zitumike kwenye minada ya mipakani na upili.Picha na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhaga Mpina (mwenye miwani) akienesha moja kati ya pikipiki kumi baada ya kuzikabidhi ili zitumike kwenye minada ya mipakani na upili.Picha na John Mapepele
Asema zitasaidia kukomesha utoroshaji wa mifugo nje ya nchi
Na John Mapepele
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina ameagiza maeneo yote ya minada ya awali na upili yapimwe na kuwekwa alama za mipaka katika mwaka wa fedha 2018/19 ili kuepuka uvamizi unaofanywa na watumiaji wengine wa ardhi.
Maelekezo hayo ameyatoa leo kwenye hafla ya iliyofanyika kwenye Ofisi ya Dar es Salaam wakati akikabidhi pikipiki kumi ili zitumike kwenye mipaka na minada ya upili kwa lengo la kudhibiti utoroshaji wa mifugo na mazao yake nje ya nchi.
Alisema Serikali inakusudia kuifunga minada yote iliyoanzishwa kiholela kwa nia ovu ambapo amesema kuendelea kubaki kwa minada hiyo kunadhoofisha minada ambayo imeanzishwa kwa kufuata taratibu za Serikali.
Aidha, Waziri Mpina alisema kuanzia sasa minada yote itaboreshwa na kuwa katika mfumo wa kielektroniki ili kudhibiti mapato ya Serikali kwa njia za kisasa zaidi.
“Kuanzia sasa wizara yangu inaingia kwenye mfumo mpya katika kusimamia minada yote ambapo utaiunganisha kwenye mfumo wa kielektroniki” alisisitiza Mpina
Sambamba na hatua hiyo Mpina amemwagiza Katibu Mkuu anayeshughulikia Sekta ya mifugo Dkt. Mary Mashingo kuhakikisha miundo mbinu ya minada yote inakarabatiwa mara moja na ili kuboresha usimamizi wa sekta ya mifugo nchini.
Alisema Wizara inasimamia minada 12 ya upili na 10 ya mipakani ambapo minada ya upili ipo nchi nzima kwa kuzingatia wingi wa mifugo katika eneo husika.
Mpina alisema hapa nchini kuna minada 465 ya awali ambayo huendeshwa na Mamlaka za Serikali za Mitaa (MSM). Aidha, minada ya mipakani imewekwa kuzingatia njia za kusafirishia mifugo kwenda nje ya nchi.
Alitaja minada ya upili na Wilaya ilipo kuwa ni Pugu (Ilala), Kizota (Dodoma), Sekenke (Iramba), Igunga (Igunga), Ipuli (Tabora) na Mhunze (Kishapu). Mingine ni Nyamatala (Misungwi), Meserani (Monduli), Themi (Arumeru), Weruweru (Hai), Korogwe (Korogwe) na Lumecha (Songea). Aidha, minada ya mipakani ni pamoja na Buhigwe (Kasulu), Kasesya (Kalambo), Kileo (Mwanga), Kirumi (Butiama), Longido (Longido) na Waso (Ngorongoro).
Minada mingine ni Mpemba (Momba), Kakonko (Kakonko), Mtukula (Misenyi) na Rusumo (Ngara). Minada itakayokabidhiwa pikipiki hizi ni Muhunze, Sekenke, Ipuli, Korogwe, Weruweru, Lumecha, Kasesya, Murusagamba, Buhigwe na Kirumi.
Aliongeza kuwa lengo la kuwepo kwa minada ya mifugo katika maeneo mbalimbali nchini ni kutoa fursa kwa wafugaji na wafanyabishara ya mifugo kuuza mifugo yao kwa faida zaidi kwa kuzingatia ushindani wa soko.
Naye katibu Mkuu Dkt. Mashingo alimshukuru Waziri kwa kuzindua matumizi ya pikipiki hizo na kuahidi kwamba pikipiki hizo zitaleta ufanisi katika utendaji kazi wa minada hapa nchini.
Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na ng’ombe millioni 30.5, Mbuzi millioni 18.8, na Kondoo millioni 5.7. Aidha, Katika mwaka 2017/18 jumla ya ng’ombe 1,614,321, Mbuzi 1,340,222 na Kondoo 315,636 wenye thamani ya shilingi trillioni 1.1 waliuzwa katika Minada mbalimbali hapa nchini.
Dkt Mashingo alisema kutokana na mifugo hii jumla ya tani 679,962 za nyama zimezalishwa ambapo jumla ya tani 1,248.4 za nyama ya mbuzi, tani 1,030.79 za nyama ya ng’ombe, tani 50 za nyama ya kondoo na tani 280 za nyama punda zenye jumla ya thamani ya dola za kimarekani billioni 5.7 ziliuzwa katika nchi mbalimbali.
Alisema matumizi ya minada yanawezesha ukusanyaji wa ushuru na tozo mbalimbali kutokana na biashara ya mifugo hivyo kuchangia katika pato la Taifa na kuiwezesha Serikali kutekeleza majukumu yake. Uwepo wa minada, hususani ya mipakani unasaidia katika kudhibiti biashara ya magendo hasa utoroshaji wa mifugo kwenda nje ya nchi.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Masoko na Huduma za uzalishaji wa Mifugo, Asimwe Lovince alisema makusanyo ya ushuru na tozo toka minada ya upili na mipakani kwa mwaka 2016/17 yalikuwa 4,775,682,750 ambapo mwaka 2017/18 ni 10,151,124,000 sawa na asilimia 129 ya lengo la makusanyo ya 7,871,000,000/= lililokuwa limepangwa kukusanywa mwaka 2017/18. Hata hivyo kutokana na uzoefu wa zoezi la doria ya Operesheni Nzagamba linaloendelea, imedhihirika kuwa kuna upotevu mkubwa wa makusanyo ya maduhuli ya Serikali.
“Tunafahamu kuwa Minada yetu imekuwa na changamoto kadhaa zikiwemo za ukosefu na uchakavu wa miundombinu, wataalamu wachache, ukosefu wa vitendea kazi ikiwemo vyombo vya usafiri, ukosefu wa fedha za kuendeshea minada na maeneo ya minada kuvamiwa na wananchi mfano Pugu mnada wenye hekta 1900 hivi sasa zimebaki hekta 108 tu. Wizara ina dhamira ya kuhakikisha kuwa changamoto hizi zinatatuliwa ili kuhakikisha kuwa minada inafanya kazi kwa ufanisi. Katika kulitekeleza hilo Wizara imenunua vyombo hivi vya usafiri ili kuongeza ufanisi wa kazi katika minada. Vyombo hivi pamoja na mambo mengine vitasaidia kufuatilia watu wanaokwepa ushuru kwa kuuza mifugo nje ya minada hivyo kuongeza ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali.” Asisitiza Dkt. Mashingo
Alisema Pikipiki hizi aina ya Honda XL 125 toka Japan zilinunuliwa na Wizara kupitia Wakala wa Serikali wa Manunuzi (GPSA) kwa thamani ya Sh 83,000,000/= sawa na Sh 8,300,000/= kila moja.
No comments:
Post a Comment