Utalii : Serikali Kuendesha Mnada wa Meno ya Viboko Januari 29 Jijini Dar es Salaam. - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


23 Jan 2018

Utalii : Serikali Kuendesha Mnada wa Meno ya Viboko Januari 29 Jijini Dar es Salaam.





Mnada huo utafanyika katika Jengo hili la Mpingo (Mpingo House) ambalo awali lilikuwa Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii kabla ya kuhamia Makao Makuu ya Nchi mjini Dodoma.


Na Hamza Temba - WMU- Dodoma


.................................................






*Wanunuzi wataruhusiwa kuyakagua (Januari 25 na 26) kabla ya mnada






*Watakaovuruga mnada kukiona cha mtemakuni






SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) itafanya mnada wa hadhara wa meno ya viboko vipande 12,467 vyenye uzito wa kilo 3,580.29.






Mnada huo utakaosimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango umepangwa kufanyika tarehe 29 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi katika Jengo la Mpingo, Barabara ya Nyerere Jijini Dar es Salaam, zilipokuwa ofisi za Wizara ya Maliasili na Utalii (Ivory Room).






Kupitia taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Dk. James Wakibara amesema mnada huo utawahusisha wafanyabiashara wa Nyara waliopewa leseni ya Nyara Daraja la Kwanza mwaka 2017.






Amesema wafanyabiashara hao wataruhusiwa kukagua meno hayo kati ya tarehe 25 na 26 Januari, 2018 kuanzia saa nne asubuhi hadi saa tisa na nusu jioni kabla ya siku ya mnada huo.






Aidha, amesema wanunuzi watakaoshinda mnada huo watatakiwa kulipa asilimia 25 ya malipo yote papo hapo na asilimia 75 itakayosalia itatakiwa kulipwa ndani ya siku kumi na nne zijazo baada ya mnada huo.






“Mtu yeyote atakayekuwa ametamka bei ya juu, kisha akashindwa kulipa asilimia 25 ya bei aliyotamka, atachukuliwa kuwa ni mwenye kutaka kuvuruga mnada na hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake,” ameonya Mkurugenzi huyo.






Amesema meno hayo yatauzwa kwa wastani wa uzito wa nusu kilo bila kugawanywa au kuchambuliwa wakati wa mnada na wanunuzi wataruhusiwa kuondoa bidhaa kwenye eneo la mnada baada ya kulipia ada na kodi husika kikamilifu na kupewa hati ya kumiliki nyara hizo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Dk. James Wakibara (kulia) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (kushoto) wakati wa hafla ya kufunga mafunzo ya 15 ya Jeshi Usu kwa kwa Maafisa wa Wanyamapori 87 wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania– TAWA, Shirika la Hifadhi za Taifa – TANAPA na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro hivi karibuni Mkoani Katavi. Katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Rachel Kasanda.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad