Matukio : Waziri ,Mpina Afuta Tozo zote za Mifugo Zisizozingatia Sheria - Wazalendo 25 Blog

Habari Mpya

Glory to Story.


Post Top Ad


11 Dec 2017

Matukio : Waziri ,Mpina Afuta Tozo zote za Mifugo Zisizozingatia Sheria



Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akisoma stakabadhi ya malipo ya sh 50,000 kwa kila ng’ombe kinyume cha sheria aliyotozwa mfugaji wa Kijiji cha Handa, Tulway Bombo ambapo Waziri Mpina alitangaza kufuta maamuzi hayo na kuamuru wafugaji hao kurudishiwa fedha zao.

Na John Mapepele


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amefuta tozo ya faini ya shilingi elfu hamsini kwa kila Ng’ombe mmoja na ameuagiza Uongozi wa Wilaya ya Singida kuwarudishia mara moja fedha wafugaji wote walizotozwa faini kinyume cha Sheria katika zoezi la kukamata mifugo linaloendelea katika Hifadhi ya Msitu wa Jamii wa Mgori.


Waziri Mpina ametoa maelekezo hayo leo alipotembelea eneo la Hifadhi ya Msitu wa Jamii wa Mgori, kwenye Kijiji cha Handa na kuwaagiza Wakuu wa Mikoa ya Singida na Dodoma kupitia kwa Wakuu wa Wilaya ya Singida na Chemba kushirikiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo anayeshughulikia Sekta ya Mifugo, Dkt. Mary Mashingo kufika katika eneo hilo kabla ya tarehe15/12/2017 kushughulikia mipaka baina eneo la Singida na Handa kwa upande wa Wilaya ya Chemba na migogoro ya wafugaji inayoendelea.


“Kama Waziri mwenye dhamana ya kushughulikia Sekta ya Mifugo na Uvuvi nchini sipo tayari kuvunja Sheria kwa kuwakumbatia wahalifu wanaokiuka Sheria za nchi kwenye Sekta ya Mifugo na Uvuvi, lakini pia wahalifu wanatakiwa kutozwa faini kulingana na Sheria na taratibu zilizowekwa. Utozaji wa faini ambao hauzingatii hili ni uvunjaji wa Sheria “ alisisitiza Mpina.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Handa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma baada ya kufika kijijini hapo kisha kuamuru wafugaji waliokamatiwa mifugo yao na kutozwa faini ya sh 50,000 kila ng’ombe warudishiwe kiasi cha sh. 30,000 kutokana na faini hiyo kutozwa kinyume cha sheria.


Waziri Mpina alisema utozaji wa faini wa shilingi 50,000/= toka shilingi 20,000/= za awali kwa kila Ng’ombe aliyekamatwa na shilingi 25,000/= kwa Mbuzi toka shilingi 5,000/= za awali haukubaliki na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Singida, Elias Tarimo kurudisha shilingi 30,000/= kwa kila Ng’ombe ambazo zimetozwa bila kufuata Sheria yoyote.


Baadhi ya wafugaji waliofika katika kijiji cha Handa kulalamikia tozo ya shilingi 50,000 kwa kila Ng’ombe mmoja walizotozwa na Halimashauri ya Wilaya ya Singida ni pamoja na Jerumani Waline aliyetozwa jumla ya shilingi 2,500,000/=, kwa idadi ya mifugo 66, Mabula Mwala aliyetozwa shilingi 1,950,000/= kwa idadi ya mifugo 45, Joel Tahan aliyetozwa jumla ya shilingi 1,000,000/= kwa idadi ya mifugo 31, Elizabeth Hamisi aliyetozwa shilingi 1,050,000/= kwa idadi ya mifugo 34,na Elizabethi Nyambi aliyetozwa jumla ya shilingi 350,000/= kwa idadi ya mifugo 8.


Akizungumza kwa niaba ya wafugaji bwana Jerumani Waline, amesema changamoto kubwa kwa sasa ni kuainishwa kwa mipaka ya Kijiji cha Handa na Hifadhi ya Msitu wa jamii wa Mgori na eneo la kunyeshea maji mifugo ambapo alimuomba Waziri kulishughulikia suala hilo. Waziri Mpina ameiagiza Halmashauri ya Singida kupitia mara moja tozo hizo na kuzipeleka kwenye Mamlaka husika ili zipitishwe na kuanza kutumika kwa taratibu zinazokubalika kisheria.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akimsikiliza kwa makini Mkazi wa Kijiji cha Handa wilayani Chemba, Jumanne Sadick kuhusu tatizo la mpaka kati ya Pori la Hifadhi ya Swagaswaga na Mgori ambapo Waziri Mpina aliagiza ifikapo Disemba 15 mwaka huu Katibu Mkuu Mifugo na viongozi wa Mkoa wa Singida na Dodoma kufika eneo hilo ili kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.


Pia amezitaka Halimashauri zote nchini kutojiingiza katika mtego wa kutoza faini ambazo hazipo kisheria kwa kuwa kufanya hivyo ni kuvunja sheria na kuagiza kuwa kuanzia sasa Halimashauri zote zinatakiwa kutoa taarifa kwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi pindi zinapotaka kuendesha operesheni za mifugo ili kuwa na ufahamu wa pamoja baina ya Wizara na wadau wengine hali ambayo itasaidia kuboresha operesheni hizo na kuondoa migongano isiyo ya lazima.


Aidha amewataka Watendaji kuwa makini wanaposhughulikia masuala ya mifugo kwa kuhusisha Sheria mbalimbali za Sekta ya Mifugo ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima kwa vyombo vya Serikali na kutolea mfano wa Uongozi wa Pori la Akiba la Swaga Swaga ulivyowazuia Wakaguzi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuangalia afya za mifugo iliyokamatwa katika pori hilo, akasisitiza kuwa ni ukiukwaji wa sheria kwa kuwa sheria namba 17 ya Magonjwa ya Wanyama ya mwaka 2003, kipengele 26 (a)1 kinawapa uwezo Wakaguzi kuingia na kuchunguza hali ya mifugo mahali popote ili kuona afya za mifugo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akimuuliza maswali Mwanasheria wa Halmashauri ya Singida, Fortunata Matinde juu ya sheria gani iliyotumika kutoza faini ya Sh. 50,000 kwa kila ng’ombe ambapo Waziri Mpina alifuta maamuzi hayo (kushoto) ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Mifugo) Dk Maria Mashingo.


Alizitaja baadhi ya Sheria za Mifugo ambazo ni muhimu kuzizingatia wakati wa operesheni za mifugo kuwa ni pamoja na Sheria ya Veternari Namba 16 ya Mwaka 2003, Sheria ya Tasnia ya Maziwa Namba 8 ya Mwaka 2004, Sheria ya Tasnia ya Nyama Namba 10 ya Mwaka 2006, Sheria ya Biashara ya Ngozi (The Hides, Skin and Leather trade Act) Namba 18 ya Mwaka 2008, Sheria ya Ustawi wa Wanyama Namba 19 ya Mwaka 2008 na Sheria ya Utambuzi, Usajili na Ufuatiliaji Mifugo Namba 12 ya Mwaka 2010.


Sheria nyingine ni Sheria ya Nyanda za Malisho na Vyakula vya Mifugo Namba 13 ya Mwaka 2010, na Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo namba 4 ya Mwaka 2012. Akizungumzia ugomvi wa wafugaji kuingiza mifugo katika Pori la Akiba la Swaga Swaga na Msitu wa Jamii wa Mgori, Waziri Mpina amesema Viongozi wa Wilaya wanajukumu la kuyalinda maeneo hayo na wafugaji kuheshimu sheria za nchi. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi , Dkt. Mary Mashingo amesema wataalamu wanatakiwa kushirikiana na kupanga mamna bora ya matumizi ya maeneo hayo ili kuleta tija kwa Sekta zote badala ya kuendelea na migogoro isiyoisha kila uchao.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Luhaga Mpina akiagana na wananchi wa Kijiji cha Handa wilayani Chemba mkoani Dodoma baada ya kutengua maamuzi yaliyofanywa na Halmshauri ya Wilaya ya Singida kutoza faini ya sh. 50,000 kila ng’ombe kinyume cha sheria aliyeko nyuma ya Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Maria Mashingo.


“Wenzetu wa Ethiopia wamefanya vizuri katika kupanga na kutumia maeneo kama haya,sisi kama Wizara tutahakikisha Sheria na Kanuni zinaboreshwa ili kuinua sekta ya Mifugo” alisisitiza Dkt. Mashingo Akitoa taarifa kwa Waziri kuhusu zoezi la kuondoa Mifugo na makazi katika eneo hilo, Mkuu wa Wilaya ya Singida Elias Tarimo amesema kwamba wameamua kufanya operesheni hiyo maalum baada ya wafugaji hao kukataa kuondoka katika eneo hilo kuanzia mwaka 2010 ambapo walianza kuvamia na kufanya makazi,kulima mazao na kuchunga mifugo kinyume cha taratibu.


Alisema Wilaya iliamua kutoza faini kubwa kutokana na hali ya wafugaji hao kuendelea na uvamizi na kuendesha shughuli mbalimbali za ujenzi, ufugaji na kulima, hata hivyo alikiri kutofuata taratibu ya kuendesha zoezi hilo na kwamba watafuata taratibu za kisheria ili tozo hizo zipitishwe katika Mamlaka husika. Aidha alisema operesheni hiyo imekuwa ikishirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kuwa wananchi wamekuwa wakitumia silaha kukataa kuondoka na kuchukuliwa mifugo yao hali ambayo imewafanya waendeshe operesheni hiyo kwa tahadhali kubwa.


Amesema hadi sasa watu 32 wanashikiliwa na Polisi katika kituo cha Singida kutokana na zoezi la kuondoa mifugo linaloendelea, ambapo jumla ya nyumba 138 zimevunjwa na tozo za jumla shilingi 19,750,000/= zimekusanywa. Mkuu wa Wilaya Tarimo amesema jumla ya ng’ombe 386 walikamatwa na Halmashauri lakini hadi sasa wameachiwa baada ya wafugaji hao kulipa faini. Eneo la Pori la Mgori lina julma ya hekta 40000.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad