WILAYA YA MUHEZA, TANGA, TANZANIA – Katika sherehe zilizofanyika katika kijiji kimoja huko mkoani Tanga, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) yaligawa tableti zilizowekewa mfumo wa elimu kwa watoto. Tableti hizo ziligawiwa kama sehemu ya mradi wa majaribio wa miezi 15 chini ya Global Learning XPRIZE, ambao ni mradi wa miaka mitano uliotokana na mashindano duniani yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 15.
Mradi huu wa dunia unatoa changamoto kwa timu za wabunifu kubuni na kuandaa zana- wazi za kiteknolojia ili kuwawezesha watoto walio na fursa ndogo ya kupata elimu katika umri wa miaka tisa hadi kumi na mmoja, kujifunza wenyewe stadi za msingi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK).
Kama sehemu ya majaribio, zaidi ya watoto 2,400 kutoka katika vijiji 167 katika wilaya za Handeni, Korogwe, Lushoto, Mkinga, Muheza, na Pangani watapewa tableti mpya ya aina ya Google Pixel C, zilizotolewa kwa hisani ya Google. Tableti hizo zimewekewa mifumo ya elimu kutoka kwa washindi watano wa mwisho wa Global Learning XPRIZE. Washindi hawa walichaguliwa kutoka katika timu 198 na paneli ya majaji 11 wa kujitegemea na walio wataalamu na kutangazwa mwezi September, 2017 wakati wa wiki ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
“Teknolojia hii inayowawezesha watoto kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu pasipo msaada wa mwalimu, ni ubunifu wa kiwango cha juu kabisa,” alisema Mayasa Hashim ambaye ni Afisa Elimu Mkoa wa Tanga. “Msaada huu utaleta matokeo mazuri katika kuwakomboa watoto walio nje ya mfumo rasmi wa elimu ili kwamba na wao wajifunze stadi hizi.”
Tableti hizo ziligawiwa na WFP kwa sababu shirika hili linasimamia uendeshaji wa kitengo cha lojistiki na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) cha majaribio katika mazingira halisi. Jukumu lake ni pamoja na kuingiza zana hiyo ya kiteknolojia katika tableti, kuanzisha vituo vya kuwekea umeme unaotokana na jua kwenye tableti hizo vijijini na kusimamia matengenezo, marekebisho na kutoa tableti mpya katika kipindi chote cha majaribio ya ugani.
“Ubunifu katika teknolojia unaweza kuwa jibu kwa baadhi ya changamoto kuu duniani,” alisema Mwakilishi wa Nchi wa Shirika la WFP Tanzania Michael Dunford. “Majaribio haya yanamaanisha kwamba tunaweza kutumia teknolojia mpya ili iwahudumie watoto wasio katika mfumo rasmi wa elimu pamoja na watu wengine walio hatarini—na hivyo kuhamasisha uletaji wa maendeleo zaidi katika mchakato huo.
Ubunifu wa aina hii unafungulia milango kwa Serikali, mashirika na biashara kuendeleza katika modeli ambazo zimekwishajaribiwa tayari na kuvunja mwiko wa ukomo katika yale tuliyodhani ndiyo pekee yanawezekana, na si tu katika sekta ya elimu bali pia katika maeneo mengine ya maendeleo ya watu.”
Upande wa elimu katika majaribio ya ugani unasimamiwa na UNESCO kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Vilevile, UNESCO ina wajibu wa kusimamia maendeleo ya watoto katika Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ili kuweza kupima ni zana ya mshindi yupi wa mwisho ilileta matokeo bora zaidi.
“Mradi huu unaendana na majukumu ya UNESCO katika kuhamasisha elimu jumuishi, itolewayo kwa usawa wenye haki na iliyo bora, na wakati huohuo kuchangia kwa kiasi kikubwa katiak juhudi zinazofanywa na wadau mbalimbali wa elimu nchini Tanzania katika kuhakikisha watoto wote, wakiwemo wale wa jamii za pembezoni na zilizo nyonge, kupata fursa sawa katika elimu,” alisema Msimamizi wa UNESCO Faith Shayo.
“Mradi huu unawapa watoto ambao hawakuwahi kujiunga na shule ya msingi pasipo sababu fursa nyingine, huku lengo kuu la kuwapa fursa ya kuingia au kuingia upya katika mfumo rasmi wa elimu ni baada ya kukamilika kwake. Hii inaonyesha juhudi kubwa za pamoja kati ya Umoja wa Mataifa na Serikali ya Tanzania katika kuimarisha viwango vya kujua kusoma na kuandika miongoni mwa vijana wa kizazi kipya nchini kwa kutumia teknolojia zinazotokana na ubunifu, zinazoweza kusambazwa kwa wingi na zenye gharama nafuu. Mradi huu unaweza kupanuliwa na hatimaye kuenewa katika mikoa yote ya Tanzania, ili kuendeleza ujifunzaji katika elimu ya awali.”
Mwisho wa awamu ya majaribio ya ugani, timu ya washindi wa mwisho ambao masuluhisho waliyotoa yana tija zaidi watapata zawadi kubwa ya Dola za Marekani milioni 10. Mshindi atatangazwa mwezi Aprili, 2019. Kufuatia mashindano, kila washindi wa mwisho watano wataweka huru zana zao na maudhui yake ili zipatikane bure na kwa yeyote mwingine kuona namna ya kuzipanua. Inatarajiwa kwamba njia hii ya kujifunza mwenyewe itawaongoza kujifunza na hatimaye kuwawezesha watoto kote nchini Tanzania kuwa na umiliki zaidi wa elimu yao.
Sherehe itafanyika mapema mwaka 2018 ili kuadhimisha kuanza kwa majaribio haya ya ugani. Sherehe hizo zitaandaliwa kwa kushrikiana na Serikali ya Tanzania, UNESCO, WFP na Global Learning XPRIZE.
No comments:
Post a Comment